Ni ubaya wa Lowassa au udhaifu wa JK?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KADRI siku zinavyosonga mbele, hali ya baadaye ya chama chetu – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – ndivyo inavyozidi kutatanisha. Wanachama na wapenzi wa chama wamechanganyikiwa kwa sababu hawana kiongozi wanayeweza kumwamini ili awaelekeze waelekee wapi.

Anatokea kiongozi mmoja anasema kitu na kutoa msimamo, kabla hakijaanza kutekelezwa, anatokea mwingine na kufuta msimamo uliotolewa na kiongozi wa awali.

Kimsingi, hakuna wakati ambapo chama hiki kilikuwa hakijapata kukosa dira na mwerekeo katika historia yake, kuliko ilivyokuwa wakati huu tulio nao sasa.

Kwa kuwa kusema ukweli daima ni moja ya imani za chama chetu, ninaamini kwa dhati kuwa wakati umefika sasa ukweli usemwe ili kuokoa chama hiki.

Niliwahi kuhoji huko nyuma juu ya uhusiano wa Rais Jakaya Kikwete na rafiki yake wa siku nyingi Edward Lowassa. Kwamba urafiki wao ndio ulioleta awamu ya nne madarakani na inaelekea uhasama wao ndio unaelekea kuiondoa serikali hii madarakani kama tahadhari na hekima havitapatikana haraka.

Lowassa ni kiongozi “mbaya” mwenye ushawishi usioshindwa kirahisi. “Ubaya wake” ni uwezo wake wa kulazimisha na kusukuma mambo yaweze kutokea. Katika masuala ya msingi na yenye faida kwake binafsi na kwa jamii, anaweza kuyasukuma kwa muda mfupi na matokeo yakaonekana.

Tabia hii imemuongezea maadui ndani ya chama na serikali na kimsingi mvutano kati ya marafiki na maadui wa Lowassa ndio wanaofanya mnyukano wa sasa uwe mgumu sana ndani ya CCM.

Rafiki mmoja wa Lowassa ameniambia kwa kumtetea kuwa, “Edward kama Edward hana maadui kwa sababu wale wanaoitwa maadui wake walipatikana kwa gharama ya kumtetea Kikwete.”

Kwamba kabla ya Kikwete kuingia madarakani, Lowassa alifanya kazi kubwa ya kusajiri mtandao na kwa hiyo wale waliokataa kujiunga walijikuta wakikosana naye, lakini ilikuwa ni kwa niaba ya Kikwete.

Aliendelea kusema kuwa baada ya awamu ya nne kuingia madarakani na Lowassa kuteuliwa kuwa waziri mkuu, alijipatia idadi kubwa ya maadui miongoni mwa watendaji wa serikali kwa jinsi alivyokuwa akifuatilia masuala mbalimbali.

Aliyenufaika na ufuatiliaji wa Lowassa kwa watendaji ni Kikwete na wala siyo Lowassa; yeye aliambulia kununiwa na kuchukiwa. Alifanya jitihada nyingi usiku na mchana kuhakikisha rekodi ya utendaji wa Kikwete na serikali kwa ujumla inaimarika kila wakati, jitihada ambazo zilimuongezea maadui wa kisiasa.

Hata kashfa ya mkataba wa kuzalisha umeme ya Richmond ambayo inaelekea kuweka msumari wa mwisho katika maisha ya kisiasa ya Lowassa ndani ya CCM, inaelezeka katika mtizamo huu.

Kwamba, nchi ilikuwa inaingia gizani kama ambavyo imekuwa gizani hata baada ya kashfa hiyo. Lowassa kwa nafasi na hulka yake ya kulazimisha mambo, akafanya maamuzi yanayomgharimu mpaka leo.

Kisiasa anaweza kujitetea kuwa alikuwa anafanya hivyo ili serikali ya rafiki yake isiaibike mbele ya wapiga kura. Tamko la namna hiyo ni tusi kwa mkuu wa nchi na ndiyo maana zigo hili linamwelemea Lowassa mpaka leo. Anabeba gharama ya kutenda vema kwa njia mbaya. Na huo ndiyo ubaya wa Lowassa.

Kama alifaidika binafsi na hulka yake hii ya kulazimisha mambo, ni vema serikali ikafanya haraka kumchukulia hatua haraka kwa manufaa ya serikali na chama kilichopo madarakani maana kuchelewa chelewa kutawafanya wananchi waiadhibu serikali na chama chenyewe.

Wakati tayari Lowassa ameadhibiwa na bunge, ni vema CCM na serikali yake wakafanya haraka kuchukua hatua ya kumuondoa kiongozi huyo ndani ya chama ili kujinusuru na hasira ya wananchi wanaoweza kuiadhibu serikali na CCM kwa pamoja. Mpaka hapa, ni “ubaya” wa Lowassa unaoitesa CCM.

Lakini upo upande wa pili unaowakilishwa na udhaifu wa Kikwete kama Rais na mwenyekiti wa chama chetu. Rais na mwenyekiti mwenye udhaifu wa kiuongozi husababisha makundi ya watu wanaojipendekeza kwake au kujituma kufanya mambo ambayo yeye angefanya.

Matokeo yake, makundi haya husababisha minyukano inayoweza kudhoofisha taasisi yoyote. Yanapokosekana maamuzi ya wakati muafaka, ombwe hujitokeza na kuzalisha watendaji wengine wanaoweza kung’ara na kutishia mustakabali wa nafasi ya mtendaji rasmi wa taasisi.

Falsafa hii yaweza kwa sehemu ikaeleza nini kinaweza kuwa kimetokea ndani ya serikali na CCM pia. Kwamba, udhaifu wa Kikwete ambao wakati mwingine unaitwa “uungwana wake” kwa vile unatendwa na mkuu wa nchi, ndio unaosababisha makada wachinjane, wauane, wakamiane, wasingiziane, na hatimaye waangamizane kisiasa.

Hali ya nchi kwa sasa ni tete kisiasa, kiuchumi na hata kijamii. Wale wanaojipendekeza kwa Rais Kikwete ni wepesi kumshauri kuwa anayesababisha haya ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Na wengine wanamwambia sababu ni mapacha watatu. Hakuna anayemwambia rais kuwa udhaifu wake ndicho chanzo cha utete wa taifa.

Samwel Sitta akiwa Spika alijaribu na kudiriki kumwambia Kikwete kuwa wewe rais umekuwa mpole mno na kumshauri kama anaona sheria zilizopo hazimpi nafasi ya kutenda kazi yake kwa ujasiri aliombe Bunge limsaidie. Sitta aliamua kuwa muungwana kwa kumwita rais kuwa ni mpole; angeweza kusema ni mdhaifu kiuongozi na akabaki kuwa sahihi.

Licha ya utete katika sekta nilizozitaja hapo juu, utete wa msingi upo katika uwezo wa Rais Kikwete kuyaleta makundi hasimu pamoja na kuyatafutia ufumbuzi. Kutokana na udhaifu wake kiuongozi, yeye ameamua kukaa kimya na kukutana na kila kundi peke yake huku akilihadaa kila kundi na kuliambia msimamo wa kundi hilo ndio ulio sahihi.

Inapotokea fursa ya yeye kukutana na makundi yote kwa pamoja, silaha ya Kikwete imekuwa ni kutumia vijembe na mafumbo yasiyokuwa na mwelekeo wa kiutendaji. Hata katika semina elekezi iliyomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Rais Kikwete alitumia muda mwingi kueleza jinsi yeye anavyokerwa na uzembe serikalini badala ya kuonyesha ujasiri wake katika kutatua tatizo hilo serikalini.

Udhaifu wa Kikwete umelifikisha taifa mahali pagumu sana. Ili kurekebisha hali hii, gharama kubwa kisiasa na kiuchumi itatumika. Rais kwa hofu na aibu ya kusemwa sana na watu, anaweza kuzinduka na kuchukua hatua kwa jazba na hasira na kufanya makosa yanayoweza kuligharimu taifa kwa muda mrefu.

Ni hatari kwa kiongozi wa nchi kufanya maamuzi makubwa asiyoyaamini au yasiyotoka moyoni mwake. Lakini pia kwa kuwa amechelewa sana na kusitasita kwa muda mrefu, makundi hasimu ambayo yameishaumizana sana, yanaweza kuungana na kumfukuza yeye katika chama. Hutokea kwa nadra wake wenza wakaungana na kumrudi mme wao anayewagonganisha vichwa kwa kukosa msimamo kwake.

Mpaka sasa, kila kundi linamwona Rais Kikwete hana shukrani na hana msimamo bali ulaghai na ubabaishaji.

Kwa kuwa hiki ni kipindi cha mwisho cha Rais Kikwete, lolote linaweza kutokea kwa sababu kila kundi linajua kwa hakika kuwa rais huyu hawezi kuliathiri kwa muda mrefu. Na kwa kuwa harakati za kuutafuta urais wa mwaka 2015 tayari zimeanza, makundi yote ndani ya chama yanaweza kubadili mwelekeo endapo yataona rais aliyepo madarakani anapoteza ushawishi kwa kasi ya kutoweza kuandaa rais ajaye.

Binadamu huvutwa na maslahi na kwa hiyo makundi haya yanaweza kubadilika na upepo unaoonyesha dalili za rais ajaye yuko kundi gani. Hivi sasa hata wale walio karibu na Rais Kikwete, wanasema wazi kuwa kimaslahi Kikwete “halipi tena” na ni hasara kumtegemea ikiwa mtu una maisha marefu mbele yako katika uwanja wa siasa.

Katika masuala ya kuongoza kwa nchi kuongozwa na upepo badala ya fikra pevu zinazoweza kubadili upepo huo.

tutikondo@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: