Ndugai na mkakati wa kuzima upinzani


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameendeleza rekodi yake ya kuwatoa nje ya vikao vya Bunge, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai wanatumia lugha chafu.

Masikio ya Ndugai, na hata wenyeviti wengine wa vikao vya Bunge, yanasikia lugha chafu ya wapinzani lakini hayasikii lugha chafu ya wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Huu ni mkakati wa uonevu. Katika Bunge la Tisa, Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliridhia madai ya wabunge wa CCM kwamba Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) alilidanganya Bunge; akamfungia miezi mitatu.

Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge Dk. Batilda Buriani ndiye aliomba mwongozo akidai Zitto amelidanganya Bunge aliposema taratibu zilikiukwa katika kuingia mkataba wa uwekezaji wa mgodi wa Buzwagi. Baada ya mjadala, Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir akatumia kanuni akiomba Zitto afungiwe.

Alipopewa fursa ya kujieleza, Zitto akionyesha uhakika wa alichokisema, na akijua kuwa CCM walifanya njama na mshikamano kumlinda tu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi alisema yuko tayari kufungiwa kuliko kuomba radhi.

Bunge linalotawaliwa na wabunge wengi wa CCM lilitoa adhabu hiyo likijua ni kweli Waziri Karamagi alibeba mkataba kwenda nao London, Uingereza alikotia saini mradi wa Buzwagi hotelini usiku.

Pamoja na furaha ya wana CCM, Karamagi alikumbwa katika kashfa ya ufisadi ya kampuni ya Richmond, mwaka 2008 akajiuzulu.

Kwa kuwa tafsiri ya maneno ya uongo au matusi au lugha ya kuudhi inatolewa na mawaziri na kuridhiwa na Spika wa chama kilekile, wabunge wa CCM hawawezi kuadhibiwa.

Ndiyo maana, mwaka 2008 Sitta  alikataa kumwadhibu Mbunge wa Nzega mkoani Tabora, Lucas Selelii (CCM) aliyesema "Mheshimiwa Sipika, mawaziri hayo hapo, yana roho mbaya, Mungu na ayalaani tena  yafe kabisa."

Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge wa wakati ule, Philip Marmo alikerwa na lugha hiyo, akafunua kanuni za bunge, akaomba mwongozo wa spika juu ya kauli za Selelii kwamba "Mungu ayalaani mawaziri tena yafe kabisa."

Sitta, aliyekuwa anajiita Spika wa Kasi na Viwango, alidai Selelii hakuvunja kanuni yoyote ya bunge, alikuwa anatoa hisia zake tu. Lakini Sitta hakuwa anatoa majibu kama hayo kwa wabunge wa upinzani – John Cheyo aliwahi kutimuliwa.

Tafsiri hiyo ndiyo aliyoibeba Spika Anne Makinda pale Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe alipowalaani mawaziri akitaka wapigwe risasi kwa ufisadi.

Mwenyekiti Sylvester Mabumba, akaona safi Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigullu Nchemba aliposema wabunge wa CHADEMA ni vichaa wapelekwe Mirembe.

Ndugai aliyepanda cheo kutoka kuwa mwenyekiti wa vikao vya Bunge hadi kuwa naibu spika, anatekeleza mkakati wa kudhibiti upinzani na kwa sasa wapinzani wenye nguvu ni CHADEMA.

Kati ya mwaka jana na mwaka huu amewatimua vikaoni wabunge watatu, tena chini ya usimamizi wa askari wa Bunge. Wabunge aliowatimua kwa madai ya kwenda kinyume na kanuni za bunge ni Tundu Lissu, Singida Mashariki; Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini; na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Wiki iliyopita, Ndugai aliboresha rekodi yake kwa kumtoa nje ya Bunge, chini ya ulinzi Mbunge wa jimbo la Ubungo, John Mnyika.

Kwa kawaida, Mbunge akitoa maneno ambayo meza inakuwa na shaka nayo – spika au naibu au mwenyekiti – humwomba mhusika ama afute kauli yake au atoe ufafanuzi na ushahidi.

Spika Makinda amekuwa akitumia njia zote mbili lakini naye, pale alipoomba ushahidi akipewa hushindwa kutoa majibu.

Mwongozo mojawapo alioshindwa kutolea majibu ni wa Lema aliyedai “Waziri mkuu mwongo” kuhusiana na taarifa ya wananchi waliouawa na polisi 5 Januari 2011 mjini Arusha.

Lema alipovuliwa ubunge na Mahakama Kuu kanda ya Arusha, mwezi uliopita, Spika Makinda alisema hata miongozo dhidi yake imekufa.

Ndugai ni tofauti. Mnyika aliposema “Rais Kikwete ni dhaifu,” Ndugai alimtaka Mnyika afute kauli hiyo huku akikataa ombi la mbunge kutaka kutoa ufafanuzi.

Mnyika, aliyejiona kwamba ana ushahidi wa kutosha kuthibitisha alichosema, alikataa shinikizo la kufuta kauli; akatolewa nje ya Bunge.

Rais Kikwete, kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni mkuu wa nchi, mkuu wa Serikali, na amiri jeshi mkuu. Japokuwa anatokana na CCM, ni rais wa wote.

Kwa hiyo, anatekeleza majukumu yake kwa maslahi ya wananchi wote. Akiwa mahiri na makini ataonekana wazi na akiwa mzembe, mwenye upendeleo na kwa hiyo dhaifu pia ataonekana wazi kwa wote.

Aliyeomba mwongozo safari hii wa kusudio la kumtia adabu Mnyika ni Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Ndugai alijua akimpa Mnyika fursa ya kutoa maelezo ya kuthbitisha udhaifu wa Rais, itakuwa aibu hivyo akaona heri lawama kuliko fedheha, akamtimua nje ili kulinda hadhi na kuwafurahisha wana CCM.

Udhaifu wa Rais Kikwete ulianza kuonekana tangu awamu yake ya kwanza. Baada ya kulihutubia Bunge, mwaka 2008, Sitta alimwomba Rais afanye mambo matatu na mojawapo lilikuwa “aongeze ukali kidogo.”

Kwa hiyo, si rahisi kuficha udhaifu wa Rais Kikwete machoni pa Watanzania kwani anaumbuliwa na utekelezaji dhaifu wa mambo mengi.

Udhaifu wa Kikwete hauwezi kufichwa na Kanuni za Bunge. Kuwaita wezi ikulu ili kujadiliana nao namna ya kurejesha fedha walizoiba, serikali kukingia kifua watu maarufu waliobainika kuwa wabadhirifu, mafisadi na walarushwa ni udhaifu.

Hatua ya Rais Kikwete kulazimishwa kubadili Baraza la Mawaziri mara mbili kutokana na utekelezaji hafifu wa majukumu ni udhaifu. Mbaya zaidi Rais anaambiwa kuwa mawaziri wake wamegeuka fisadi, lakini yeye haoni.

Katika mahojiano na jarida la Financial Times mwaka 2007, alipoulizwa kwa nini Tanzania pamoja na misaada inayopata na raslimali ilizonazo bado ni masikini  Rais Kikwete alijibu kwamba hata yeye hajui. Miaka miwili tangu aingie madarakani Rais anasema hajui kwa nini Tanzania ni masikini si udhaifu kweli?

0754575524/0753651912. kibonadickson@ymail.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: