Ndiyo, Twiga Stars iko kundi la kifo


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version

KOCHA mkuu na meneja wa timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, wameeonyesha kukasirishwa na uchambuzi wa vyombo vya habari kwamba timu hiyo imepangwa kundi la kifo katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini mwezi ujao.

Wanasema habari hizo ni za kukatisha tamaa. Charles Boniface Mkwasa, ambaye ni kocha mkuu anasema hadhani kama timu hiyo iko kundi la kifo.

Furaha Francis, ambaye ni meneja wa timu hiyo anasema timu inaendelea vizuri na mazoezi na kwamba itafanya maajabu katika michuano hiyo.

“Wengi wanasema ooh, sijui tumepangwa kundi gumu. Mimi nasema mambo hapa yanaendelea vema, mimi nasema subirini muone mambo,” alisema Furaha.

Furaha amewataka wapenzi wa soka nchini kuendelea kuiunga mkono timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika michuano hiyo kwani tayari baadhi ya wadau wamekata tamaa.

Mkwasa na Furaha wanataka kuanzisha malumbano na waandishi wa habari pasipo na msingi wowote. Ukweli utabaki Twiga Stars iliyopangwa Kundi A pamoja na Mali, Nigeria na wenyeji Afrika Kusini iko kundi la kifo.
Uzoefu

Mara kadhaa Twiga Stars imekuwa ikipangwa katika mechi za awali dhidi ya Eritrea na Ethiopia, lakini kila ikijaribu kuvuka hatua ya pili imekuwa ikishindwa. Mara ya mwisho iling’olewa na Zimbabwe.

Twiga Stars ina wachezaji wazuri, wanaovutia dimbani lakini ukweli haina uzoefu wa kimataifa ikilinganishwa na Nigeria na Afrika Kusini.

Nigeria ndiyo yenye mafanikio makubwa katika kundi hilo kwani imewahi kutwaa ubingwa huo mara tano, wakati Twiga Stars inashiriki kwa mara ya kwanza.

Nigeria, mbali ya kushiriki takriban kila fainali, hizi zikiwa za saba, imekuwa ikishiriki fainali za Kombe la Dunia sawa na Ghana iliyoko Kundi B.

Timu nyingine zilizoko Kundi B pamoja na Ghana ni mabingwa watetezi Equatorial Guinea, Algeria na Cameroon.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo kila timu itakutana na nyingine hatua ya makundi na timu mbili za kwanza kutoka katika kila kundi zitacheza hatua ya nusu fainali na kisha fainali.

Michuano hiyo ya fainali inatarajiwa kuanza Oktoba 31 hadi Novemba 14 kwenye viwanja vya Sinaba mjini Daveyton na Makhulong mjini Tembisa.

Washindi wataiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake zitakazofanyika kuanzia Juni 26 hadi Julai 17 mwaka 2011 nchini Ujerumani.

Hakuna anayebeza

Timu yoyote isiyofahamika inapopangwa katika kundi lenye bingwa mtetezi au lenye timu zilizowahi kutwaa ubingwa au kushiriki mara nyingi hufikiriwa kuwa iko kundi gumu au la kifo.

Kadhalika timu ngeni katika mashindano yoyote yale na ambayo nyota au bahati au haijulikani uwezo wake huitwa black/dark horse.

Hiyo haina maana zitakuwa ‘mchekea’ au mteremko. Timu zinazopewa nafasi ya kushindwa huitwa favorites.

Lakini kuitwa favorite siyo tiketi ya ushindi. Baadhi ya timu zinazoitwa dark horse huzifunga timu favorites.

Hata wakati wa kupanga makundi seeding huanza na timu maarufu au zenye uwezo au zilizofanya vizuri katika mashindano yaliyopita, kisha hufuata zilizoshiriki mara nyingi na mwisho timu ngeni.

Mara nyingi timu zinazopewa nafasi kubwa kushinda hubweteka wakati timu ambazo hazipewi nafasi kubwa hufanya juhudi ili zitimize ndoto ya kuduwaza wadau kwa kupata ushindi.

Kwa hiyo waandishi wa habari na wadau wengine wa soka waliposema Twiga Stars iko kundi la kifo haikuwa kwa lengo la kubeza uwezo wake au kukatisha tamaa, lakini ni ukweli kuwa ndiyo timu pekee inayoshiriki mshindano hayo kwa mara ya kwanza.

Baada ya kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza Twiga Stars kwa kuifungasha Eritrea jumla ya mabao 11-4, ilikwenda Marekani kufanya mazoezi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya fainali hizo za Afrika Kusini.

Haikufanya vizuri, lakini ilipata uzoefu mkubwa katika ushiriki wa mechi za kimataifa ambao utatumika kupata ushindi katika michuano hiyo ya Afrika Kusini.

Hii haiondoi ukweli kwamba Twiga Stars inashiriki kwa mara ya kwanza tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1998. Twiga inahitaji msaada wa kila mdau wa soka kwani mafanikio yoyote yataitangaza Tanzania kimichezo na utamaduni.

0
No votes yet