Nguza anasota, wauaji wanasamehewa


Joster Ramadhani's picture

Na Joster Ramadhani - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitia saini hati tatu za adhabu ya kifo katika kipindi chote cha uongozi wake. Hati mojawapo ilikuwa dhidi ya Said Mwamwindi ambaye mwaka 1972 aliua kwa kumpiga risasi aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Wilbert Kleruu.

Katika awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi alitia saini hati 85 za kifo wakati Benjamin Mkapa maarufu kama Mr Clean na Rais wa sasa Jakaya Mrisho Kikwete maarufu kama JK hawajatia saini hata hati moja.

Badala yake Mr Clean na JK wamefanya ubia katika kubatilisha hukumu ya kifo na kuwaachia huru polisi wawili, koplo Juma Mswa na konstebo Mataba Matiku waliofungwa maisha kwa kumuua Mkurugenzi mstaafu wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe mwaka 1996.

Mr. Clean na JK kwanza walibatilisha hukumu ya kifo iliyowakabili polisi hao kuwa kifungo cha maisha jela; pili wakapunguza adhabu hiyo kuwa kifungo cha miaka miwili.

Baada ya kumaliza kifungo hicho polisi hao sasa wako huru mitaani wakila kuku kwa mrija.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu imesema uamuzi wa kubatilisha hukumu na kusamehe ulifanywa kabla ya JK kuingia madarakani mwaka 2005. Kwa vile mauaji hayo yalifanyika mwaka 1996 na hukumu ikatolewa mwaka 1998, bila shaka aliyetumia madaraka yake kikatiba alikuwa Mr. Clean.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya ikulu haikueleza kwa nini utekelezaji umefanyika Mei mwaka huu, miaka saba baada ya kumaliza kifungo chao cha miaka miwili.

Hatua ya kuachiwa huru polisi hao imefurahiwa sana na wanaharakati wanaopinga adhabu ya kifo. Kwao huu ni ushindi wa kampeni yao. Wanasubiri kuona mamia ya waliofungwa maisha kwa kosa la mauaji wakiachiwa huru.

Wanasema lengo la hukumu nyingi ni kutoa adhabu na kufundisha, hivyo mtu aliyeua naye akihukumiwa kifo atakuwa amepotezewa maisha badala ya kumwadhibu na kumfundisha. Hata hivyo, hili si lengo la makala haya.

Makala haya yanahoji ubaguzi wa kikatiba kwamba rais anaweza kumsamehe huyu akamkatalia yule wakati wote wameua na wameomba msamaha.

Duniani kote, mara nyingi wahusika wa mauaji ya kisiasa ndio hubahatika kufutiwa adhabu na kurejea uraiani. Vilevile wafungwa wa  kisiasa au watu maarufu huweza kunufaika ikiwa mifumo ya siasa itabadilika.

Adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni kunyongwa hadi kufa. Mkuu wa nchi ndiye hutia saini kuidhinisha mtu aliyehukumiwa kifo anyongwe, japo kutokana na kampeni ya asasi zinazopigania kufutwa adhabu ya kifo, hukumu ya kifo imekuwa ikibatilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela.

Ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2005 inamruhusu Rais kutoa msamaha.

Ibara hiyo inatamka “Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii, Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu.”

Wako mamia ya watu magerezani waliohukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia lakini adhabu zao zimebatilishwa kuwa kifungo cha maisha jela.

Mr Clean ndiye anadaiwa kubatilisha adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha na ndiye alipunguza adhabu tena kuwa kifungo cha miaka miwili. Hiyo ilikuwa mwaka 2003. Utekelezaji wa kumtoa umefanyika miaka saba baadaye. Kwa nini”

Kama adhabu ya kuua kwa kukusudia inasameheka, kwa nini Rais asiwasamehe mamia ya ‘wauaji’ walioko magerezani kwa maana wameadhibiwa vya kutosha? Kama adhabu ya kuua kwa kukusudia inasameheka, kwa nini Rais asiwasamehe wenye vifungo virefu vya makosa tena siyo ya kuua kama Nguza Viking na mtoto wake Papii Nguza?

Ushahidi uliotolewa wakati wa kesi hiyo ulionesha wazi Koplo Mswa na konstebo Matiku walimuua Jenerali Kombe kwa kumpiga risasi baada ya kudhani kwamba alikuwa mtuhumiwa sugu wa uhalifu.

Polisi hao walimkimbiza Jenerali Kombe aliyekuwa na mkewe. Alipoona hatari Jenerali Kombe alinyanyua juu mikono kujisalimisha, lakini bado wauaji wakamimina risasi kifuani na kumuua.

Mauaji hayo yalifanyika katikati ya uvumi kwamba Jenerali Kombe alikuwa akikisaidia chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi ambacho mwenyekiti wake alikuwa Augustine Lyatonga Mrema.

Hicho ndiyo kipindi ambacho Mrema alikuwa akilipua mabomu akifichua mipango, mikakati na njama za serikali kuua upinzani.

Mazingira haya ndiyo yaliwafanya watu wahisi kwamba mauaji ya Jenerali Kombe yalikuwa ya kisiasa. Ilihisiwa kwamba polisi hao hawawezi kusota jela miaka mingi kwa vile walitumwa. Miaka 16 tangu Jenerali Kombe auawe mazingira yanathibitisha hisia za watu – mauaji ya kisiasa!

Kwa nini wanaonufaika ni wanasiasa tu? Mwaka 1969  na 1983 wanasiasa na wanajeshi waliokamatwa kwa tuhuma za kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu Nyerere wote waliachiwa huru baada ya mifumo ya kisiasa waliyopigania kubadilika.

Waliokamatwa kwa tuhuma za uhaini mwaka 1969 ni pamoja na Bibi Titi Mohammed, Waziri wa Kazi, Michael Kamaliza. Walihukumiwa kifungo cha maisha jela lakini wakasamehewa mwaka 1972.

Mwaka 1983 vijana kadhaa wakiwemo kepteni Eugene Maganga, Suleiman Kamando, Zakaria Hanspop, Vitalis Mapunda, Mbogolo, Kajaji Badru, Hatty MacGhee na Christopher Kadego walikamatwa na wakatiwa hatiani mwaka 1985 kwa kula njama kutaka kumpindua Nyerere.

Watuhumiwa hao walipewa kifungo cha maisha jela lakini baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991 waliachiwa huru mwaka 1995.

Juhudi za serikali kubatilisha adhabu ya kifo zilionekana kwa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri. Mkuu wa mkoa huyo alichukua bastola yake akaelekeza kwa dereva wa daladala, Hassan Mbonde akafyatua na kumuua katika njiapanda ya Kawe na Bagamoyo.

Kortini wakasema Ditopile (sasa marehemu) ameua bila kukusudia kosa ambalo mtuhumiwa anaweza kusamehewa au kupewa kifungo cha miaka kadhaa. Halafu akapewa dhamana.

Koplo Mswa na Konstebo Matiku wako huru baada ya Mr Clean kutumia madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba. Vema.

Wafungwa wengine wa maisha wanapaswa kutimiza vigezo gani ili wafikiriwe kusamehewa? Wawe maarufu? Wawe na ndugu wanaojua sheria? Wawe viongozi kama vile Ditopile? Wawe polisi? Ndiyo wawe polisi maana hata polisi 13 waliofanya njama na kuua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi mmoja mwaka 2006 waliachiwa huru eti kwa kukosa ushahidi. Kikatiba si watu wote sawa mbele ya sheria?

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: