Ni kweli Kikwete ameshindwa


Haji AmeirAmeir's picture

Na Haji AmeirAmeir - Imechapwa 11 August 2009

Printer-friendly version

MAKALA ya Salva Rweyemamu, aliyepinga kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kazi, ndiyo imenivuta katika mjadala huu.

Lakini Salva ameshindwa kujibu hoja za Profesa Lipumba. Makala ya mwandishi Mohamed Yusuph (MwanaHALISI la 22 Julai) inathibitisha hilo.

Nitangulie kusema kuwa huu ni mjadala wenye rutuba kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kuondoa maadui watatu wakuu waliotangazwa na Mwalimu Julius Nyerere baada uhuru.

Maadui hao ambao wanasiasa wameimba kwa karibu miaka 50 sasa ni: umasikini, ujinga na maradhi.

Lakini maadui wameongezeka. Rushwa na ubadhirifu vimetamalaki. Ni maovu yaliyochangiwa na sera mbovu na itikadi isiyotekelezeka ya CCM.

Bado Watanzania wanaogopa mabadiliko. Wanajua ulegevu wa serikali ya CCM ndio umefikisha nchi ilipo, bali wanaamini CCM ingali chama makini kuongoza.

Salva ni mfano. Anajua CCM imeshindwa kubadilisha maisha ya Mtanzania wa kawaida, lakini anashikilia kutetea rais.

Halaumiki maana kazi yake ni kumkinga rais dhidi ya lawama na shutuma. Lakini anajua CCM ya sasa inayoongozwa na Kikwete ilivyokumbatia matajiri na kuacha maskini waangamie.

Anajua habari za migomo ya watumishi ilivyotawala; anajua malalamiko ya wakulima kuhusu ongezeko la bei ya mbolea, pembejeo na zana za kisasa; bado mazao yao wanauza kwa hasara.

Salva anajua pia hali duni ya wafugaji. Kila siku wanafukuzwa kwa kisingizio cha kuvamia maeneo ya wakulima. Hawana pa kulishia mifugo yao; hawana majosho na dawa na hawana soko zuri kwa mazao ya mifugo.

Mtetezi wa rais anajua tatizo sugu la uvujaji wa mitihani kila mwaka pamoja na lile la vyeti bandia. Anajua hakika hali ngumu ya maisha ya Mtanzania, inayozidishwa na mfumuko wa bei usiokwisha.

Anajua namna watoto wa wakulima na wafanyakazi wanavyohangaikia karo vyuoni; bali anajua Tanzania inahitaji wataalamu ili kutoa mchango katika maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayokwenda kwa kasi duniani.

Tuangalie uchumi wa taifa. Mtetezi wa rais anajua kuwa hakuna usimamizi wa raslimali na maliasili za nchi. Hawezi kukana kuona nguvu ya ufisadi na mafisadi wanavyomaliza nchi.

Anajua walafi, wezi, mafisadi wanavyolindwa kwa visingizio tele vinavyotolewa kwa lugha laini ya wale walipaswa kuwafichua, kuwakama na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Hivi kweli Salva hajui kuwa mtandao wa ufisadi ndio unakwamisha urekebishaji sheria ya madini na uwindaji hata kuthubutu kuchomeka vifungu vya sheria katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali, vinavyoruhusu uporaji maliasili na uharibifu wa mazingira?

Je, anajua jinsi serikali ya CCM ilivyoshindwa kuinua kilimo, licha ya hazina kubwa ya ardhi iliyopo kwa umwagiliaji? Hivi anajua kuwa bila ya kilimo cha kisasa hakuna uhakika wa chakula?

Tuseme kweli. Lazima Salva atakuwa anajua kuwa CCM imekuwa ikikataa kila jitihada za kupanua demokrasia. Haitaki katiba mpya, tume huru za uchaguzi wala mabadiliko ya sheria za uchaguzi. Haitaki bunge la viwango wala mgombea binafsi kwenye uchaguzi.

Vikosi vya ulinzi na usalama vinaendelea kutumika hata kuua wananchi; mfano ni mauaji ya 26 - 27 Januari 2001 huko Unguja na Pemba, ilimradi CCM itawale hata pale inapokataliwa.

Yote haya ni mifano bora ya kushindwa kwa CCM kwa vile katika utawala wake kunakosekana siasa safi na viongozi na uongozi bora.

Kushindwa kwa CCM ndiko kushindwa kwa Rais Kikwete. Kwa nini? Kwa sababu, asingekuwa ameshindwa angeona dosari zote hizo; angependekeza mabadiliko.

Mashambulizi ya Salva kwa wanaosema Rais Kikwete ameshindwa kazi ya kuongoza taifa, ni msukumo wa makusudi wa kung'ang'aniza kile ambacho wananchi wamechoka na wanasema hawataki.

Hali ya sasa ya utawala wa Kikwete ndiyo inachochea wananchi kutamani utawala mbadala; na hilo Salva analijua fika. Uongozi mbadala ni wa akina Profesa Lipumba na wenzake na vyama vyenye sera tofauti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: