Ngeleja atajwa katika ‘dili’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
William Ngeleja

WAZIRI wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja ametajwa katika “mpango” wa kampuni binafsi inayodaiwa kutaka kuchota fedha katika Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), MwanaHALISI limeelezwa.

Ngeleja anadaiwa kutambulisha wamiliki wa kampuni ya Asia Business Channel (ABC) kwa ofisa mmoja wa TMAA; kampuni ambayo sasa inadaiwa kukaba koo mamlaka kwa kuidai pauni za Uingereza (GBS) 35,500 (sawa na Sh. 100 milioni).

Taarifa zinasema ABC walikwenda TMAA kuomba kutengeneza programu ya televisheni kwa ajili ya kutangaza shughuli za uwekezaji katika sekta ya madini.

Mtoa taarifa wa gazeti hili amesema, kwanza walikataliwa, lakini baadaye ofisa wa TMAA alikubaliana nao kwamba iwapo watapata fedha, watawaita ili watengeneze programu hiyo.

Hatua hiyo ilifuatiwa maandishi kuwa ofisa wa TMAA awafahamishe, ifikapo Julai mwaka huu iwapo mpango huo umekubaliwa na fedha zimepatikana.

Februari mwaka huu, miezi mitano kabla ya muda wa ahadi, ofisa aliwaandikia barua pepe akiwaeleza kuwa fedha kwa ajili hiyo hazitapatikana. Ndipo ABC wakaanza kudai kuwa TMAA wamevunja mkataba wa kulipwa GBS 35,500.

Lakini Ngeleja alipohojiwa na gazeti hili juzi Jumatatu usiku, alisema “Hakuna kitu kama hicho. Kwa ufafanuzi zaidi, naomba uwasiliane na CEO wa TMAA ambaye atakupa ukweli zaidi.”

ABC imetishia kushitaki TMAA kupitia wakili mashuhuri nchini, Nimrod Mkono ambaye imeelezwa tayari amewapelekea hati ya madai.

Mtoa taarifa anasema, “…ni juzi tu mtendaji mkuu (CEO) wa TMAA alipokea barua kutoka kwa kampuni ya mawakili ya Mkono ikimtaka kulipa Pauni 35,500 ndani ya siku kumi, vinginevyo watafungua kesi mahakamani.”

Mwandishi alimfuata Paul Masanja, mtendaji mkuu wa TMAA kutaka kujua iwapo kulikuwa na kitu kama hicho.

Masanja amekiri kuwepo kwa madai hayo lakini amekataa kuongea kwa urefu, akisema gazeti liongee na mwanasheria wa mamlaka.

Mwanasheria Bruno Mteta ameliambia gazeti hili kuwa suala hilo “…si uongo, ila hakuna kinachoweza kuitwa mkataba kati ya TMAA na ABC.”

“Hawa watu wenye kampuni kutoka Uingereza, walikuja TMAA na kutaka kushirikiana na wakala kutangaza vivutio. Walijibiwa kwamba wakala hahusiki na kazi hiyo kwani wao wanashughulika tu na kazi ya ukaguzi,” amesema Mteta.

Amefafanua kuwa inaonekana ABC walitaka Tanzania ijitangaze; lakini walijibiwa kuwa “Kazi ya TMAA ni ukaguzi tu siyo kutangaza vivutio.”

“Tuliona wale jamaa labda wamepotoshwa tu,” ameongeza.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amekana kufahamu suala hilo ambalo CEO wa TMAA na mwanasheria wao wanajua na wamelitolea maelezo.

Alimwelekeza mwandishi aende ofisini kwake Jumanne ili aangalie iwapo “kuna kitu kama hicho.”

“Tangu ulipoanza kunitafuta nimekuwa vijijini mkoani Dodoma kikazi. Kwa sasa, na hivi tunavyoongea, nipo njiani kurudi Dar es Salaam. Ukinitafuta kesho (jana), labda naweza kukueleza zaidi…” amesema Maswi.

Ofisa mmoja Hazina ameliambia gazeti hili, “Hata pale kwetu tuliishakumbana na kampuni kama hizi, zikilazimisha ushirikiano na ubia hata pasipowezekana.”

Jitihada za kupata anwani na simu za ABC zimeshindikana, lakini ofisa mmoja wa TMAA ameahidi kulipa gazeti baruapepe ya kampuni hiyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: