Nguvu ya spika ni imani ya wabunge


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

UENDESHAJI wa bunge kwa sasa unaelekea kuwa janga la kitaifa na maafa ya kisiasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Yamesemwa mengi kuhusu uwezo wa Spika Anna Makinda katika kukiendesha chombo hiki muhimu kwa ustawi wa demokrasia nchini.

Kudhoofisha Bunge kwa njia ya kuhujumu mijadala na majadiliano, ni kuua kabisa mbegu za uwajibikaji wa serikali kwa wananchi na hata kuwajibika kwa serikali mbele ya bunge. Mtindo wa sasa wa Spika Makinda ni kutaka bunge liwajibike kwa serikali.

Tuliwahi kuandika huko nyuma kuwa Watanzania walitaka spika, lakini wakaletewa Makinda. Hawa walitaka spika wa bunge, wakaletewa mwanamke kwa maana kigezo kikuu kilichoangaliwa katika kumchagua kilikuwa ni jinsi yake na siyo uwezo wake.

Haya yanaweza kubakia kuwa makosa makubwa yaliyowahi kufanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uhai wake wa kuliongoza taifa hili.

Hasira za kumchukia spika aliyepita ziliwanyima watawala wa CCM na washauri wao, muono wa mbali zaidi; wakaishia kuona kuwa spika Sitta alikuwa anakihujumu chama tawala kwa kutaka kiwajibike. Hawakujua kuwa spika anayekifanya chama kisiwajibike ni hatari zaidi kuliko yule wa kwanza.

Kwenye baraza za serikali mjini Dodoma na kwenye vijiwe vya starehe za wakubwa, hivi sasa kuna gumzo la namna mbili kuhusu Spika Makinda. Gumzo la kwanza linachochewa na wapambe wa spika Makinda kuwa chanzo cha spika kuzongwa na wapinzani ndani ya bunge na kwenye vyombo vya habari, ni Spika Samwel Sitta ambaye anaendeleza majungu kuwa Makinda ameshindwa kazi.

Siyo siri kuwa spika Makinda na Sitta hivi sasa wanapishana kama magari yasiyo na indiketa; na chanzo cha uhasama huu ni maneno ya yanayodaiwa kusemwa na Makinda akiwatuma wapambe wake ili wamseme Sitta.

Gumzo la pili, ni watendaji wa serikali wanaoona kwamba rekodi yao ya utendaji haionekani kwa sababu ya Spika Makinda kuwatetea watendaji wabovu serikalini wanaoongozwa na waziri mkuu Mizengo Pinda.

Watendaji hawa, wakiwamo baadhi ya mawaziri na manaibu wao, makatibu wakuu na washauri mahsusi wa ikulu wanadai Pinda anapoteza muda mwingi kufanya kazi “kiseminari;” na matokeo yake uzembe wa watendaji haushughulikiwi kwa wakati.

Kwa kuwa yeye kama kiongozi mtendaji ameshindwa kuwawajibisha watu hawa, tumaini pekee lililokuwa limebaki kuwawajibisha ni wabunge kuwaweka kitimoto bila huruma. Lakini Makinda amekuwa mwiba kwa wabunge wakali wanaotafuta kuwawajibisha wazembe hawa akiwamo hata waziri mkuu.

Kitendo hiki kinatafsiriwa kuwa Makinda anawaona watendaji wabovu kama “makinda” yake asiyotaka yapate madhara mbele ya mwewe. Mwisho wa siku, utetezi na ulinzi wa spika kwa wazembe si msaada kwa serikali wala kwa CCM; kwani uzembe uliolindwa hauondoki, badala yake unaitafuna serikali na chama chenyewe.

Mpaka hapa, Samwel Sitta aliyeruhusu serikali itoe majibu na Makinda anayezuia majibu yasitolewe, ni nani anaisaidia CCM na serikali yake?

Maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu kila siku ya Alhamisi asubuhi, ni fursa muhimu kwa wananchi kuona kama viongozi wao wana uelewa wa kutosha kuhusu matatizo yao.

Aidha, maswali hayo ni fursa pana ya serikali kujibizana na wawakilishi wa wananchi kwa masuala yasiyohitaji urasimu wa kiserikali. Kwa hali hiyo, ni kasoro kubwa kwa spika kumgeuza waziri mkuu kama kinda lake analolilinda lisinyakuliwe na mwewe.

Nijuavyo mimi, waziri mkuu ni mtu mzima mwenye uelewa wa masuala ya serikali kuliko hata spika mwenyewe; na kwa hiyo anao uwezo wa kueleza, kuahidi, kukataa na hata kuangaliza kuwa swali fulani linavuka mipaka ya kiusalama, kiitifaki na hata kimhimili.

Wauliza maswali pia ni watu wazima walioaminiwa na wananchi. Kwa hiyo wana uwezo pia wa kuridhika na majibu ya waziri mkuu pale atakaposita kujibu swali fulani endapo amejiaminisha kuwa kujibu swali hilo kutaleta madhara kwa taifa.

Kwa maoni yangu, kwa spika kumzuia waziri mkuu kujibu swali fulani, ni dharau ya rejareja kwa kiongozi huyo na serikali anayoiongoza. Ifahamike na kusisitizwa kuwa siku ya Alhamisi ni siku ya maswali kwa waziri mkuu na si kwa spika. Kimantiki, swali hawezi kuulizwa waziri mkuu na jibu likatolewa na spika!

Tatizo la Makinda katika uendeshaji wa bunge ni kubwa na ni la msingi. Malalamiko ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wadau wengine yakiendelea kupuuzwa kwa sababu za kiitikadi na ushabiki usio na faida, kuna hatari kubwa mbele yetu.

Katika mengi, yanaweza kutokea mambo mawili. Kwanza, ni sehemu kubwa ya wabunge kwa wazi au kwa kujificha, watakapokosa imani na spika wao. Zipo dalili na ushahidi wa wazi kuwa kundi lisiloridhika na uendeshaji wa bunge wa Makinda linaongezeka na linajumuisha wabunge wote bila kujali itikadi wala vyama vyao.

Pamoja na kuwepo vitisho vya wanadhimu ndani ya bunge, vitisho hivyo haviwezi kulazimisha mioyo ya wabunge iwe na imani na spika wa Bunge anayepungukiwa na weledi pamoja na mizani ya haki.

Nimeongea na maspika wawili katika kanda ya Afrika Mashariki na wao wameniambia wazi kuwa nguvu ya spika ni imani ya wabunge, si wingi wa wabunge wa chama anachotoka. Spika anayefanya kazi kwa kutegemea wingi wa wabunge wa chama anachotoka, ni mamluki anayeweza kutumiwa na hata kutupwa na wanaomtumia.

Imani ya wabunge kwa spika ni sawa na imani ya wananchi kwa jaji wa mahakama yoyote. Hata kama jaji analindwa na katiba, sheria na walinzi wa mwili, lakini kinachomlinda zaidi na kumpa heshima mbele ya jamii ni imani ya watu kuwa huyu ni mtenda haki.

Hata waovu na wahalifu wanamheshimu jaji mtenda haki. Spika Makinda yeye anaheshimiwa na watendaji wazembe pamoja na wabunge wasio na hoja katika michango yao. Kwao, spika huyu ni mtetezi na mkombozi wao. Huu si ulinzi wa maana hata kidogo.

Pili, kwa sababu Spika amedhihirisha kupungukiwa na weledi katika wajibu wake na kuongozwa zaidi na jazba pamoja na makundi ndani ya chama chake; analazimika kila wakati kukimbilia kufanya marekebisho ya kanuni ili apate sababu ya kutimiza azma yake.

Matokeo ya hulka hii, ni kuandaa mazingira ya kuidhoofisha serikali zaidi na zaidi pale itakapotokea ajali ya utawala kwenda mikononi mwa wapinzani.

Jazba huzaa upofu hatari. Sheria kandamizi zilizotumiwa kukandamiza wapinzani, zinaweza siku moja kutumika kukandamiza chama tawala pale kitakapoondoka madarakani.

Tulikofikia, unahitajika uzalendo uliotukuka kutoka ndani ya wabunge wa CCM. Wanatakiwa kueleza waziwazi kuwa hawaridhishwi na uendeshaji wa bunge ili spika aamue moja la maana – kuyaacha makinda yajitetee mbele ya mwewe au aendelee kuyafunika akidhani anayalinda ili mwewe atafute mbinu ya kusomba wote – makinda na mama yao!

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: