Ngeleja anasubiri miujiza


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MAJIBU aliyowahi kutoa Makamu wa Rais wa Uganda, Dk. Specioza Kazibwe kwa mwandishi mmoja maarufu hapa nchini yanafaa kutumika kujadili hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Dk. Kazibwe aliyekuja nchini Julai 2001 kwa mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Omar Ali Juma, alichefuliwa na swali moja aliloulizwa alipotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Aliulizwa, “Aaah, eeeh! What message did Mr. Museveni give you when he was escorting you to the airport?”

Baada ya kushtuka, alijibu: “Mr. Museveni is my president, he can not escort me.” (Bw. Museveni ni rais wangu hawezi kunisindikiza mimi).

Dk. Kazibwe aliweka historia kuwa mwanamama wa kwanza barani Afrika kushika na kumudu nafasi hiyo.

Nimekumbuka majibu haya nilipomwona Waziri Ngeleja akijishusha katika mapokezi yaliyojaa mbwembwe ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, David Jairo.

Picha za vituo vyote vya televisheni zilionesha Ngeleja akipiga foleni kumsubiri Jairo na amefuatilia gari lililombeba Jairo likisukumwa na ‘mibaba’ huku kina mama wakiimba ‘Tunaimani na Jairo’.

Baada ya gari kufika wizarani, Ngeleja, aliyechomoka bungeni ili kuandaa kumpokea Jairo, alitimua ‘mibio’ kufungua mlango wa gari, akamdaka na kumkumbatia.

Hapa nikakumbuka majibu ya Dk. Kazibwe. Nikajiuliza kicheo nani bosi kati ya Jairo na Ngeleja? Ni nani kati yao anatakiwa kumpokea mwenzake? Kweli, Ngeleja alistahili kufungua mlango ili Jairo atoke?

Sina tatizo na wafanyakazi kupagawa wakati wa mapokezi ya Jairo ila twisti za Ngeleja. Mtu akifuatilia mikasa katika wizara hii atapata picha kuwa Ngeleja hakufurahia Jairo kurejeshwa ofisini, bali zilivyozimwa tuhuma za rushwa inayoikabili wizara ambayo Jairo alifanywa kafara.

Kabla ya bajeti yao kuwasilishwa, wabunge walishajipanga kuikwamisha. Zikasikika habari za jaribio la kuhonga wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.

Bajeti ikakwamishwa kweli kwa kuwa haikuwa na maelezo ya kutosha ya mikakati ya kumaliza tatizo la upungufu wa umeme nchini.

Wakati wa kuchangia hoja ikagundulika katibu mkuu, Jairo aliziandikia taasisi kadhaa zilizo katika wizara hiyo kutaka zichangie fedha za kuwezesha bajeti kupita. Kashfa hii haikumhusu Jairo binafsi bali wizara.

Ndiyo maana, hata Katibu Mkuu kiongozi, Philemon Luhanjo alipokuwa anatoa taarifa ya kumrejesha kazini Jairo, alisema huo ni mfumo uliopo.

Luhanjo anathibitisha Jairo hakukosea maana alichokifanya ni mazoea. Jiulize, nani anabeba lawama bajeti inapokwamishwa, ni katibu mkuu au waziri? Ni nani anabebeshwa lawama kwa kusambaza giza badala ya umeme kati yao?

Luhanjo alipothibitisha Jairo alifanya kosa la mazoea, alikuwa anasema wizara ilipanga kosa. Kama wizara ilipanga kuhonga inayookolewa hapa ni wizara.

Katibu ni mtendaji mkuu, lakini waziri ndiye msimamizi mkuu wa sera za serikali hivyo watendaji wote wa chini hujitahidi kulinda hadhi na heshima ya waziri. Hii ndiyo sababu ya Waziri Ngeleja kufikia hatua ya kumfungulia mlango katibu wake na kumkumbatia, ishara kuwa wamekwepa kashfa.

Lakini baada ya Rais Jakaya Kikwete kuendeleza likizo ya Jairo ili asubiri Bunge lichunguze tuhuma zake, Ngeleja naye atakuwa anasubiri miujiza kuepuka balaa lililowapata watangulizi wake – Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, na hata Edward Lowassa.

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: