NCCR ipi ya kushikamana na CUF leo?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
James Mbatia na Ibrahim Lipumba

TAZAMA picha hii: Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia wamesimama pamoja jukwaani. Mikono yao miwili imeshikamana. Profesa ndiye ameshika mkono wa kushoto wa Mbatia kwa kutumia mkono wake wa kulia. Ameuinua juu na anapiga mayowe ya mshikamano.

Profesa Lipumba ni mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) na Mbatia anaongoza NCCR-Mageuzi.

Kutokana na picha hii, iliyopigwa Machi 25 kwenye uwanja wa Demokrasia uliopo Kibandamaiti, mtaa wa Mikunguni, mjini Zanzibar katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CUF, nahisi inawaumiza wanachama wa CUF, na hasa wa Zanzibar ambako NCCR-Mageuzi hakisahaulika kilivyoifanyia CUF Mei 2003.

Wakati huo, kulifanyika uchaguzi mdogo wa majimbo ya Pemba, na CUF, chama chenye ngome isiyovunjika kwa Pemba na tishio kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kilitaka kuendelea kulinda ngome hiyo ya Pemba iliyokuwa ikinyemelewa sana na CCM.

Uchaguzi huo ulitokana na azimio la Bunge kuwavua ubunge wabunge wa CUF katika majimbo kadhaa, kwa madai kuwa walikosa sifa ya kuendelea kutumikia nafasi hiyo baada ya kususia vikao. Hali hiyo ilitokana na mgogoro walioutangaza mara baada ya kuvurugwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Mgogoro huo uliosababisha mauaji ya zaidi ya raia 30 waliokuwa katika maandamano ya amani yaliyoitishwa nchi nzima na CUF, ulitulizwa kwa muafaka uliofikiwa baadaye. Uchaguzi mdogo uliitishwa ili kujaza viti vilivyokuwa wazi kisiwani Pemba.

Wakati wa uchaguzi huo, NCCR-Mageuzi iliwekea pingamizi wagombea wa majimbo matano wa CUF kwa madai ya kutokuwa na sifa za kugombea. Tume ilizikubali pingamizi hizo na ikawaengua wagombea hao.

Kinyang’anyiro kikabaki kwa CCM na NCCR-Mageuzi, chama ambacho hakitimizi hata matawi matatu yenye wanachama hai kisiwani Pemba.

Kampeni ya NCCR-Mageuzi ilikuwa ya aina yake na ilivuta wananchi wengi hadi kwenye mikutano yake ya hadhara ambayo maandalizi yake yalionyesha chama hicho kiliwekeza sana.

Ikumbukwe kwamba NCCR-Mageuzi ilipoteza udhibiti wa siasa nchini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 kufuatia mgogoro wa uongozi uliokikumba chama hicho katikati ya miaka ya 1990.

Na wakati kikitia fedha nyingi kutafuta viti kule kisikokuwa na wanachama, kilipoteza kiti chake cha Kigoma Kusini ambako aliyekuwa mbunge wake, Kifu Gulamhussein Kifu, alitaka kurudi bungeni baada ya mahakama kutengua ushindi wake.

Uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kuengua wagombea wa CUF uchaguzi mdogo wa majimbo ya Pemba, uliipa CCM njia rahisi ya kutwaa viti vilivyogombewa kwa kuwa CUF haikuwa tena na wagombea, na NCCR-Mageuzi, haikuwa na ngome.

Ni katika uchaguzi huo, uliibuka msamiati mpya katika siasa za Tanzania wa “Kura za maruhani” ambao ungali unakumbukwa mpaka leo. Msimiati huo ulitokana na uamuzi wa wananchi kupiga kura zao kwa walewale wagombea waliosimamishwa na CUF na ambao walikuwa wameenguliwa na Tume ya uchaguzi kwa kudaiwa walikosa sifa za kugombea.

Majina ya wagombea wale yalifutwa katika orodha ya wagombea lakini penye nafasi zao katika karatasi ya kupigia kura yalibaki huku kwenye picha zao kukiwa na kivuli. Wananchi walipiga kura zao hapo kwenye kivuli.

