Ni makosa kumhoji Spika nje ya Bunge


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

SPIKA wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta amefanya kazi iliyowashinda watangulizi wake, Pius Msekwa na Sapi Adam Sapi.

Sitta amelibadilisha Bunge kutoka kuwa taasisi ya chama tawala, hadi kuwa Bunge la wananchi. Tangu achaguliwe kuwa Spika, Desemba 2009, Sitta amejitahidi kulinda uhuru wa mawazo bungeni; uhuru ambao unalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Katiba, majadiliano ndani ya Bunge hayapaswi kuhojiwa na chombo chochote kile, kikiwamo chama kilichoko madarakani.

Hata yale yanayotamkwa bungeni yana kinga ki-Katiba. Hayo nayo hayawezi kuhojiwa na mtu yeyote ikiwamo Mahakama.

Hivyo kumhoji Spika, au mbunge yeyote kwa matamshi yake katika vikao vya bunge ni ukiukaji au uvunjaji wa Katiba. Ni bunge lenyewe tu kwa kanuni zake linaloweza kumhoji spika au mbunge yeyote na kumchukulia hatua.

Lakini kinyume na ukweli huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa makusudi kimejitwisha jukumu la Bunge kwa kuhoji kazi ya Spika Sitta katika vikao vyake vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) vilivyofanyika mjini Dodoma mwezi mmoja uliyopita.

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na yule wa Uenezi, John Chiligati, wamethibitisha Sitta kuhojiwa na kukaripiwa kwa madai kuwa amewapa uhuru mkubwa wabunge bungeni kuijadili serikali.

NEC haikufurahishwa na hatua ya wabunge kushupalia watuhumiwa wa ufisadi na hatua ya baadhi ya mawaziri kushidwa kuwajibika.

Chanzo cha yote haya, ni tuhuma za ufisadi zinazokabili baadhi ya wafanyabiashara, mawaziri na watendaji wengine serikalini ambao serikali imeshindwa kuwachukulia hatua.

Hivyo niliposikia kwamba kulikuwa na hoja za kumnyang’anya Sitta kadi ya chama ili kumuondoa katika ubunge na nafasi yake ya spika, haraka niliona hatari ya kuzuka mgogoro mkubwa wa kikatiba iwapo Sitta angefungua kesi mahakamani kukishtaki chama chake.

Ni dhahiri kwamba Sitta angeshinda na kurudishwa katika nafasi yake na mahakama.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaeleza wazi kuwapo kwa uhuru wa Bunge na jinsi linavyotaja "Uhuru wa Mawazo wa Wabunge na Bunge lenyewe," kwamba ni moja ya mihimili mitatu ya dola katika dhana ya mgawanyo wa madaraka ambayo ni kielelezo chake halisi cha utawala wa sheria.

Ibara ya 100 (1) inasema, "Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge."

Kutokana na ibara hii, ina maana kwamba na Kamati ya wazee inayoundwa na rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi, makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na spika wa zamani wa Baraza la kutunga Sheria la Afrika Mashariki, Abdurhaman Kinana, ni batili.

Kamati hii inaonekana inataka kupingana na Katiba ya nchi iwapo itajiingiza katika kuhoji uhuru wa wabunge na wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Nayo Ibara ya 100 (2) inatoa kinga kwa mbunge yeyote, akiwemo Spika ya kutoshtakiwa mahakamani kwa matamshi yake ndani ya Bunge.

Ibara hiyo inasema, "Bila kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au aliloleta bungeni kwa njia ya maombi, muswaada, hoja au vinginevyo."

Tukiiangalia ibara hii kwa tafsiri pana tutaona kwamba hata vikao vya ndani ya CCM kama vile CC na NEC, haviwezi kujadili matamshi ya mbunge yeyote ndani ya Bunge akiwemo spika mwenyewe.

Hii ina maana kwamba kauli ya Makamba kwamba spika asipohojiwa na CCM atahojiwa na nani, ni kielelezo kingine kuwa mzee huyu amechoka na anahitaji kupumzika.

Makamba anapaswa kufahamu kuwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge, spika anaweza kuhojiwa na Bunge lenyewe. Kwa mujibu wa sheria, Bunge ndilo lenye meno dhidi ya spika au mbunge yeyote yule. Mbunge au spika hawezi kuwajibishwa na chama chake.

Najua makada wa CCM kama Makamba na Chiligati hawatanielewa kwa vile wanasema, "Serikali ni ya CCM." Sawa nakubaliana nao kisiasa.

Lakini kisheria sio sahihi. Serikali ikishapatikana kupitia chama chochote kile, inakuwa ni serikali ya wananchi inayolindwa chini ya Katiba ya nchi ambayo inamhusu kila mwananchi bila ubaguzi wowote.

Tahadhari ni kwamba chama tawala kinaweza siku moja kutamka hadharani kwamba Mahakama nayo ni yake. Hii itakuwa ni hatari sana kwani uhuru wa mahakama unaolindwa na Ibara ya 107B utakuwa umevunjwa.

Chama hakiwezi, kwa mfano, kumhoji Jaji Mkuu au Jaji wa Mahakama Kuu au Hakimu yoyote (hata wa Mahakama ya Mwanzo) katika vikao vyake kuhusu uendeshaji kesi.

Tuelewe kwamba kumhoji spika nje ya Bunge kuhusu matamshi au utendaji wake wa kazi wa ndani ya Bunge ni ukiukaji au uvunjaji wa Katiba ambao unapaswa kuachwa mara moja ili kudumisha misingi ya utawala bora iliyoanza kuimarishwa nchini.

Badala ya kumsakama Spika Sitta, ni vema CCM ijue kwamba inaweza kumtumia msemaji wa serikali (waziri anayeshungulikia Bunge) kutetea serikali au kutumia kanuni zilizopo kumuomba spika kuipa muda serikali kujiandaa kutoa ufafanuzi wa masuala yanayoonekana yana utata.

Serikali inaweza kumtumia waziri mkuu, au mwanasheria mkuu kuitetea pale inapoona kuwa mambo yanakwenda mrama. Lakini kuendelea na utamaduni wa kale wa kutisha wabunge na spika, kunaiweka mahali pabaya zaidi serikali.

0715/0786 362 544 alloycekomba@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: