Ngombale asaidiwe kuonyeshwa mlango wa kutokea


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 02 September 2008

Printer-friendly version
Kingunge Ngombale-Mwiru

KAMA kuna mwanasiasa katika nchi hii ambaye hataki kwenda na wakati, basi huyo ni Kingunge Ngombale-Mwiru. Ni mwanasiasa mkongwe pengine kupita wote ambaye bado anajishughulisha katika siasa.

Ni mwanasiasa mbaye kwa zaidi ya miongo minne – na katika awamu zote nne – bado yumo na anaendelea kusikika.

Lakini karibu kila mtu ukimuuliza sasa, atakuambia kwamba ni bora asaidiwe “kuutafuta mlango wa kutokea.”

Sababu ya kun’gang’ania madaraka bado haijawekwa wazi, ila tu kinachojulikana ni kwamba ameanza kuwa kero kwa kiwango kikubwa.

Kero ya sasa imetokana na matamshi yake ambayo kwa hakika yanaonyesha kuwa bado yuko katika enzi zile za 47, za chama kushika hatamu, hatamu ambazo zilishakatika zamani.

Na kwa vile bado anazo ndoto hizo, basi si rahisi kwake kuona na kubaini uchafu uliyomo ndani ya chama chake, uchafu ambao polepole unaanza kukiozesha chama na kukipeleka kaburini.

Ajabu kubwa ni kwamba kutokana na umri wake, na busara alizonazo ilitegemewa yeye awe mtu wa kukanya, kukaripia na kuelekeza wale wanaokichafua chama hasa kwa ufisadi uliokithiri.

Badala yake, anafanya kinyume na inavyotarajiwa. Anawaponda wale hasa wanaokemea maovu katika chama na serikali na kuwaambia hawana shukurani wanapokikosoa chama chao. Anasema bila chama wasingepata nyadhifa walizonazo.  

Lakini hajasema kama wakiamua kukaa kimya, wataendelea kushikilia nafasi hizo. Si hapo chama kitakuwa kimeporomoka? Kingunge hataki kuliona hilo.

Huko nyuma, Kingunge alikuwa “mchungaji” mkuu katika chama” tangu enzi za TANU, msemaji wake mkubwa na mnadharia wa kitini katika itikadi iliyokufa ya ujamaa.

Inawezekana kwamba imani yake kubwa katika itikadi hiyo ambayo kuendeshwa kwake hakuwezekani katika mfumo wa vyama vingi, ndiyo vinamfanya aendelee kuwa na mawazo ya enzi hizo. Ni enzi zile za gizani zisizokuwa na demokrasia wala ushindani.

Kwani kwa wale tunaokumbuka, wakati huo viongozi walikuwa sahihi, huku wakosaoji wakionekana waongo na wasio na hoja daima.

Ilikuwa ni enzi ya giza kuliita mwanga na wananchi wakakubali na kuimba hivyo. Mzee Kingunge bado anaishi katika enzi hizo.

Kingunge alikuwa ni mpiga debe mkubwa wa itikadi hiyo hapa nchini na nje pia – hususan katika nchi za Ulaya ya Mashariki zilizokumbatia itikadi hiyo na zilizokuwa zikiongozwa na Urusi ya Kisovieti.

Mara kadha alikuwa akialikwa kuhudhuria mikutano ya vyama vya Kikomunisti vilivyokuwa vikitawala nchi hizo, akiiiwakilisha TANU, na baadaye CCM na hata wakati nchi hizo zilikuwa zikiporomoka kutokanana na wimbi la demokrasia lililoikumba dunia mwishoni mwa miaka ya 80.

Wananchi wa huko hawakutaka kuendelea na laghai za utawala wa chama kimoja, achilia mbali itikadi ya Kikomunisti.

Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka 1989 wakati wa wimbi la maandamano ya kudai demokrasia nchini Romania lilipokuwa likivuma, Kingunge alialikwa katika mkutano mkuu wa chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo.

Baadaye kuhudhuria tafrija ya siku ili kuonyesha mshikamanao kati ya CCM na chama hicho. Huko walikunywa na kuimba, bila kujali kwamba mitaa ya mji mkuu wa Bucharest, kulikuwa na maanadamo yakipinga utawala wa Rais Nocolae Ceausescu.

Mwisho wa utawala huo ulikuja siku chache baadaye, siku ya mkesha wa krismas pale Caucescu na mkewe walipouawa kwa kupigwa risasi na wapigania uhuru baada ya kuhukumiwa kifo katika kesi iliyochukuwa muda wa dakika 15 tu.

Hii inaonyesha jinsi Kingunge alivyogizani mpaka sasa. Hajaona kwamba giza la wakati huo tayari limegeuka mwanga.

Alikwenda Romania pamoja na kwamba aliona kila dalili kuwa Waromania wanapinga itikadi ya Kikomunisti.

Na ndiyo maana hivi sasa anatumiwa sana na baadhi ya wanachama wa CCM kujaribu kuonyesha kuwa tuhuma za ufisadi unaowaandama ni jambo la kijinga. Naye anaifanya kazi hiyo kwa utiifu mkubwa.

Karibu miaka miwili iliyopita, baada ya viongozi wa Chadema, wakiongozwa na Dk. Wilbroad Slaa kutangaza hadharani majina ya vigogo 11 wanaotuhumiwa kwa rushwa kubwa, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema kuwa tuhuma hizo zilikuwa za hewani tu – hakuna ufisadi wowote katika chama chake wala serikali yake.

Hadi sasa hivi kuna mawaziri wanne wamejiuzulu – akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu – kutokana na kuhusika na madai ya matumizi mabaya ya madaraka, baadhi yao ni wale waliotajwa katika orodha ya Dk. Slaa.

Kwa ujumla, kutokana na umri wake, wengi wangetegemea kumuona Kingunge akiwa miongoni mwa wazee ambao wangesaidia chama chao.

Hata wanasiasa chipukizi wangeomba ushauri kutoka kwake, na yeye kuwa tayari kuutoa na kuonyesha njia iliyo nyofu na sahihi hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ufisadi. Lakini hivyo sivyo alivyo Kingunge.

Kwa ujumla umri wake mkubwa alionao unaonekana hauna maana sana kwa Watanzania kwani anaonekana kama vile anajitambulisha zaidi kwa mafisadi kuliko upande wa wananchi ambapo mali zao zinaporwa na wakubwa.

Na hili lilijidhihirisha wiki iliyopita alipokuwa akipokea maandamano mjini Dodoma yaliyokuwa yakipongeza “hatua” za Rais Kikwete kuhusu mafisadi wa EPA.”

Katika hotuba yake aliwashambulia wabunge wa CCM wanaotoa tuhuma kali dhidi ya mafisadi akisema ni vema wakanyamaza kwani bila CCM wasingekuwa na nyadhifa hizo CCM. Alidai hakuna kikubwa kama chama.

Hakika, kauli hizo zilizopaswa kutolewa katika miaka ya 70 ya enzi za “chama chashika hatamu” na siyo sasa.

Kwa kumkumbusha tu, ingekuwa ni wakati ule, wizi wa EPA usingejulikana kamwe. Kugundulika kwa wizi huo unatokana na tabia ya kujisahau ya viongozi wa chama tawala, au tuseme tabia ya kujiamini mno kwamba wanaweza kufanya kitu chochote na lisitokee lolote dhidi yao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: