Ni kikosi cha ‘mazishi’ ya CCM


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi
UTEUZI WA MAWAZIRI WAPYA

RAIS Jakaya Kikwete ametangaza timu mpya iitwayo baraza la mawaziri.  Wapo wanaosema ni watu walewale bali wamevaa nguo mpya; au wasemavyo, mvinyo uleule katika chupa mpya.

Kwangu mimi, baada ya kupitia vigezo kadhaa vya kiuchambuzi, napata ujasiri wa kusema kikosi hiki kinachoitwa kipya, ni dhaifu kuliko kilichopita.

Kwa maana hiyo, kikosi hiki kinabadilisha matumaini yote ya wananchi. Kama kazi ya kikosi kilichopita ilikuwa kuokoa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM); basi kikosi hiki kitafanya kazi ya kuvizika.

Kwa kutumia lugha ya picha ya kivita, ni kwamba merikebu ya CCM – chama na serikali yake – haina tena viongozi.

Abiria wamepata kiwewe na kuanguka baharini. Safari imesimama na kazi ya kuokoa imekuwa ikiendelea kitambo sasa.

Baadhi ya abiria waliobahatika kuopolewa, wameonyesha tabia ya ajabu pale wanapojirusha tena majini na kufanya kazi ya uokoaji iwe ngumu zaidi. Sinema hii inaendelea na haionyeshi kuwa itakuwa na mwisho mzuri.

Baada ya kamati za bunge kusema, bunge likasema, kamati ya wabunge ikasema na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ikasema, hapakuwa na sababu ya kubakiza baadhi ya mawaziri katika baraza lililotangazwa.

Aidha, hapakuwa na sababu ya kuongeza idadi ya mawaziri; na hapakuwa na sababu ya kubakiza hata wale ambao hawakutajwa na wabunge.

Hii ilikuwa fursa ya kufanya mabadiliko makubwa yakiongozwa na mchakato mkali wa uchunguzi wa wale ambao wangerejeshwa au kuteuliwa kwa mara ya kwanza katika baraza la mawaziri.

Hili halikufanyika na litamgharimu sana rais pamoja na chama chake. Kosa la kwanza la kukosekana kwa mchakato makini limekwishaonekana.

Hili linahusu rais kuteua wabunge na halafu kuwateua kuwa mawaziri na hatimaye kutangaza kuwaapisha kuwa mawaziri kabla ya kuapa kuwa wabunge.

Anaweza kuahirisha kuwaapisha kuwa mawaziri mpaka bunge likae, lakini tayari kosa kubwa limefanyika na kutia dosari mchakato mzima wa uteuzi na uendeshaji serikali.

Katika serikali makini, dosari hii ingeondoka na mtu huko ikulu; lakini kwa kuwa kuna ombwe la uongozi, hilo haliwezi kutokea.

Kasoro hii kubwa inanipeleka katika jingine kubwa katika uteuzi. Kada maarufu wa CCM, George Mkuchika ameteuliwa kuwa waziri mpya ofisi ya rais anayeshughulikia utawala bora.

Hili naliita kosa la mwaka. Ni kwa sababu kuu mbili. Kwanza, serikali hii inakabiliwa na tatizo kubwa la utawala bora. Mambo ya kiserikali, siri na taratibu zake, yanaenda ovyo.

Ni mwenendo huu ambao umefanya Mkuchika kuteuliwa kuwa waziri wa wizara inayohusika na idara nyeti kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Usalama wa taifa.

Bila uovyo katika wizara hii na vyombo vyake, Mkuchika asingeteuliwa kuwa waziri wa wizara hii labda kama lengo ni kumwezesha yeye kulipa visasi vya waliombanika akiwa TAMISEMI.

Tatizo la utawala bora katika miundombinu ya utawala wa serikali yetu, linahitaji mtu makini zaidi, mwadilifu zaidi, asiye na makundi na asiye na huruma za kifisadi.

Pili, Mkuchika ametokea TAMISEMI ambako hata rais amesikika mara kadhaa akilalamika kuwa mambo yako ovyo mno na kuagiza halmashauri zichukue hatua kali.

Alisikika Dodoma akilalamika kwenye semina elekezi. Mara ya mwisho alilalamikia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani wiki iliyopita, mjini Tanga.

Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kuonyesha uozo uliokithiri katika halmashauri zetu, hata kama Mkuchika aliukuta au hahusiki nao, ingetosha kutomteua katika nafasi nyeti kama hii.

Uteuzi wa Mkuchika ni kofi la usoni kwa CAG, kamati za bunge, kamati ya wabunge na hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Hata kama wananchi hawafahamu yote yaliyo nyuma ya pazia kuhusu uteuzi huu, rais ajue yeye ni mwanasiasa.

Hatimaye, kazi yake itafanywa kuwa ngumu kutokana na teuzi anazofanya bila kujali jamii inajua nini juu ya wateule wake.

Si ajabu kigezo muhimu kilichotumika kumteua ni hatua ya Mkuchika kuandika barua ya kujiuzuru bila kujitetea kama wengine.

Uteuzi mwingine tata ni ule wa Profesa Jumanne Maghembe aliyehamishiwa wizara ya maji akitokea kilimo na chakula.

Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya kilimo na maji na uhusiano huo ungemwongoza rais katika kufanya uteuzi wake kwa umakini wa ziada; hata wa kuazima.

Baada ya yeye mwenyewe na “swahiba” wake Lowassa kutofautiana juu ya nini kiwe cha kwanza, serikali ya Kikwete ilitangaza kilimo kiwe cha “kwanza” huku Lowassa akitangaza katika ziara zake kuwa elimu ndiyo “kwanza.”

Bila kujali tofauti zao binafsi tusizojua chanzo chake, tukubaliane kimsingi kuwa kilimo na maji ni vitu viwili muhimu. Aliyeshindwa Kilimo hawezi kuongoza Maji.

Ukiacha Mkuchika na Maghembe, hawa wawili ambao wamepigiwa kelele karibu na kila mtu, kikosi kizima hakina muunganiko.

Kwa Hawa Ghasia kupelekwa Tamisemi ni sawa na kupakia tembo kwenye pick up. Hussen Mwinyi kupelekwa Afya licha ya kukiuka utamaduni mzuri wa Muungano, ni kuifungia wizara iache kufikiri tena.

Ni Mwinyi aliyegoma kujiuzuru wakati wa mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala; lakini akawa kinara wa kuwataka wenzie wajiuzuru.

Kuwabakiza mawaziri wanaotuhumiwa ufisadi, wizi na kushindwa kufanya kazi; na ambao vitendo vyao viovu vinaonekana kwa wengi, ni kuonyesha wazi kuwa mteuzi hana mawasiliano na wananchi.

Kwa naibu mawaziri, huko ni vurugu tupu. Baada ya kufichuka siri za jinsi wanavyovurugana na mawaziri wao, kuongeza idadi yao siyo tija, bali ni kuongeza gharama.

Mpaka sasa, hakuna kazi maalum ya naibu waziri inayojulikana, zaidi ya kujibu maswali yaliyoandikwa bungeni.

Gharama kubwa ya utitiri wa manaibu siyo suala la magari, ofisi, mishahara na ukwapuzi mwingine; bali muda wa rais na waziri mkuu, ambao wanatumia kutatua migogoro ya watu hawa “wasio na kazi.”

Kwa hiyo utitiri wa manaibu ni kuongeza gharama za kikosi cha mazishi badala ya kuokoa jahazi lililokwishaanza kuzama.

Kwa haya, ongeza uteuzi wa manaibu kama Adam Malima, katikati ya kashfa nzito, tena za hivi karibuni; kukiwemo kukutwa na silaha ya kivita na ukimya uliofuatia.

Kwa vyovyote vile, wananchi wanajua sasa nani mchimba kaburi la CCM.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet