Ni bajeti mtihani


editor's picture

Na editor - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI inatarajiwa wiki hii kuwasilisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2011/2012 kwenye bunge la bajeti.

Tunatarajia kama ilivyofanya mwaka wa fedha wa 2010/2011, unaokwisha tarehe 30 Juni hii, itawasilisha kile tunachoita, “bajeti mtihani.”

Wakati inavyo vipaumbele, imeshindwa kuvipatia fedha kwa ukamilifu kama zilivyoidhinishwa na Bunge. Inatumia kuliko inavyochuma; inaachia fedha nyingi ziibwe; inapenda anasa na inalea rushwa na ufisadi.

Utamaduni huo mbaya wa kupenda kulea ufisadi na kushabikia matumizi ya anasa, unadhoofisha uwezo wake wa kuhimili mahitaji ya jamii ambayo yanazidi kukua.

Inazalisha kidogo kuliko inavyopanga kutumia. Huko ni kula zaidi ya kile unachoweza kuzalisha. Na hiyo maana yake unajichimbia kaburi kwani utalazimika kukopa zaidi. Ukikopa zaidi unakaribisha madhila zaidi.

Kwa sababu serikali haitaki kutumia kwa nidhamu, inajilazimisha kukopa na kwa hivyo, inazidisha deni kila mwaka. Takwimu zinaonyesha deni la taifa limekua kwa asilimia 18 kutoka lilivyokuwa 2009/2010.

Hapa, ndipo bajeti mtihani inapokuja. Itaendelea kukadiria tu kukusanya mapato yasiyofikia Sh. 11.97 trilioni (Sh. 11,970,000,000,000) huku ikitegemea wahisani wajaze pengo la nakisi (upungufu).

Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imejifunza zaidi kujua kukopa kuliko kutumia vizuri. Haitaki kudhibiti wizi serikalini; uzembe na ulafi. Bado inapenda fakhari.

Bali rais, makamu wake, waziri mkuu, baraza la mawaziri, makatibu wakuu na wachumi wa serikalini, wanajua wazi hayo yanachukiza wahisani inaowategemea kuiokoa isishindwe kuhudumia watu.

Watanzania wanazidi kulalamika hawapati huduma stahiki kwa ufanisi na kwa wakati; wanalia njaa na wanasikitika jinsi viongozi serikalini wanavyofisidi mapato na mali ya umma.

Kwa yote hayo, bado serikali ina ugonjwa wa kutotambua wajibu wake kwa wananchi waliochagua CCM na wengi walioikataa. Wote wana haki ya kuhudumiwa.

Ni bajeti mtihani kwelikweli. Maisha ya wengi yanazidi kudhoofika. Kiwango cha ukuaji wa uchumi cha wastani wa asilimia 7 kwa mwaka hakiendani na kuimarika kwa hali zao.

Badala yake kinachoonekana ni kuongezeka kwa pengo la Watanzania walio nacho (matajiri) na wale wasio nacho (mafukara). Hili ni jambo la hatari maana linachochea uhalifu.

Watanzania wanasukumwa kuichukia serikali. Athari za chuki, ni kubwa. Ubaya wake ni kwamba zitaanzia kwa viongozi. Wao ndio watakaosakamwa kwanza, wakati wa amani, au amani itapochafuka.

Sasa CCM inasubiri nini? Kwanini haibadiliki. Inakuaje viongozi wake wakuu wazidi jeuri na ufisadi? Mbona wanajikaribisha kuteketezwa?

Hatuchochei wananchi waichukie serikali. Hapana. Ila, kila tunavyotazama na kupima kiwango cha uvumilivu, tunabaini watu wenyewe wamechoka. Subira imewaishia.

Kilichobaki? Tunaasa viongozi wa CCM waamue sasa. Wajali watu kwa kuondokana na bajeti mtihani ili kunusuru kuteketezwa?

0
No votes yet