Nchi kuingia gizani tena


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

NCHI inaweza kuingia gizani wakati wowote kuanzia sasa, kutokana na kupungua kwa uzalishaji umeme, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema uzalishaji umeme unaoingia katika gridi ya taifa umepungua kwa kiasi kikubwa na tayari athari zake zimeanza kuonekana kwa mgao wa kimyakimya.

Hali hiyo imechangiwa na kukwama kwa mpango wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wa kukopa Sh. 408 bilioni kwa ajili ya kununua mitambo ya dharura na mafuta ya kuzalisha umeme.

Vyanzo vya taarifa ndani ya Tanesco vimesema kuchelewa kwa mkopo ulioombwa City Bank, kunatokana na serikali kushindwa kutoa udhamini kwa wakati mwafaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Injinia William Mhando alipoulizwa kwa simu juzi, alisema mkopo huo umechelewa kutokana na masuala ya kisheria.

Alisema, “Wanasheria wa serikali na wale wa City Bank walikuwa hawajaelewana katika maeneo fulani, lakini kesho (jana) tutafanya nao kikao na nina matumaini sasa tutafikia mwisho. Huenda mkopo huu sasa ukapatikana wiki hii.”

Kwa zaidi ya mwezi sasa kumekuwa na mgao wa umeme wa kimyakimya katika jiji la Dar es Salaam na mikoa inayopata umeme kutoka gridi ya taifa.

Mgao huo, zimeeleza taarifa, umesababishwa na kupungua kwa umeme kati ya megawati 120 na 130 katika gridi ya taifa, kila siku asubuhi na jioni, wakati matumizi ya nishati hiyo yanakuwa makubwa.

Kuhusu hali ya mgao wa kimyakimya, Mhando amesema, katika siku za karibuni kumekuwa na tatizo la gesi, na sasa tatizo limekuwa kubwa kutokana na mvua kuangusha nguzo nyingi za umeme.

Katika hatua nyingine, uzalishaji umeme kwa kutumia nguvu za maji, nao unazidi kuwa mgumu kutokana na kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa yanayosimamiwa na shirika hilo.

Taarifa za ndani ya Tanesco zimesema hali ya upungufu wa umeme imefikia “hatua mbaya na mgao mkubwa nchi nzima sasa haukwepeki.”

Kwa mujibu wa habari hizo, uzalishaji umeme katika mabwawa yote makubwa ulikuwa wa chini kutokana na upungufu wa maji na kwamba hata zikinyesha mvua kipindi hiki uimarikaji wa kina utachukua muda.

Vilevile, uzalishaji umeme katika mitambo ya dharura, kama  Symbion, Dodoma - 50 MW, Aggreko, Ubungo - 50 MW, Aggreko, Tegeta - 50 MW, ulisimama kutokana na ukosefu wa  mafuta na gesi.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, uzalishaji katika mtambo wa Symbion uliopo Ubungo, umepungua kutoka megawati 112.5 hadi megawati 55 kutokana na ukosefu wa mafuta.

Mikataba ya uzalishaji umeme kati ya Tanesco na makampuni binafsi (EPP) inaweka wazi kwamba shirika hilo ndilo linalopaswa kutoa mafuta ya kuendeshea mitambo.

Lakini, hali yake kifedha ni mbaya kiasi cha kushindwa jukumu hilo.

Wakati hali hiyo ikiendelea, Machi 6, mwaka huu, transfoma ya pili katikati ya Jiji la Dar es Salaam iliharibika na kufanya hali kuwa mbaya zaidi. Transfoma ya kwanza iliharibika tangu Januari mwaka huu.

Hata hivyo, Mhando amesema tatizo hilo la katikati ya jiji lilipata ufumbuzi wa muda hapo  8 Machi 2012 kwa kuunganisha umeme kutoka kituo cha Makumbusho.

“Unajua, transfoma hizi zimekaa pale kwa zaidi ya miaka 30 sasa; muda wake wa kufanya kazi umeisha. Aidha, miundombinu mingi ya Tanesco inahitaji marekebisho makubwa,” amesema Mhando.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari, wataalam wa umeme kutoka kampuni ya ABB ya jijini Dar es Salaam wanafanya tathmini kuona iwapo transfoma hizo mbili zinaweza kukarabatiwa.

Shughuli hiyo inakadiriwa kuchukua muda wa wiki nne.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Tanesco imeanzisha mchakato wa kununua transfoma mpya kutoka kampuni ya Tanelec ya hapa nchini, ambazo zitachukua kati ya wiki sita na nane kupatikana.

“Ununuzi wa transfoma mpya au kukamilika kwa ukarabati wa transfoma hizo mbili, ndio utakuwa ukombozi kwa maeneo ya katikati ya jiji...maana umeme wa Makumbusho ni ufumbuzi wa muda tu,” alisema mpashaji habari.

Taarifa za uhakika zimeeleza kuwa sehemu kubwa ya nchi inayopata umeme kutoka gridi ya taifa, inatarajia kuwa gizani kwa saa 13, Jumamosi na Jumapili wiki hii, kutokana na kusimamisha mitambo ya Songas kwa ajili ya ukaguzi.

Habari za Songas zinasema kampuni ya Pan African Energy (T), itakuwa inafanya ukaguzi wa mitambo yake ambao hufanyika kila mwaka. Ukaguzi utaanza saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 usiku.

Mgao huo ambao vyanzo vyetu vimesema utatangazwa kwenye vyombo vya habari wakati wowote sasa, utasababisha uzalishaji wa umeme wa Songas usifikie megawati 150 zinazozalishwa kila Jumamosi na 112 zinazozalishwa kila Jumapili.

0
No votes yet