Nchi yaingia gizani


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete atajikuta akiongoza taifa gizani siku chache kutoka sasa, MwanaHALISI limeelezwa.

Tayari wachunguzi wa mambo wanasema, kama hali itakuwa hivyo, mauaji na vitendo vingine vya uhalifu vilivyoanza kujitokeza, vitashamiri zaidi katika maeneo yatakayoingia gizani.

Taarifa za uhakika ndani ya serikali na Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO zinasema:

  • TANESCO inaelekea kufilisika
  • Mabwawa ya kuzalisha umeme karibu yaishiwe maji
  • Hakuna fedha za kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha maji
  • Makampuni ya mafuta yanameza karibu kiasi chote kinachokusanywa<
  • Presha au mkandamizo wa gesi inayotoka Songosongo ni mdogo

Tayari rais ameambiwa kuwa mgao wa umeme umeanza. Ulianzia mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Mwanza, Mbeya na Shinyanga.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Jenerali mstaafu Robert Mboma, mgao ulianza 10 Julai 2012.

Siku hiyo mgao ulianza saa 1.10 jioni hadi 5 usiku na uliongezeka siku iliyofuata kwa kuanzia saa 6 usiku hadi saa 12 asubuhi.

Katika taarifa rasmi kwa rais, Jenerali Mboma amesema, “…tumeanza kutoa mgawo wa umeme kwa megawati 64.5 mikoani nchi nzima isipokuwa Dodoma.”

Jenerali Mboma anasema katika barua yake ya 11 Julai 2012 aliyomwandikia rais kupitia katibu wake, Prosper Mbena, kuwa alichelewa kupeleka ujumbe huo kwa vile hakujua baruapepe ya Mbena.

Anasema katika mikoa ambako mgao ulianzia ilikuwa Tanga megawati 10.9; Kilimanjaro MW 8, Arusha MW 14, Morogoro MW 5.2, Mwanza MW 10, Mbeya MW 9 na Shinyanga MW 7.4.

Mboma anasema kwa tarehe 11/7/2012 uzalishaji kwa kutumia maji ungekuwa MW 151.6 na  gesi 291.

Anasema hata hivyo, IPTL na Symbion (Dodoma) wangetoa MW 60 tu kwa sababu “TANESCO hatuna fedha ya kuwalipa wanaotudai na tumeshindwa hata kuwanunulia mafuta ya kuendesha mitambo yao.”

Serikali iliahidi bungeni mwaka wa fedha uliopita, kuipa TANESCO mkopo wa Sh. 408 bilioni ili kujiendesha. Hata hivyo Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ameliambia bunge kuwa serikali imefuta mpango wake wa kuidhamini TANESCO.

Bali Mboma anasema ni muhimu fedha hizo kupatikana kwani kutawezesha mitambo ya mafuta kufanya kazi na hivyo kuifanya Mtera na Kidatu kubaki na maji ya kutosha hadi Desemba 2012.

Anasema upo umuhimu wa pekee kwa mitambo ya maji kuwa na maji ya kutosha kwa sababu mitambo mingine (ya gesi na mafuta) ikizima ni lazima iwashwe na mitambo ya umeme inayotumia maji.

Katika andishi hilo, Mboma anasema, iwapo mgawo wa umeme utaendelea basi litakuwa janga ambalo “litaathiri upitishaji bajeti ya wizara ya nishati na madini.”

Hakueleza jinsi bajeti itakavyoathirika, lakini inatarajiwa wabunge watang’aka na kusakama wizara na waziri kwa madai ya kushindwa kazi.

Tangu bunge la bajeti lianze mwaka huu, umeme umekatika mara mbili, huku wabunge wakiachwa gizani; tena kwa vipindi virefu kabla jenereta kuwashwa.

Angalau bunge limelazimika kuahirisha shughuli zake mara moja kutokana na kukatika kwa umeme. Wachunguzi wanahoji itakuwaje pale wabunge watakapowekwa kwenye mgao.

Jenerali Mboma amemwandikia pia Profesa Muhongo akieleza kuwa TANESCO haiwezi kulipa madeni iliyoamriwa na makampuni ya kuzalisha umeme na kumwomba ahakikishe serikali inawapatia “mapema sana fedha walizoahidi.”

Katika barua yake ya Jumanne 10 Julai 2012, Mboma anasema, “Rejea maagizo yako ya kunitaka nifanye kila njia kuwalipa Songas, Pan Africa Energy na wengineo.

“Nakiri kuwa tunadaiwa na makampuni hayo na kwa ujumla wake mpaka sasa tunadaiwa jumla ya dola za Kimarekani milioni 270. TANESCO haina hela na hivyo kwa sasa haina uwezo wa kulipa,” ameeleza.

Taarifa ndani ya TANESCO zinadai kuwa Mboma aliandika barua kwa rais na waziri baada ya kuarifiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando juu ya hali mbaya ya uzalishaji umeme nchini.

Hivi sasa Mhando amesimamishwa kazi na bodi ya wakurugenzi kwa kilichoitwa kuchunguzwa kwa madai ya ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Lakini katika hali isiyotarajiwa, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Eliakim Maswi amemjibu Mboma kwa “njia ya ukali.”

“Gen. Rtd. Mboma, nimeona barua yako kwenda kwa Mheshimiwa Waziri…Tatizo kubwa ni unakusanya Sh. 75 bilioni kwa mwezi, unalipa mishahara na kiasi kinachobaki kilitegemewa kulipa madeni angalao kwa mpango maalum ili kuondoa kila mdai kulalamika.

Katika mawasiliano yake ya Jumatano 11 Julai 2012, Maswi anasema, “Lakini hakuna deni  linalolipwa na madai yanaongezeka. Nani anatumia fedha hizo…? Anahoji.

“Nitapenda kuona mpango wa malipo kwa wanaotudai na jinsi ya kuwalipa. Sitaki kusikia  kisingizio cha kutopata mkopo. Hivi kweli kila kitu ni mkopo wa shilingi bilioni 408?,” anauliza Maswi.

Habari za ndani ya TANESCO zinasema shirika hilo lina madeni yanayofikia Sh. 500 bilioni.

Kamati ya bunge ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Zitto Kabwe, inatarajiwa kukutana leo na bodi ya wakurugenzi ya TANESCO kwa kilichoitwa kupata maelezo zaidi juu ya hatua ya kumsimamisha kazi Mhando na wenzake watatu.

0
No votes yet