NEC isikimbie matatizo ya Pemba


editor's picture

Na editor - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame, amenukuliwa akisema tume yake haihusiki na matatizo yanayojitokeza katika uandikishaji wapiga kura kisiwani Pemba.

Anasema kuwa jukumu hilo linasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kwa hiyo, NEC haiwezi kufanya lolote kuwanusuru Wazanzibari na vurugu za uandikishaji wapigakura.

Kauli ya Jaji Makame inaweza kukanganya wananchi. Watu wanapata picha kuwa NEC na ZEC hazitangamani. Kwamba hazina uhusiano wowote kikazi.

Inafahamika kuwa ZEC imekuwa ikitumiwa na NEC kama wakala wakati wa uchaguzi unaohusu rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge na madiwani kwa upande wa Zanzibar.

Kama hali imekuwa hivyo kwa muda mrefu, kauli ya Jaji Makame haiwezi kuachwa hivihivi. Kwa kutafakari hilo peke yake mtu hawezi kusita kuihusisha NEC na ZEC. Kasoro zozote za ZEC moja kwa moja zinaigusa NEC.

Uandikishaji unaofanywa na ZEC hivi sasa unahusu pia kuwaandikisha wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani. Iweje Jaji Makame ashindwe kuliona hilo?

Hali ilivyo Pemba inatosha kumsikitisha yeyote mpenda amani. Ni bahati mbaya kuwa kauli kama ya Jaji Makame inaweza ikatonesha vidonda badala ya kuponya. Ni kauli ya kutia chumvi kwenye jeraha.

Sisi tunachelea kusema ni afadhali kukaa kimya kuliko kutoa kauli yenye maumivu kama hii, kwa kuwa kisiwani Pemba kuna watu wamepoteza mali au kuumia kutokana na vurugu za uandikishaji. Haifai kujifanya hatuoni hali hii mbaya au kukimbia uhusiano bayana kati ya NEC na ZEC.

Wakati umefika hizi nyimbo za “Tanzania ni kisiwa cha amani” zitekelezwe kwa vitendo, kwa kutafuta suluhisho kwa vurugu za Pemba mapema kabla mambo hayajawa mabaya.

Jaji Makame na NEC wanayo fursa ya kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya uandikishaji Zanzibar. Hawajachelewa. Waanze sasa kwa kushirikiana na wenzao wa ZEC, kwa sababu ni wakala wao kwa Zanzibar.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: