Nchimbi aingizwa kikaangoni Songea


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version

DURU za kisiasa mkoani Ruvuma zinaonyesha kwamba kuna wanasiasa ambao tayari wameanza harakati za maandalizi za kuwania Jimbo la Songea Mjini. Wamo  aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Oliver Mhaiki, wabunge wa Viti Maalum,  Devotha Likokola na Injinia Stela Manyanya .

Hakuna aliyetoa kauli za hadharani za kuingia katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo. Lakini taarifa zinazopatikana kutoka kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mashabiki wa wanasiasa hao zinatoa mwelekeo wa ukweli wa mambo, wa kuliwania jimbo hilo.

Likokola anapoulizwa anasema kuwa  hajawahi kutamka kwa mtu yeyote kwamba anahitaji kugombea Songea Mjini. Kauli hiyo hiyo imetolewa na Manyanya.

Jimbo la Songea Mjini ni miongoni mwa majimbo sita ya uchaguzi yaliyopo katika Mkoa wa Ruvuma . Hivi sasa linawakilishwa Emmanuel John Nchimbi wa CCM.

Majimbo mengine ni Namtumbo, ambalo mbunge wake ni Vita Kawawa, Peramiho, linalowakilishwa na Jenista Mhagama, Mbinga Magharibi ambalo mbunge wake ni Kapteni John Komba.

Majimbo mengine ni Tunduru ambalo mbunge wake ni Mtutura Mtutura na Mbinga Mashariki linalowakilishwa na Gaudence Kayombo. Wote hao ni wabunge wa CCM.

Nchimbi alichaguliwa kuwa mbunge wa Songea Mjini baada ya kumshinda Dk. Lawrence Gama katika kura za maoni za CCM zilizofanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2005.

Hata hivyo, Nchimbi ana kibarua kigumu hivi sasa. Kuna kero nyingi zinazowakabili wapiga kura wake. Zinamweka katika wakati mgumu, na hasa wakati jimbo hilo linakodolewa na wanasiasa wengi.

Wakazi wa kata kadhaa wanashindwa kuficha hisia zao dhidi ya Nchimbi. Ni kutokana na kutokuonekana jimboni na kushindwa kutekeleza ahadi alizotoa kwa wapiga kura wake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2005. 

Malalamiko dhidi yake yanajidhihirisha katika kata za Mshangano, Namanditi, Ruhuwiko, Mletele, Lizaboni na Msamala. Wanalalamika kuwa wamesahaulika katika kutatuliwa kero zao kubwa za maji, umeme na afya.

Wakazi wa maeneo hayo wanamtaka mbunge wao asikie na atekeleze ahadi zake alizoziahidi wakati wa kampeni.

Mkazi mmoja wa Mshangano ndani ya Jimbo la Songea Mjini, Samsoni Komba, anasema licha ya mbunge huyo kutokuwatembelea katika maeneo yao na kujua kero zinazowakabili, pia amekuwa hasikiki bungeni.

“Hajatusemea wala kutuletea maendeleo kama alivyotuahidi. Hali hiyo inatufanya tuamini kuwa unaibu waziri alioupata katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na sasa katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ndivyo vikwazo. Vinasababisha asitekeleze vizuri wajibu wake aliopewa na wapiga kura baada ya kuomba yeye mwenyewe,” anasema Komba.

“Kwa kweli tumechoka. Mbunge wetu ameshindwa kututatulia kero ya maji, umeme na huduma za afya katika kituo cha afya kilichopo Mjimwema. Ameshindwa kuitisha hata mkutano wa wananchi tangu  alipochaguliwa,” anasema Hamza Uonjo, mkazi mwingine wa jimbo hilo.

Kituo cha Afya cha Mjimwema kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa wahudumu, vitanda, dawa na vifaa-tiba vingine. Hata umeme sio huduma ya uhakika. Umeme unapokatika hakuna vipimo vinavyotolewa kwa wagojwa.

Inafikia hatua daktari anamwandikia dawa mgonjwa kulingana na maelezo yake aliyoyatoa na kisha hupewa dawa bila vipimo kutokana na tatizo sugu la umeme.

Wananchi wamehojiwa. Wanatoa kilio chao kwa Nchimbi. Wanamtaka kuboresha  huduma za afya kwani ni mmoja ya matatizo sugu katika jimbo lao.

Huduma ya maji nayo ni mbaya. Adha kubwa inayakumba maeneo yaliyopo  katikati ya Mji wa Songea. Lakini ni kubwa zaidi kwenye maeneo ya pembezoni mwa Jimbo la Songea Mjini. Hali ni mbaya katika kata za Ruhuwiko, Subira, Mletele, Lizaboni, Msamala na Mshangano.

Zuhura Hamidu, mkazi wa Mletele anasema wanaamka saa 11 asubuhi kwenda kusaka maji umbali wa zaidi ya kilomita mbili. Kwamba hali hiyo inawaletea adha kubwa kiafya kutokana na kubeba mizigo mizito na kutembea umbali mrefu

Lakini pia anasema adha hiyo inawaathiri kiuchumi kwa kuwa muda mwingi wanautumia kusaka maji kuliko kufanya kazi za kimaendeleo.

Ukiweka kando tatizo la maji, jimbo la Songea Mjini, kama yalivyo majimbo mengine, linakabiliwa na tatizo sugu la umeme.

Ally Swai, mkazi wa kata ya Mjini, ambaye ni fundi wa kuchomea vyuma, anasema huduma ya umeme katika Manispaa ya Songea sio ya uhakika. Mara kwa mara umekuwa ukikatika na kusababisha adha kubwa. Kazi zinazotumia nishati hiyo husimama na kudumaza kipato.

Katika sekta ya miundo mbinu ya barabara za Manispaa ya Songea hali pia ni mbaya. Zile zilizowekwa lami mwishoni mwa miaka ya 1970 zimeharibika.

Kwa vyovyote vile, lawama za wananchi kwa Nchimbi zinamweka katika kikaango. Hii inatokana na nafasi ya ubunge anayoishikilia inakodolewa kwa hamu na wanasiasa na makada wengine wa CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: