Ni kufa na kupona vita vya umeya Dar


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version

WAGOMBEA umeya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Dar es Salaam watatoana ngeu.

Vuta nikuvute ambayo inaendelea kwa miezi kadhaa sasa, imehamia kwenye tuhuma za kutoa na kupokea rushwa.

Mvutano mkubwa upo katika manispaa ya Ilala ambayo inachukua sehemu kubwa ya maeneo ya katikati ya jiji, ikiwemo ikulu, wizara, mahakama kuu na maeneo makuu ya biashara.

Kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa jiji la Dar es Salaam, dola za Kimarekani 462 milioni (karibu Sh. 700 bilioni) zitatumika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Aidha, sehemu kubwa ya fedha hizo inatarajiwa kutumika katika manispaa ya Ilala.

“Hili ndilo linazidisha ushindani, hasa kwa manispaa ya Ilala ambako kila diwani mashuhuri, na mwenye ushawishi, anakimbilia kugombea,” ameeleza mmoja wa madiwani wa zamani.

Taarifa kutoka serikalini zinasema chini ya mpango mpya, hakutakuwepo na Meya wa Jiji la Dar es Salaam; isipokuwa kila manispaa – Ilala, Temeke na Kinondoni – itakuwa na meya wake.

Katika manispaa ya Ilala, wagombea umeya wanaotajwa kuingia katika vuta ni kuvute, ni aliyekuwa naibu meya wa Ilala, Jerry Slaa na diwani wa kata ya Mchafukoge ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Dodoma Mjini, Hashim Sagaff.


Wengine wanaotajwa kuwa katika vuta ni kuvute hiyo, ni meya wa zamani wa manispaa hiyo, Abuu Jumaa na mbunge wa Baraza la Kutunga Sheria la Afrika Mashariki, Didas Masaburi.


Taarifa zinasema, Slaa ndiye anaonekana kuungwa mkono na madiwani wengi hasa wanawake, kutokana na msimamo wake thabiti wa kutetea chama na rasimali za taifa.


Katika kinyang’anyiro hicho, Masaburi ambaye ni diwani wa Kivukoni anadaiwa kubebwa na baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini kwa kile wachambuzi wanaita, “Mkakati wa kuelekea 2015.”

Miongoni mwa wanaodaiwa kumbeba Masaburi kwa “mwelekeo wa 2015,” ni Sophia Simba, mwenyekiti wa taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).


“Hapa kuna mkakati wa 2015, si vinginevyo. Tusidanganyane. Hebu jiulize, kwa nini Masaburi amejiingiza katika kinyang’anyiro cha udiwani, wakati tayari ni mbunge wa Afrika Mashariki?” anauliza kigogo mmoja wa CCM ambaye hakupenda kutajwa gazetini.


Anasema, “Kambi hii imejenga mtandao mkubwa wenye lengo la kumuingiza ikulu mtu wao. Ni kujiimarisha kisiasa na kiuchumi kwa ajili ya uchaguzi ujao ndani ya chama na katika serikali. Hakuna jingine ndugu yangu,” kimeeleza chanzo cha taarifa.


Inadaiwa kuwa Masaburi amekuwa akiita baadhi ya madiwani na kufanya nao vikao kwa lengo la “kujiweka sawa.”

Baadhi ya vikao vimekuwa vikifanyika katika klabu za Selander Bridge na Lamada.


“Huyu bwana amekuwa akikutana na baadhi ya madiwani na viongozi wengine wa chama wenye ushawishi katika vikao vya uteuzi hapa Selander Bridge Club na kule Lamada Hotel.


“Amekuwa akiwaeleza kuwa wale wagombea wanaowataka, majina yao hayatarudi; na ameandaa pesa nyingi kuwasambaratisha,” ameeleza mtoa taarifa mmoja aliyekutwa katika baa akidai kuwa anamsubiri Masaburi.


Amesema, wagombea ambao Masaburi amejiapiza kuwa hawatarejeshwa katika kinyang’anyiro hicho ni Sagaff na Slaa.


Katikati ya miaka ya tisini, Masaburi alituhumiwa kutafuna mabilioni ya shilingi katika mradi wa mabasi ya wanafunzi mkoani Dar es Salaam.


Mradi huo ambao ulitajwa kuwa mwarobaini wa matatizo ya usafiri kwa wanafunzi wa jiji la Dar es Salaam, uliuawa katika mazingira ambayo hayajawekwa wazi hadi leo.


Juhudi za MwanaHALISI kuzungumza na Masaburi hazikufanikiwa kwani simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokewa. Hata alipopelekewa meseji ya simu kuwa gazeti hili linahitaji kuzungumza naye, hakujibu pia.


Gazeti hili limefahamishwa kuwa vuta nikuvute hiyo sasa imeelekezwa katika vikao vya Kamati Kuu (CC) na Kamati ndogo ya Maadili ya chama hicho.


Mkutano wa CC umepangwa kufanyika keshokutwa. Utatanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili kitakachofanyika leo kuanzia saa nane mchana.


Taarifa zinasema vikao vya CC na kamati ya maadili vinatarajiwa kuibua mjadala mkali wa nani hasa anayefaa kuwania nafasi hiyo kutokana na madai kuwa baadhi ya wagombea tayari wamepanga watu wa kuwatetea.


Tayari mvutano mkali umeibuka katika kikao cha sekretarieti ya wilaya ya Ilala kilichofanyika 23 Novemba 2010 na kamati ya siasa ya wilaya kilichofanyika siku iliyofuata.


Katika mikutano hiyo miwili, taarifa zinasema baadhi ya wajumbe walitumika kuwakandamiza Abuu Juma na Slaa. Majina yaliyopendekezwa na mikutano hiyo, ni Sagaf, Masaburi na diwani wa Kata ya Gerezani, Bisalala Salum.


Hata hivyo, vikao vya sekretarieti ya mkoa na kamati ya siasa ya mkoa, vilivyofanyika 28 Novemba, vilirejesha majina ya Slaa na Jumaa.


Kwa mujibu wa mtoa taarifa, baada ya mvutano mkali, wajumbe wa vikao hivyo walikubaliana kupeleka majina ya wagombea watano kwenye vikao vya juu vya CCM.


Majina yaliyopelekwa kwenye vikao vya juu vya chama, ni pamoja na Abuu Jumaa, Jerry Slaa, Hashim Sagaff, Didas Masaburi na Bisalala Salum.


Katika kuhakikisha Masaburi anapitishwa na hatimaye kushinda nafasi hiyo,  inadaiwa baadhi ya wapambe wake wamekuwa wakiendesha kile kilichoitwa “hujuma” za kuondoa majina ya wagombea udiwani wa viti maalum.


Anayedaiwa jina lake kukatwa kwa kuwa “si mtu wa Masaburi,” ni Rukiya Riyami. Tayari mwanachama huyo wa CCM amewasilisha malalamiko yake kwa katibu mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba.


MwanaHALISI limeelezwa kuwa katika mchakato wa awali wa kupata madiwani wa viti maalumu, Riyami alishika nafasi ya tatu miongoni mwa nafasi nne za viti hivyo zilizotengwa kwa ajili ya jimbo la Ilala.


Lakini, badala ya kumpitisha Rukia, Halmashauri ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ilimpitisha Moshi Kinyogoli Kondo, ingawa kwenye kura za kuwania viti maalumu, Kondo alikuwa ameshika nafasi ya sita.


Hata hivyo, baadaye CCM mkoa ilibadilisha na kumpa nafasi hiyo Tumike Jabir Malilo, ambaye kwenye kura za awali alishika nafasi ya nne.


Akizungumza na gazeti hili kuhusu uamuzi wa kumwacha Rukia na kumchukua Tumike, Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda, amesema, “…hilo ni suala la kawaida.”

Alisema vikao vya chama vimepewa mamlaka ya kuteua wagombea wa chama kwa kuangalia vigezo vilivyowekwa na si lazima kufuata kura zilizopigwa.


“Katiba ya CCM inatamka wazi kuwa vikao vya halmashauri ya chama mkoani, vitafanya maamuzi ya mwisho kuhusu wagombea mbalimbali wa nafasi za uongozi.


“Imeshawahi kutokea kwa chama kumpitisha mtu aliyeshika nafasi ya pili au ya tatu kwenye kuwania ubunge au udiwani na kumwacha aliyekuwa wa kwanza. Haya ni maamuzi ya vikao,” alisema.


Miongoni mwa madiwani wa CCM waliofanikiwa kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu aliliambia MwanaHALISI kuwa kuna “vita vikubwa.”

“Hata kutofanya vizuri kwa CCM katika mkoa wa Dar es Salaam, kulichangiwa na hujuma ya baadhi ya wana-CCM wenyewe ambao waliamua kuwaangusha wale ambao waliamini kuwa hawatawaunga  mkono katika vita vya umeya,” alisema.


Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, zaidi ya wana-CCM 10 wamejitokeza kuwania umeya.


Baadhi ya waliojitokeza ni Julian Bujugo, Tarimba Abbas, Athumani Chipeta, Shariff Abbas na John Momo Moro
Wanaotajwa kuwa na nafasi zaidi ya kutwaa nafasi hiyo ni Bujugo, Tarimba na Moro, ambao wametajwa kuwa na mtandao miongoni mwa makundi yanayotaka kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM.


Katika manispaa ya Temeke, zaidi ya wana- CCM wanane wamejitokeza kuwania nafasi hiyo nyeti.


Baadhi ya waliojitokeza ni Anderson Chale, Zena Mgaya, Wilfred Kimati na Noel Kipengule. Miongoni mwa majina hayo manne, mmojawapo anaweza kuibuka kuwa meya.


Chale, Mgaya na Kimati ni miongoni mwa madiwani wa muda mrefu katika manispaa hiyo na wanatumia uzoefu wao kama turufu ya kuwapatia ushindi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: