Nazir Karamagi "ajinyonga"


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati  na Madini, Nazir Karamagi

ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi "amejinyonga." Hawezi kupata kile alichoahidi kukitoa bungeni. Chenyewe, kwa mujibu wa Sheria na Katiba, ni siri isiyotoleka hadharani, MwanaHALISI limeelezwa.

Karamagi anatakiwa kulithibitishia Bunge la Jamhuri ya Muungano, kauli yake kwamba uamuzi wa kuiongezea mkataba kampuni yake ya Kupakua na Kupakia Mizigo bandarini (TICTS), ulifanywa na Baraza la Mawaziri.

Akichangia hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi, Karamagi alijiingiza kitanzi na kusababisha mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah, kuomba mwongozo wa Spika akitaka Karamagi athibitishe kauli yake hiyo.

Akizungumza huku akitolea macho Karamagi, Anna alisema, "mshehimiwa Spika, wakati haya yanafanyika, Karamagi hakuwa waziri, sasa aliyajuaje hayo."

Taarifa kutoka ndani ya Bunge zinasema kwamba kwa hali ilivyo, Karamagi hawezi kukwepa kibano. "Kwa vyovyote vile, Karamagi hawezi kunusurika," anasema Afisa mmoja mwandamizi wa Bunge.

"Akileta ataulizwa, amepata wapi? Aliyajuaje haya wakati yeye hakuwa waziri. Nani aliyempa siri za vikao vya ndani, wakati vikao hivi ni vikao vya siri," amesema mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema, "kwa kufanya hivyo, Karamagi atakuwa amethibitisha kwa umma, kwamba uamuzi wa kuiongezea mkataba TICTS ulifanywa kwa shinikizo kutoka Ikulu."

Miongoni mwa matamshi katika hati ya kiapo kwa mawaziri wa Serikali nchini, ni kuahidi kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kulinda siri za Baraza la Mawaziri.

Tayari Spika wa Bunge, Samwel Sitta, ameshatamka kuwa iwapo Karamagi atashindwa kuwasilisha uthibitisho wake hadi Ijumaa hii, atalipeleka suala hilo kuamuliwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ni Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same.

Septemba 6, mwaka 2005, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, alimuandikia waraka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya, akisema "Mheshimiwa Rais (Benjamin Mkapa) ameagiza Wizara ya Mawasiliano, hususan Mamlaka ya Bandari, kutekeleza mambo matatu.

"Moja: TICTS waruhusiwe kutumia Berth Na. 8 na ardhi ya karibu naye."
"Pili: Matumizi ya Ubungo Container Depot kuhifadhi mafuriko ya makontena yanayotokana na kuongezeka kwa ufanisi."
"Tatu: Muda wa mkataba uongezwe kuwa miaka 25."

Barua ya Mramba ndiyo inayozua utata zaidi. Ni kutokana na kuwa aliyetoa agizo lililoruhusu mkataba wa TICTS kuongezewa muda wa miaka 15, kutoka ile 10 ya awali, ni kiongozi mstaafu, Mkapa, ambaye tayari anatuhumiwa kwenda kinyume na maadili ya uongozi wa umma.

Imefahamika pia kwamba wakati Mramba na Karamagi wakiidhinishiana mkataba mpya, tayari Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 ilishapitishwa.

Sheria hiyo inataka kuwapo kwa ushindani katika zabuni. "Kama serikali ilitaka kuiongezea TICTS mkataba, ilipaswa kutangaza zabuni na kuruhusu ushindani kutoka kwa makampuni mengine," anasema kiongozi mmoja mwandamizi katika serikali.

Taarifa zaidi zinasema kwamba kwa ustadi wa hali ya juu, Karamagi alifanikiwa kupenyeza kwa wabunge nyaraka "tata" ndani ya nyaraka halali za Bunge.

"Ilikuwa ni asubuhi ya 24 Aprili 2008, Karamagi alituma mtu katika Idara ya Uchapaji (ya Bunge) akidai 'ameagizwa na Waziri kumtolea kopi.' "Mtu huyo alishindwa kumtaja waziri," alisema kiongozi mmoja wa Bunge.

Uchunguzi wa MwanaHALISI unaonyesha kwamba mara baada ya nyaraka hizo kurudufiwa, nakala ziliwekwa kwenye sanduku katika eneo linalowekwa nyaraka za kila siku za shughuli za Bunge (order paper).

"Vijana walipoagizwa wakaziweka kama walivyotakiwa. Spika alipoulizwa, alikubali baada ya kuambiwa kwamba zilitumika katika Kamati ya Bunge ya Miundombinu," mbunge mwingine aliliambia MwanaHALISI.

Anasema, baada ya uongozi wa Ofisi ya Bunge kupata taarifa hiyo, haraka iliagiza uchunguzi kufanyika. "Nusura wafanyakazi wa Bunge wafukuzwe maana jambo hili halikuwa dogo. Ni jambo zito na linalotia aibu Bunge."

Uchunguzi wa MwanaHALISI umegundua kuwa nyaraka ambazo Karamagi alizichomeka kwa Bunge, hazikuwa zimesainiwa na mtu yeyote, jambo linalothibitisha kwamba zilitolewa kimbinu.

Vilevile inasemekana Karamagi aliambatanisha nyaraka nyingine inayofanana na ile inayotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LART) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC).

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge, kamati hizi pekee ndizo zinazoandika maelezo yake kwa mfumo wa Hansard.

Imebainika pia kwamba nyaraka ambayo Karamagi aliiwasilisha, haikuandikwa na Bunge, bali na TICTS, jambo linalothibitisha madai ya wengi kwamba ilichomekwa.

Katika hoja yake mbele ya Bunge, Zambi alitaka serikali ivunje mkataba kati yake na TICTS kutokana na malalamiko mengi ya wadau mbalimbali juu ya utendaji wa kiwango cha chini wa shughuli za upakizi na upakuaji wa makontena pamoja na kiwango cha uwekezaji kilichofanywa na kampuni hiyo kuwa chini ya kile kilichokubaliwa kwenye mkataba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: