NEC isisubiri uchaguzi kuvurugika


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 30 March 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

TANZANIA ni nchi yenye matatizo mengi, lakini ukitafakari kwa kina sana chimbuko la hali hii kwa kiwango kikubwa utabaini ni hulka ya watu waliokabidhiwa majukumu mbalimbali katika jamii, kuanzia mitaani hadi kwenye ofisi za umma.

Ipo mipango na sera nyingi mno vimebuniwa kwa nia ya kutoandoa kwenye mkwamo wa umasikini, lakini miaka inapita bila kupatikana kwa tija yoyote; ukichunguza chimbuko la hali hiyo ni hulka ya watu wetu.

Watanzani kwa ujumla wetu tunapenda ukubwa na kila mbwembwe zinazoambatana na ukubwa, cheo kikubwa, heshima kubwa, ofisi kubwa, gari kubwa, kila kitu kikubwa! Kikubwa, lakini kwa bahati mbaya hatutendi makubwa ila tunaishia kutenda madogo, kwa hali hiyo mwaka baada ya mwaka hatuondoki pale tulipo. Mkwamo!

Mwishoni mwa wiki Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilikabiliwa na changamoto ndogo juu ya utendaji wake, hii ni uandikishaji wa wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura; kazi iliyokuwa ikifanyika ni ya kuboresha daftari hilo kwa mara ya pili kwa mkoa wa Dar es Salaam .

Hakuna ubishi kwamba Dar es Salaam ni mkoa wenye changamoto za kipekee ukilinganishwa na mikoa mingine nchini. Ni ukweli usiohitaji maelezo marefu kwamba kwa ukubwa wa eneo la mkoa huo idadi ya wakazi wake ni kubwa mno kuliko mikoa mingine yote ya Tanzania.

Ni kwa sababu hiyo, NEC inafahamu licha ya udogo wa mkoa huo ina majimbo ya uchaguzi saba ambayo hata hivyo kwa sasa yanaelezwa kuwa hayatoshi kwa kuwa idadi ya wakazi wake tangu mwaka 1995 yalipogawanywa imeongezeka mara dufu. Mkoa wa Dar es Salaa kwa sasa unakadiriwa kuwa na wakazi 4 milioni.

Uboreshaji wa mara ya pili wa daftari la wapigakura kwa jijini Dar es Salaam ulianza 22 Machi na ulikuwa uishie 27 Machi, ikiwa ni kazi ya siku sita.

Lakini kwa kuwa watu waliojitokeza siku ya mwisho walikuwa ni wengi kuliko kawaida, hadi ilipotimu jioni saa 12 muda wa kufunga vituo bado kulikuwa na msisururu mirefu ya watu katika vituo wakisubiri kuandikishwa.

Kwa bahati nzuri NEC waliona hali hiyo na kuamua kuongeza siku moja zaidi, ingawa nayo haikutosha kwa kuwa ilipotimia saa 12 jioni ya Jumapili ya 28 Machi 2010, bado idadi kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam walionekana katika vituo vya kujiandikisha.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba NEC imeona kama hali hii ya kujitokeza kwa watu wengi muda wa majeruhi kama ni adha kwao, na hata kauli iliyotolewa Jumamosi jioni ikimnukuu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Lewes Makame, kwamba eti ni huruma tu ya NEC kuongezwa kwa muda wa siku moja kwa mkoa wa Dar es Salaam, na kwamba muda huo hautaiongezwa tena kwa kuwa mikoa mingine nayo haikuongezewa, ni kauli ya ajabu kidogo.

Nilianza kusema kwamba moja ya sababu za kukwama kwetu katika mambo mengi kama taifa ni hulka ya watu wetu, wapenda ukubwa lakini bila kuutumia ukubwa huo kuongeza tija, hivyo kutuondoka kama taifa pale tulipo hadi ngazi ya juu yenye mafanikio na tija zaidi.

Kwa kauli ya NEC kwamba eti wakazi wa Dar es Salaam wamehurumiwa kwa kuongezewa muda ni kauli ambayo kimsingi hastahili kutoka kwenye kinywa cha mtu mwenye dhamana kama hiyo; ni kauli ambayo tunaiita ya bahati mbaya na inayostahili kujutiwa!

Kwa akili ya kawaida inadhaniwa kwamba ni furaha ya NEC watu wengi zaidi kujitokea kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura, kwa sababu ni kigezo kimojawapo cha kupima uwajibikaji wao.

Kwa maana hiyo kadri watu wengi zaidi wanavyojitokeza ingekuwa na maana kwa NEC kutafuta njia za kuwapa fursa ya kuandikishwa, Tume haiombi ruhusu kokote kutekeleza majukumu yake, ni sehemu ya wajibu wao kutafakari kila changamoto inayojitokeza katika kutelekeza majumu yake, lakini mwisho wa yote iwe ni kuwatumikia wananchi ipasavyo ili haki zao zisiporwe kiujanjaujanja au waziwazi.

NEC katika mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapigakura kwa mara ya pili kwa mkoa wa Dar es Salaam haikutekeleza wajibu wake sawasawa; hii ni kwa sababu nyingi.

Mojawapo kwanza imeshindwa kutambua changamoto za mkoa huo; imeshindwa kutumia changamoto hizo kujielekeza katika kutatua sababu ya watu wachache kujitokeza kujiandikisha katikati ya wiki.

Wakati NEC inazungumza habari ya usawa wa mikoa, haitaki kujielekeza katika mambo mengine ya kipekee yanayokabilia kila mkoa, kwa mfano, kuna maeneo ambayo NEC inafahamu kwamba inapogawa majimbo ya uchaguzi kigezo pekee si wingi wa wakazi wa eneo husika, kuna hali ya kijiografia ya eneo hisika, hili haliepukiki.

Kwa maana hiyo hiyo, ukitazama mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla wake haufanani na mikoa mingine yote kwa vigezo vingi, una msongamano mkubwa wa watu na magari barabarani ambayo husababisha wakazi wake kutumia muda mrefu zaidi kuwa barabarani kabla ya kufika kazini au kurejea kwenye makazi yao.

Ni mkoa pekee ambao watu wake wanatumia muda wa zaidi ya saa mbili kusafiri kilometa 30 tu; ni mkoa ambao ni nadra kusikia mfanyakazi akirudi nyumbani kupata chakula cha mchana kwa sababu hana nafuu hiyo kwa sababu ya kero za masongamano wa magari barabarani.

Kwa bahati nzuri NEC makao yake makuu ni Dar es Salaam, kuanzia mwenyekiti wake na makamishna maofisa wake wote waandamizi wanaishi Dar es Salaam; wanafahamu adha hii.

Katika mazingira ya mtu kuondoka nyumbani kwake alfajiri ya saa 10 na kufika ofisini saa 12, haitarajiwi mtu huo achomoke mchana kwenda kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura.

Ndiyo maana wakazi wengi walivizia siku za mwisho wa wiki ambazo wengi hawaendi kazini, lakini kwa bahati mbaya wakawa wengi na muda wa siku hiyo ukawa hautoshi kulikangana na idadi kubwa ya wakazi hao. Katika mazingira kama haya, kitu ambacho NEC ingefanya ni kuongeza muda wa kutosha si kutoa matamko ya kuudhi kama haya ya “kuwaonea huruma”.

Ningependa kuikumbusha NEC kuwa kuna mambo mengi ya ovyo imeyafumbia macho na ikapata huruma ya wananchi. Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi maofisa wa NEC walipashwa kujiuzulu kwa jinsi walivyoendesha uchaguzi katika mkoa wa Dar es Salaam . Umma ungali na kumbukumbu angavu kwamba NEC ilishindwa kusambaza vifaa vya kura kwa wakati ndani ya jiji hili.

Jaribu kufikiria, masanduku ya kura yaliyochukuliwa makao makuu ya NEC mtaa wa Garden saa 12 asubuhi hayakufika Magomeni hadi ilipotimia saa 12 jioni umbali wa takribani kilomita tatu tu. Kwa bahati mbaya haya yalitokea wakati mwenyekiti wa NEC akiwa ni huyu huyu na idadi kubwa ya makamishna wakiwa ni hao hao.

Kilichotokea ni kauli kwenye ripoti yao ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kwamba kulikuwa na hujuma ambazo hazikuelezwa zilifanywa na nani.

Tunajua uchaguzi wa Dar es Salaam uliahirishwa na kufanywa peke yake, lakini kwa kuvuruga ule wa siku moja kwa nchi nzima kilichotokea kila mtu anajua, watu kukata tamaa kwa kuwa badala ya kuwa uchaguzi mkuu ulionekana kama uchaguzi mdogo ambao hakuwa na mwamko na shamrashamra kama za awali. NEC hata leo bado umma unataka kujua kwa yakini nini kilitokea.

Si nia yangu kuisimanga NEC, lakini ni vema kila wakati ikae mkao wa kupokea changamoto na kuzifanyia kazi kwa kasi ambayo kwa kweli inaweza kubadili hali ya mambo na hivyo kuvunja hulka yetu kwamba taifa hili limeamua kufa na utamaduni wa business as usual- mambo kama kawaida tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: