Ni nani aliye msafi ndani ya CCM


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

SASA hakuna anayeshangaa katika nchi hii anapopita mitaani, vijijini, machimboni na makondeni na kusikia watu wanasema kuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakuna aliyemsafi.

Ni jambo la kawaida hata ndani ya CCM wenyewe hawashangazwi na kauli hii. Mara nyingi ukweli haushangazi.

CCM wenyewe hawajishangai kwa sababu wanawaza namna moja. Watu wa fani moja huwa hawajishangai wakiwa katika fani yao mpaka pale wanapojilinganisha au kujitofautisha na watu wa fani nyingine au wasio na fani.

CCM imenyimwa uwezo wa kujilinganisha au kujitofautisha na wengine kutokana na fikra potofu kuwa chama tawala ndiyo kila kitu na ndiyo chama bora. Wanaona yote wayafanyayo kuwa ni sawasawa.

Matokeo yake ni kwamba viongozi wake wamekuwa na fikra zinazozunguka ndani ya duara. Siku zote hawana jipya. Wamebaki na sera na dhana zilezile, wanachofanya ni kubadilisha majina tu ya sera zao. Ikitoka sera ya ufisadi inakuja sera ya gamba, upuuzi uleule.

Wataimba ufisadi hata miaka mitatu mfululizo na wakiona wimbo huo unaanza kuwakifu wananchi wataanzisha wimbo wa kujivua gamba. Sera ni ileile ya chuki, fitina dhidi ya wengine kwa faida ya wafitini.

Walichofanya ni kubadilisha jina tu. Chuki na fitina ziko palepale. Mafisadi wanatuonyesha mafisadi wengine na wenye magamba wanawataka wengine ndiyo wavue magamba yao. Wamehubiri fitina, chuki mpaka wameishiwa maneno sasa wamebaki kutukana matusi kila wanapopanda katika majukwaa.

Ni bahati mbaya sana kwamba wengine wanafanya upuuzi huu huku wakitumia majina yanayofanana na ya wazee wetu waliyojijengea heshima kubwa katika siasa za nchi hii kama vile mzee wetu Job Lusinde!

Wilson Mukama, Katibu Mkuu wa CCM anaonyesha kufurahishwa na matusi aliyoyatoa Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde kule Arumeru Mashariki akidai kuwa alikuwa akijibu mapigo.

Waziri wa Uwezeshaji Mary Nagu anamshauri kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe kuachana na maneno yanayotolewa wakati wa kampeni kwani yanakuwa mengi na kwamba yakifuatwa yanaweza kusababisha kutoweka kwa amani nchini.

Anakiri yalikuwa ya kipuuzi. Lakini anasema kwake hiyo ndiyo siasa. Huu ni upungufu mkubwa. Siasa gani za kutukana wananchi? Baada ya matusi kushindwa wamekuja na mapanga na mashoka. Hizi nazo ni siasa?

Maneno ya upuuzi ndiyo yanayoweza kusababisha kutoweka kwa amani nchini. Hivi Nagu haelewi kuwa siasa na upuuzi ni vitu viwili tofauti?

Mukama alipopata ukatibu mkuu wa CCM aliahidi kuirudisha CCM ya Nyerere. Wengi walidhani sasa CCM imempata mtu. Alipoanza na yeye kuhukumu kwa kutumia tuhuma za upuuzi wa gamba akadhihirisha kuwa hayati Mwalimu Julius Nyerere hakuacha mtu wa kufuata nyayo zake.

Halafu Mukama amenukuliwa akisema, “Tatizo la nchi hii wajinga ni wengi kuliko werevu lakini haiwezekani nchi ikawa chini ya uongozi wa wajinga na wahuni ambao hawawezi kuliletea taifa manufaa.”

Hapa sijui ana maana gani. Viongozi wajinga na wahuni ni nani? Heri angewataja kwa sababu anawachanganya wananchi. Wananchi wanawajua viongozi wao waliopo.

Akaona hiyo haitoshi akaongeza, “Ndani ya CCM si watendaji wote ni Richmond”. Kumbe Mukama anajua uhuni uliofanywa hadi Richmond ikapatikana na sasa anawajua wahuni hao. Kwa nini chama chake kimeacha kuwashughulikia?

Mukama aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma dhidi yake ambazo zimetolewa katika vyombo mbalimbali vya habari zikimhusisha na ufisadi wa mabilioni ya fedha za miradi ya machinjio ya kisasa na maji katika Jiji la Dar es salaam alipokuwa akiiongoza iliyokuwa Tume ya Jiji.

Lakini tuhuma nyingine dhidi yake ni kuhusika kwake kuruhusu ujenzi wa bwawa la maji kwa ajili ya wananchi lakini likiwa kwenye ranchi ya mtu binafsi.

Katika utetezi wake Mukama alisema, “Ieleweke wazi kuwa, miradi inakufa inapotokea yule aliyepewa nafasi ya kuisimamia anapoondolewa na kuwekwa mwingine ambaye anashindwa kuiendeleza”.

Utetezi hakuishia hapo, akaendelea, “Inaonekana wengine wanatumia fursa hiyo kutaka kunichafua ili nionekane nashiriki ufisadi, mimi ni msafi, nafanya kazi kwa kuzingatia maadili na nina wito ndiyo maana pamoja na kuwa mstaafu bado nilionekana nafaa kuwa na wadhifa ndani ya chama.”

Angeacha wengine wamsifie kuwa ni safi. Lakini kujitangaza mwenyewe kunamwondolea sifa hata kama zingekuwako. Watanzania wenzangu hawa wanaoanza kuwaomba urais japo wa miaka mitano tu wakidai ni waadilifu, wazalendo, wavurumisheni wakafie mbele! Ni wanafiki wakubwa. Hawafai kwa urais hata kidogo!

Amesema taratibu za kisheria zipo, hivyo kama kuna mtu mwenye tuhuma kama hizo kuna vyombo ambavyo vinaweza kushughulikia. Leo ndiyo anayajua haya? Mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu. Anapowahukumu wenzake kwa tuhuma za gamba, hakumbuki kama kuna taratibu za kisheria na vyombo vinavyoweza kuwashughulikia?

Anajichanganya zaidi anaposema suala la kujivua gamba katika chama litaendelea. Hivi Mukama bado anaamini kuna mtu atajivua gamba mwenyewe! Ni kweli, baada ya kusakamwa sana Rostam Aziz anayedai kuwa ana mamlaka ya kisheria kusimamia kampuni ya Dowans, alijiuzulu kwa kile alichodai kuchoshwa na uongo, unafiki na siasa uchwara.

Hata hivyo, mbunge huyo wa zamani wa Igunga na mfanyabiashara maarufu nchini alikana kuhusisha hatua yake ya kujiuzulu na madai kwamba yeye ni gamba ndani ya CCM.

Uongozi wa juu wa CCM umekuwa ukiwaaminisha watu kwamba watu wengine wanaotuhumiwa katika sakata la rada na Richmond watajiuzulu lakini hakuna aliyefanya hivyo. Imekuwa kama hadithi ya fisi ambaye inadaiwa alimfuata binadamu akitegemea mkono ungedondoka.

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mdogo jimbo la Igunga, CCM ililazimika kumpigia magoti Rostam na kumwomba akasaidie kampeni. Alifanya hivyo na CCM ikashinda.

Maana yake nini? CCM haina ujasiri. Kuendesha chama kwa majungu na fitina wakati kumbe taratibu za kisheria zipo, ni uongozi wa kale sana, tena kabla ustaarabu haujaingia nchini mwetu. Kuutumia leo ni aibu kubwa!

Wananchi wamechoshwa na malumbano yasiyokwisha. Mipango ya maendeleo inafanyika saa ngapi? Watu wana maisha magumu wangependa kuona ufumbuzi wa shida zao!

Kama kila mtu ndani ya CCM anatuhumiwa kuwa ni fisadi, nani sasa msafi? Mukama anyamaze awaache wananchi waendelee na dhiki zao. Watakapopata ari na moyo watajua kuwa hakuna wa kuwakomboa bali wao wenyewe! Watatafakari na kuchukua hatua Mukama na CCM yake watakuwa watu wa kupokea majibu.

0713334239
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: