Ni gharama kurudia kufanya makosa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

HUHITAJI kuwa mtafiti kujua ukweli kuwa ni gharama kubwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea urais wake Jakaya Kikwete.

Hawaaminiki na ni mabingwa wa kutelekeza wanayoahidi. Hata katika mabango yao, hakuna sehemu iliyoandikwa kauli mbiu waliyoingia nayo madarakani mwaka 2005 ya “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.”

Nenda Mbeya, nenda Kigoma, rudi Dar es Salaam, kauli mbiu hiyo imeachwa, si kwa bahati mbaya, bali ni baada ya kubaini ukweli kwambas hawana uwezo wa kuwaletea watu maisha bora.

Vigezo vya wazi ni hivi. Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, kilo moja ya sukari iliuzwa kwa Sh. 750; leo ni Sh. 1600.

Mkate uliuzwa kwa Sh. 300; leo ni Sh. 1,000. Petroli ilikuwa Sh. 700 kwa lita, leo ni kati ya Sh. 1,600 na 2000. Saruji ilikuwa Sh. 5,000 kwa mfuko; leo ni Sh. 12,500. Umeme unapandishwa kila kukicha na gesi iliyodaiwa kuja kukomboa maisha sasa ni bei ya kuruka.

Uongo huu ni sehemu ya urithi wa CCM. Baada ya vita dhidi ya Uganda au ukipenda dhidi ya Nduli Idd Amin Dada, hali ya maisha ya watu ilikuwa ngumu. Serikali ya CCM ikawaambia Watanzania wajifunge mikanda kwa miezi 18.

Baada ya miezi 18 kupita wakaambiwa miaka mitatu, nayo ilipoisha, wakaambiwa wajifunge kwa muda mrefu ujao. Katika kipindi hicho Watanzania wakashuhudia uhujumu uchumi na sasa wanashuhudia viongozi wao wakineemeka kwa ufisadi.

Wahujumu uchumi walishughulikiwa, lakini leo mafisadi wananyenyekewa. Hao ndio waliojaa katika serikali ya CCM wakiwa la lugha ya kejeli ya kuletea Watanzania maisha bora.

Baada ya uongo wao kujulikana sasa wamestuka. Mabango ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania hayapo tena mitaani; ila wamepeleka dukani yakionyesha kupanda bei za sukari, unga, ngano, saruji, huku bei za mahindi na mpunga kwa wakulima zikiwa chini.

Katika miaka mitano hii ya ahadi, hakuna aliyenufaika; si mfanyakazi wala mkulima. Mfugaji anafukuzwa kila kona na vijiji vimechomwa moto ili kupisha upanuzi wa hifadhi kwa manufaa ya watu kutoka nje ya nchi.

Ahadi za ujenzi wa barabara kubwa kama vile kutoka Tunduma hadi Sumbawanga zimeanza kuota kutu. Hata Benjamin Mkapa, rais mstaafu, aliahidi.

Mwaka 2001 zilivunjwa nyumba bila fidia kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Kilwa kuanzia eneo la Bandari hadi Mbagala kwa msaada wa serikali ya watu wa Japan. Utekelezaji uliachwa uwe sehemu ya kampeni za mwaka 2005.

Kama kwa miaka mitano rais ameshindwa kutimiza ahadi zake. Je, atawezaje kutekeleza ahadi mpya na za zamani katika kipindi hiki ambacho anajua harudi tena? Tunahitaji kutafakari na chukua hatua.

Wana CCM ni kama nzi na nyuki ambao hufa kutokana na kulazimisha kupenya katika kioo angavu. Hujigonga tena na tena, baada ya muda mrefu wa kujigonga, huku wakikosa chakula, hukosa nguvu kisha hudondoka chini na kufa.

Maisha bora chini ya CCM yameshindikana, kilichobaki ni kilio. Wana-CCM wanalia, wapinzani wanalia, kila mtu analia kwamba hakuna maisha bora.

Bungeni wabunge wa CCM wanalia – hatutendewi haki, tuliahidiwa kuletewa maziwa, chama kina mafisadi, katibu anawapendelea mafisadi, mafisadi hawa wanafilisi nchi, mafisadi wanatumia Takukuru kutumaliza na kelele kibao huku wabunge wa upinzani wakicheka.

Gharama ya kupinga ufisadi ndani ya Bunge imewakuta Lucas Selelii, William Shelukindo, Samweli Malecela; wameshughulikiwa, wameondolewa. Na wale ving’ang’anizi kama Joseph Mungai wameshughulikiwa na Takukuru.

Ujumbe tunaopata hapa ni kwamba kumbe wanaoona udhaifu katika serikali ya Kikwete si wapinzani tu, bali hata wana-CCM. Ujumbe mwingine tunaopata kutoka kwa wabunge wa chama tawala ni kwamba mshikamano wa wana-CCM uko shakani.

Wanaoona gharama kubwa kuichagua CCM wametoka na wanaendelea kuhamia upinzani. Upinzani uliopo ni mkubwa mijini na vijijini; ndiyo maana CCM ina hofu ya kuondolewa.

CCM wamehama kwenye agenda ya sera, wamekimbilia hoja za kuchafuana. Ndio maana hii leo wanamwandama Dk. Slaa kwa vineno dhaifu vya mahusiano ya suruali na sketi. Huku ndiko kuishiwa.

Wanafanya hivyo kwa gharama kubwa na kwa kodi za wananchi. Kuendelea kuwa na CCM ikulu ni kufilisi nchi; ukitaka ni kuleta laana kwa Watanzania.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: