Ngasongwa: Niko karibu na wananchi


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 15 July 2008

Printer-friendly version

UKITAKA kujua usemi wa 'Nabii hakubaliki kwao,' basi linganisha utendaji kazi wa Mbunge wa Ulanga Magharibi Dk. Juma Kharifa Ngasongwa na kauli za baadhi ya wananchi katika jimbo lake.

Ngasongwa amekuwa mbunge wa Ulanga Magharibi baada ya wilaya ya Ulanga kugawanywa katika majimbo mawili ya Mashariki na Mgaharibi.

Mbunge Ngasongwa alichukua ubunge jimbo lake likiwa na shule moja ya sekondari ya Kipingo iliyoko katika kata ya Malinyi. Leo hii jimbo lina shule 12 kutokana na usimamizi wake, ushirikiano wa karibu kati yake na wahisani pamoja na wananchi.

Katika mahojiano ya ana kwa ana na gazeti hili, Ngasongwa alizitaja sekondari mpya kuwa ni Itete, Biro, Malinyi, Mtimbira, Mavimba na Igota.

Nyingine ni Sofi, Minepa, Lipiro, Kiswago na Ngoheranga ambayo bado haijaisha kutokana na kuwa katika mgogoro wa kiwanja ambamo inajengwa.

Juhudi za mbunge hazikuishia kwenye shule. Yeye ni chachu katika mradi wa kilometa 670 za barabara kutoka Mikumi hadi Namtumbo mkoani Ruvuma, kupitia Ulanga Magharibi.

Ngasongwa ndiye mwenyekiti wa mradi huo ambao mpaka sasa Wizara ya Miundombinu umeutengea kiasi cha Sh. 100 milioni kwa ajili ya maandalizi ya awali ya ujenzi huo.

Pamoja na kutoa fedha hizo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha pia serikali iliishatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa la Mto Furua lilipo katika barabara hiyo.

'Serikali ilianza kwa kutoa fedha kwa ajili ya daraja la Mto Furua ambalo linatarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu,' ameeleza Ngasongwa.

Ngasongwa amejitosa katika kutatua matatizo ya wananchi. Kwa mfano, kutatua mgogoro mkubwa wa mashamba ya Kikwanju na Nanji.

Mashamba hayo yanayomilikiwa na wananchi wa Nakafuru, Lupiro, Igota Kichangani Igumbiro na Milola yalikuwa yamevamiwa na mwindaji Moses Shalon. Hivi sasa mgogoro umeisha na wafugaji na wakulima wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Mbunge huyo amekuwa akitoa misaada ya hali na mali kwa ajilli ya vikundu mbalimbali vya akina mama ili kusukuma la maendeleo kwa watu wa jimbo hilo.

Pamoja na hayo Ngasongwa aliweza kuvunja rekodi kwa wabunge wa mkoa wa Morogoro kwa kuiwezesha shule ya msingi Lupiro kuwa shule ya kwanza kuwa na Kompyuta kwa ajili ya shughuli zake za utawala.

Kutokana kujua umuhimu wa elimu kwa ajili ya wanajimbo wake, mbunge huyo anasomesha watoto sita (6) kuanzia Kidato cha I hadi cha IV katika shule mbalimbali za sekondari kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo.

Kuhusu tatizo la maji, Ngasongwa amesadia katika uchimbaji visima katika kata mbalimbali lakini msada mkubwa unonekana katika kata ya Malinyi na Seminari ya Kipingo ambako aliweza kununua na kufunga pampu za maji zenye thamani ya Sh. 3,250,000.

Hiyo ni baadhi ya misaada mbayo ameweza kuitoa lakini kuna misada mingi imetolewa na mbunge huyo kwa lengo la kuiweka Ulanga Magharibi kuwa moja ya majimbo bora hapa nchini na kujiandaa kwa mchakato wa kudai wilaya kamili.
.
Lakini pamoja na hayo, Ngasongwa amekuwa akisukumiwa lawama na baadhi ya wananchi wa jimbo lake kwa kile walichokiita, 'Kutokuwa na msaada na jimbo.'

Ngasongwa amesema katika mahojiano, kwamba hiyo ni moja kati ya propanganda za kisiasa kwani anaamini kuwa tangu awe mbunge wa jimbo hilo amekuwa akitoa misaada mingi ya hali na mali.

Amesema baadhi ya wananchi wanataka kuona akitoa hotuba za kuomba hiki au kile bungeni, kama wabunge wengine wanavyofanya, jambo ambalo anasema hakuweza kulifanya kwa kuwa amekuwa waziri.

'Unapokuwa waziri huwezi kuuliza maswali bali unatakiwa kujibu; nafikiri hilo ndilo somo ambalo watu wangu wanatakiwa kupewa na kufahamu vema,' alisema

Alisema kutokana na yeye kuwa katika serikali kwa muda mrefu, na sasa amepumzika, anatarajia kuwa katika wakati mzuri wa kuweza kuwasadia wananchi wake.

'Kusema kweli, tokea nistaafu uwaziri, nimekuwa karibu sana na wananchi wangu; naamini kuwa nitaweza kufanya yote niliyokusudia kuwafanyia,' alisema Ngasongwa huku akitabasamu.

Ngasongwa alizaliwa mwaka 1941 katika kijiji cha Ngombo, kata ya Biro, tarafa ya Malinyi, wilayani Ulanga katika mkoa wa Morogoro.

Alipata elimu ya msingi katika shule ya Mpapala, Ngombo; elimu ya kati katika shule ya Nawenge, Mahenge na elimu ya sekondari katika shule ya Mzumbe, Morogoro.

Ngasongwa alipata shahada ya kwanza ya kilimo mwaka 1967 na shahada ya pili katika maendeleo ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baada ya hapo alikwenda nchini Uingereza kusomea shahada ya tatu ya udaktari wa falsafa (Ph.D), katika uchumi kutoka chuo ya East Angalia, Uingereza mwaka 1988.

Ngasongwa ameshawahi kushika nafasi mbalimbali za utawala na katika taaluma. Alikuwa Mkurugenzi Maendeleo wa wilaya Geita (DDD) 1972-1976,

mhadhiri na mhadhiri mwandamizi vyuo vikuu vya vya Dar es Salam (UDSM) na Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa muda wa miaka 17.

Amekuwa mshauri wa rais wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi katika masuala ya uchumi mwaka 1993 hadi 1995.

Mwaka 1995 Ngasongwa alichaguliwa kuwa mbunge wa Ulanga Magharibi na kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo hadi sasa. Akisema kwa kujiamini, Ngasongwa alimwambia mwandishi, 'Naweza kugombea tena.'

 

Katika kipindi chake cha ubunge, Ngasongwa amewahi kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Amekuwa waziri wa Maliasili na Utalii, Viwanda na Biashara, na Mipango, Uchumi na Uwekezaji hadi Rais Jakaya Kikwete alipovunja baraza la mawaziri Februari mwaka hu.

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CM), Ngasongwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwa ni pamoja na kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia mkoa wa Morogoro kuanzia 1997 hadi mwaka jana alipoangushwa na Aziz Aboud.

0
No votes yet