Natuulinde muungano kwa mabavu!


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version

KWA namna mjadala wa muungano unavyokwenda, ni dhahiri huu ndio wakati hasa kwa Watanzania kupewa fursa ya haki ya kuamua wanachokitaka.

Mjadala mzito huu kuhusu muungano kila mtu anajua kuwa aliyeuchochea si mwingine bali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na majibu aliyoyatoa bungeni kwa swali la Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa (CCM).

Watanzania wanataka fursa sasa kwa sababu wamezuiwa kwa miaka mingi kujadili muungano, na kwa namna wanavyoufahamu. Lakini ni ukweli pia kwamba wapo mamilioni ya Watanzania hawaufahamu muungano wenyewe licha ya kuhimizwa kila mwaka kuzidi kuudumisha.

Ni mara ngapi fukuto dhidi ya muungano limetokea na kuzimwa na watawala kwa kutumia mabavu? Ni bahati mbaya sana kwamba hata viongozi wakuu walipodadisi uhalali wa mwelekeo wa muungano huu, walidhalilishwa na kuporwa mamlaka ya kuongoza.

Kila Mtanzania anakumbuka namna rais wa awamu ya pili wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, pamoja na msaidizi wake mkuu, Waziri Kiongozi, Ramadhani Haji Faki, walivyoondolewa madarakani mwaka 1984.

Walikuwa na hoja ya msingi au hawakuwa nayo, lakini utaratibu uliotumika kuizima, haukuwa wa kiungwana hata kidogo.

Si hivyo tu. Namna Mzee Jumbe alivyosimamiwa katika kulazimishwa kujiuzulu urais wa Zanzibar na nyadhifa nyingine ikiwemo ya umakamu wa kwanza wa rais wa Jamhuri ya Muungano, ilikuwa ni fedheha kwa taifa.

Utaratibu ule wa kuondolewa viongozi wenye ridhaa ya wananchi wa Zanzibar, hakika haukuelekeza taifa katika kuimarisha uhusiano mwema uliokuwepo miongoni mwa nchi na unaokubalika na wengi.

Utaratibu ule ulitofautiana kwa mbali na hatua zilizochukuliwa mwaka 1994 pale utawala ulipokabiliana na mkakati wa wabunge wa upande wa Tanganyika waliounda kundi la G55 kutaka azimio la kurejeshwa serikali ya Tanganyika.

Matukio yote yale; lile la mamlaka ya Zanzibar kutaka muungano unaokubalika na wote au tuseme muungano endelevu, na hili la G55 kudai Tanganyika, yalikuwa ni ya kuipa indhari dola na viongozi wakuu kwamba lipo tatizo linausibu muungano.

Kasoro kubwa ikawa na ingali ni hatua zipi madhubuti za kutatua tatizo. Inazidi kudhihirika kuwa zilikuwa ni hatua za kuahirisha tu tatizo. Yanayotokea tangu wakati ule hadi haya ya sasa, ni matokeo ya kutoziba ufa.

Tanzania inapopita kipindi hiki ni mahali pa kujuta (majuto mjukuu) kwamba viongozi wake wakuu walishindwa na wameshindwa kuziba ufa na sasa wanalazimika kutafuta namna ya kujenga ukuta. Misemo ingali na nguvu hii!

Matatizo yanayoukumba muungano yamekuwa yakielezwa kila mara lakini wakati wote viongozi wamekuwa wakiyafunika kwa kauli za 'tutashughulikia.' Watawala wakabatiza matatizo ya muungano kwa kuyaita ni 'kero.' Pia wakashindwa kuzitafutia ufumbuzi.

Tume na kamati mbalimbali za wataalamu ziliundwa kujadili matatizo ya muungano lakini hakuna cha maana kilichofanywa baada ya mapendekezo kukabidhiwa serikalini.

Hata Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika siku za mwisho za utawala wa Dk. Salmin Amour Juma iliunda tume yake ya kuchambua mwenendo na athari za mfumo wa muungano wa serikali mbili na kutoa taarifa nzuri, lakini hakuna kilichofanywa zaidi ya hapo.

Kabla, mwaka 1992, kulikuwa na mapendekezo ya kihistoria ya Tume ya Nyalali (Francis Nyalali, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye sasa ni marehemu) yaliyotokana na maoni ya Watanzania.

Tume hiyo ilieleza wazi kuwa pamoja na raia wengi kupendelea mfumo wa muungano wa serikali mbili, masharti au kasoro walizozitoa kuuimarisha muungano, iwapo zingetekelezwa, ingekuwa na maana ya kuwepo serikali tatu.

Rai hii ilijitokeza hata katika maoni ya wananchi juu ya Waraka Namba 1 (White Paper) wa mwaka 1999 uliokuwa unazungumzia mahitaji ya marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Haya, yananikumbusha mwaka 1992 wakati Jaji Nyalali alipofika Zanzibar na kufungua Kituo cha Huduma za Sheria cha Zanzibar (ZLSC) kilichoanzishwa na maprofesa Haroub Othman, Chris Peter Maina na wenzao, alipata kusema:

Tanzania haijawahi kuwa na maadili thabiti ya taifa kama ilivyo nchi kama Marekani. Tunahitaji kuwa nayo baada ya majadiliano makini. Ni vema maadili ya taifa letu yajulikane na kutangazwa kwamba haya na haya ndiyo mambo tunayokubaliana kuyazingatia na kuyafuata. Kila Mtanzania atayafuata hata akitoka chama gani na kuunda serikali. Umuhimu wa maadili ya taifa unazingatia ukweli kuwa yanabaki hivyo daima dumu.

Watawala walimuelewa lakini, kwa sababu za binafsi, au tuseme kwa sababu wanazozijua wao, hawakutilia mkazo ushauri wake na hawakutekeleza chochote hadi sasa.

Ndio ukweli kwamba Tanzania inakosa muongozo kama taifa katika karne ya 21. Ni taifa linaloendeshwa tu lakini hakuna mambo mahsusi yanayounganisha wataifa wake. Waingereza wanaongozwa na mfumo wa kifalme. Tanzania ni upi wakati ujamaa na kujitegemea umebezwa?

Pengine muungano waliouasisi viongozi waliopendwa ungekuwa mahali pazuri pa kuanzia. Ungetumika kuandika maadili haya tusingesikia kero na zingetokea, zingetatuliwa kirahisi maana ipo misingi murua ya kuitatua.

Leo muungano ulioasisiwa kwa msingi wa kikatiba na sheria, unadhoofika kila leo huku Zanzibar wakilalamika wanaonewa lakini wenzao wanasema 'mhh na hawa wenzetu wamezidi ulalamishi.'

Je ni ulalamishi kweli au mtu lazima adai haki yake? Ni swali jepesi kulipuuza lakini kwa hali ilivyo, ni zito ambalo majibu yake hayawezi kupatikana kwa watawala kuendelea kuamini kuwa kujadili utata wa muungano ni haki ya kipekee kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) tu.

Nini "bwana" CCM mbele ya Watanzania? Tanzania si ya CCM bali ya Watanzania wote bila ya kujali misimamo yao ya kisiasa. Imani kwamba muungano ni suala la kisiasa ndiyo inayoponza taifa.

Ukweli, muungano ni suala la kikatiba na kisheria. Sasa iweje jamhuri haitaki kutoa hati ya Mkataba wa Muungano bali ihimize muungano ulindwe kwa nguvu zote? Muungano wa mabavu haujadumu popote duniani.

0
No votes yet