Kura hizo zilikuwa nyingi kwa idadi kuliko zile halali zilizopigwa kwa wagombea wa CCM na NCCR-Mageuzi, lakini, kwa vile Tume iliwaengua wagombea wa CUF kutokana na pingamizi za NCCR-Mageuzi, wagombea wa CCM ndio waliotangazwa washindi kwa kupata kura zaidi ya wale wa NCCR-Mageuzi.

Ile ilikuwa ni staili ya aina yake katika demokrasia ya Tanzania. Kwamba awananchi wanapiga kura za hasira na kumpa mgombea waliyemtaka licha ya kuwa alienguliwa na tume ya uchaguzi.

CUF ilikosa viti vile na vikatwaliwa na CCM, hasimu wake mkubwa kisiasa Zanzibar. Chimbuko la matokeo yale, si kitu kingine isipokuwa NCCR-Mageuzi kilichowawekea wagombea wa CUF pingamizi.

Mpaka leo imebaki kwenye kumbukumbu kwamba CUF walionewa kwani Mahakama Kuu ilikuja kutengua maamuzi ya Tume yaliyoengua wagombea wake. Kwa ufupi, uamuzi wa tume kuengua wagombea wa CUF ulikuwa batili kisheria. Hata hivyo, kwa kuwa maamuzi ya mahakama yalichelewa sana, hakuna manufaa iliyopata CUF.

Tukio hilo lilitokea wakati CUF na NCCR-Mageuzi, vilikuwa katika ushirikiano pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Tanzania Labour Party (TLP).

Kwa upande mwingine, tukio hilo lilikoleza uhasama wa kisiasa kati ya CUF na NCCR-Mageuzi, chama kilichoonekana kutumiwa na CCM.

Ushirikiano wa CUF na CHADEMA ulishika kasi hadi mwaka 2005 ulipoingia dosari katika baadhi ya majimbo ambako vyama hivyo vilishindwa kuachiana kwa kila kimoja kilipokuwa na nguvu. Uhasama ukazidi mwaka 2008 wakati wa uchaguzi mdogo baada ya kifo cha Chacha Wangwe, aliyekuwa mbunge wa CHADEMA jimbo hilo.

CHADEMA ilitaka kutetea kiti hicho walichoshinda 2005 huku CUF ikimteua Charles Mwera aliyekuwa amehama CHADEMA, chama ambacho ndicho kilichompatia uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kabla ya kuhama baada ya kutoteuliwa kugombea 2005.

Sasa ngoma imegeuka. Vuguvugu lililoanzishwa na CHADEMA Septemba 2007 kwa kuikalia kooni CCM, lilileta nguvu kubwa na chama hicho kikapata mafanikio katika uchaguzi wa Oktoba 2010. CHADEMA imeteka hata ngome za CUF.

Upinzani kwao umefikia hatua mbaya ya kutengana katika uundaji wa kambi ya upinzani bungeni. CHADEMA, kilichopata kura nyingi zaidi ya CUF – kilichokuwa kinashikilia serikali kivuli tangu uchaguzi wa mwaka 1995 – kimeunda serikali kivuli ya peke yao kikiiacha pia NCCR-Mageuzi, TLP na United Democratic Party (UDP cha John Cheyo.

Hayo yakaibuwa upinzani wa kushangaza kati yao na hali ikawa mbaya zaidi pale CUF – na hasa ushawishi wa Hamad Rashid Mohamed, mwanasiasa wake mkongwe na mbunge wa Wawi aliyekuwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni – alipotaka kulazimisha CHADEMA ishirikiane na NCCR-Mageuzi pamoja nao katika kuunda serikali kivuli.

Haieleweki katika mazingira gani CUF inaamua leo kujenga uswahiba wa kisiasa na NCCR-Mageuzi, kile kilichowakosesha tonge mdomoni mwaka 2003 kilipowekea pingamizi wagombea wao waliokuwa na uhakika wa asilimia 100 kushinda.

Ndipo kunakuja swali uswahiba huu umeanzaje? Kwamba NCCR-Mageuzi wamebadilika kwa lipi kutoka ukorofi walioonyesha 2003 dhidi ya CUF? Kwamba NCCR-Mageuzi inaweza kutoa mchango gani kuiwezesha CUF kurudisha udhibiti kwenye maeneo mbalimbali Tanzania Bara yaliyodhoofishwa kutokana na nguvu waliyojenga CHADEMA?

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: