Ngeleja amdhoofisha Prof. Mwandosya?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Ni kwa kutaka kumnyang’anya EWURA
Yadaiwa ni mbinu za urais mwaka 2015
Haruna Masebo afanyiwa vitimbi vipya

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja anatuhumiwa kuandaa njama za kudhoofisha wizara moja na kuangamiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam wiki iliyopita zilidai kuwa Ngeleja amepanga kuivunja EWURA ili kuunda mamlaka mpya itakayoripoti kwake moja kwa moja.

Kwa hatua hiyo, Ngeleja atakuwa ameingilia Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambako EWURA inawajibika.

Ngeleja aliiambia Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, wiki iliyopita (22 Februari 2011), kuwa wizara yake ina mpango wa “kuing’atua  EWURA” na kuunda taasisi inayodhibiti nishati peke yake na kuwajibika tu kwa wizara yake.

Alisema, “Moja ya changamoto zinazoifanya wizara yangu ishindwe kutekeleza majukumu yake, hususani ya kutatua mgawo wa umeme, ni EWURA kutowajibika wizarani kwangu.”

Maombi ya Ngeleja ya kutaka kuizima EWURA, ni mwendelezo wa mivutano ya muda mrefu kati ya wizara ya nishati na madini na wizara ya maji.

Kiutendaji EWURA inawajibika kwa wizara ya maji na umwagiliaji inayoongozwa na Profesa Mark Mwandosya.

Moja ya mivutano ya muda mrefu kati ya wizara ya Ngeleja na EWURA ni hatua ya wizara hiyo ya Machi 2009 ya kupitisha “azimio” lililolenga kutoishirikisha EWURA katika mipango yake ya kutekeleza miradi ya gesi asilia na umeme.

Hata hivyo, tuhuma dhidi ya Ngeleja zinawagusa pia wafanyabiashara wa mafuta. Tuhuma zinasema baada ya wafanyabiashara  “kushindwa kumweka kiganjani” Profesa Mwandosya, sasa wanataka kumtumia Ngeleja kuivunja EWURA.

Baadhi ya tuhuma inazoshushiwa EWURA ili kuhalalisha mkakati wa Ngeleja wa kuiangamiza, ni ile kwamba mamlaka hiyo imekwamisha uwekezaji katika sekta ya mafuta. Inataja mradi wa umeme kwa njia ya gesi wa makampuni ya Songas na Artumas.

Hoja kuhusu mradi wa Songas iliibuliwa kwa mara ya kwanza Septemba 2008, baada ya kampuni hiyo kuwasilisha kwa EWURA maombi ya kutaka kuongeza bei ya gesi asilia. EWURA waligoma kuridhia ombi hilo.

Ni katika mvutano huo, serikali inadaiwa kuanzisha mkakati wa kuipora EWURA mamlaka ya kusimamia gesi. Hadi sasa, wakati visima vya gesi vinakaribia kukauka, serikali imeshindwa kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya gesi ambao ungetoa meno kwa EWURA kusimamia sekta ya gesi.

Lakini kuna hili pia. Baadhi ya vigogo serikalini wanadaiwa kuchukizwa na kudorora kwa mradi wa umeme wa Mtwara, chini ya kampuni ya Artumas.

Mradi huo umeshindwa kuanza kutokana na serikali kukiuka Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 ambayo imeifanya kampuni ya Artumas kukosa uhalali wa kupewa lesseni.

Baada ya Artumas kukosa leseni, navyo vyombo vya fedha vya kimataifa viligoma kutoa fedha za kuendeshea mradi uliotarajiwa.

Sheria ya umeme ya mwaka 2008 ilipitishwa katika kipindi ambacho Bunge la Jamhuri lilikuwa bado linanguruma na sakata la mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC).

Ndipo ndani ya sheria hiyo, serikali kwa kujua au kutojua, ilipitisha kifo cha Artumas baada ya kuruhusu kuwekwa kwa kifungu kinachozuia makampuni ya madini ambayo tayari yalikuwa yameanza biashara nchini, kunufaika na sheria iliyopitishwa.

Hivyo basi, mradi wa Artumas na ule wa Umoja Light, imecheleweshwa na serikali yenyewe ambayo ilijiruhusu kuingia katika mkataba wenye utata na usiojali matakwa ya sheria ya umeme ya mwaka 2008.

Lakini badala ya wizara ya nishati kuangalia ilipojikwaa, imeamua kutuhumu EWURA kuwa inakwamisha uwekezaji katika sekta ya nishati.

Ugomvi wa wizara na EWURA ulifikishwa kwa waziri mkuu, Mizengo Pinda mara kadhaa, ikiwamo Septemba 2008, Aprili 2009 na Novemba 2009 ambapo ulijadiliwa kwa kukutanisha pande zote na mjadala kufungwa.

Hata hivyo, Juni 2010, tuhuma hizo ziliibuliwa upya. Safari hii, mbali na kupelekwa kwa waziri mkuu, zilifuatiliwa na katibu mkuu kiongozi, na sasa wigo wake umepanuka hadi kwa Rais Kikwete; na juzi Ngeleja amezifikisha Bungeni.

Kifungu cha sita cha Sheria ya EWURA, Sura ya 414 kinasema ni wajibu wa EWURA, katika kutekeleza majukumu yake, kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaboreshwa kwa kushamirisha ushidani huru na uwekezaji wenye tija.

EWURA wanatakiwa kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa; kulinda maslahi ya kifedha ya watoa huduma makini; na kushamirisha usambazaji wa huduma zinazodhibitiwa kwa wote wanaohitaji.

Aidha, ni jukumu la EWURA kuhakikisha wananchi wote, wakiwamo wenye kipato cha chini, wanapata huduma zinazosimamiwa na taasisi hiyo; kutoa elimu ya udhibiti kwa watoa na wapokea huduma; na watoa huduma kuzingatia utunzaji bora wa mazingira.

Wengine wanasema hatua ya Ngeleja kulifikisha suala la kuisambaratisha EWURA kwa Kamati ya Bunge imelenga kuwalisha maneno wabunge, hasa wale wapya, ili kufanikisha “masilahi ya watu wachache wizarani,” huku kukiwa na madai kuwa Ngeleja anatumika bila kujijua. 

Wachunguzi wa mambo wanaona kuwa kashifa za miradi ya umeme nchini zitaendelea kuwepo kama Rais Kikwete hatabadilisha safu ya watendaji wasio wanasiasa ndani ya wizara hiyo ambao wanazeekea humo na kubadilisha wizara kama taasisi za watu binafsi.

Leo hii kuna madai kuwa mkakati wa kuibomoa EWURA umelenga siasa na mikakati ya kuingia ikulu mwaka 2015, ambapo kundi la watuhumiwa wa ufisadi katika sekta ya mafuta wamepanga kuweka mtu wao.

EWURA ndiyo ilikuwa taasisi ya kwanza kushusha bei za mafuta nchini na kuweka historia mwaka 2009 baada ya mafisadi wa mafuta kuendelea kupandisha bei nchini huku ikiendelea kushuka katika soko la dunia.

Pamoja na changamoto mbambalimbali, EWURA wamekuwa wakipambana na uchakachuaji wa mafuta unaofanywa waziwazi tu kwa jeuri ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

Wapo wanaofika mbali zaidi. Wanasema mkakati wa kuibomoa EWURA mbali na kulenga 2015, wapo wanaoutumia kutaka kumkomoa binafsi Haruna Masebu, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo.

Tayari baadhi ya wachunguzi wa mambo  wanasema, wanaopanga mkakati wa kuisambaratisha EWURA wamefanikiwa kupenya hadi kwa Rais Kikwete ili kumshinikiza kumfuta kazi Masebu.

Mkurugenzi huyo anadaiwa kuponzwa na msimamo wake dhidi ya wafanyabiashara wa mafuta wasiofuata taratibu; na waliobobea katika vitendo vya uchakachuaji wa mafuta.

Kingine kinachomponza ni kusimamia bei ya mafuta ikiwamo kuweka bei elekezi, hadi kubuniwa kwa mradi wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja (Bulk Procurement) ambao haujatekelezwa.

Mwezi uliopita, taarifa kutoka ndani ya ofisi ya Masebu zilisema, nyaraka mbalimbali za kiofisi, ikiwemo kompyuta yake na ile iliyokuwa inatumiwa na katibu muhtasi wake viliibwa.

0
Your rating: None Average: 3.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: