Ni vita ya wakali Taifa Stars, Algeria


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version

KOCHA mkuu wa Taifa Stars, Jan Borge Poulsen sasa anakijua kikosi chake. Anawajua wachezaji na anajua uwezo wa kila mmoja.

Mdenmark huyo amewajua katika mazoezi na katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambe Stars ya Kenya ambapo zilifungana bao 1-1 kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ni kutokana na kuwajua wachezaji amemwita kipa Juma Kaseja wa Simba kwenye kikosi kitakacokwenda Algeria wiki ijayo kwa mechi ya kwanza ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Ni kutokana na kuwajua wachezaji ndiyo maana amemtema Kigi Makasi katika kikosi hicho ambacho kina kazi nzito ya kusaka pointi mbele ya Algeria ambayo ina historia ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mara tatu; 1982, 1986 na 2010.

Algeria, mbali ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara kadhaa pia imewahi kutwaa kombe hilo mwaka 1980 ilipokuwa mwenyeji.

Poulsen, ameteua wachezaji watakaopambana na timu hiyo yenye uzoefu. Mbali ya Kaseja makipa wengine ni Shaaban Kado (Mtibwa), na Jackson Chove (Azam FC).

Katika safu ya ulinzi amewateua Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub ‘Cannvaro’ (Yanga), Salum Kanoni, Juma Jab na Kelvin Yondani (Simba), Aggrey Moriis na Erasto Nyoni (Azam FC).

Viungo amewaita Jabir Aziz, Selemani Kassim (Azam), Athumani Idd ‘Chuji’, Nurdin Bakari, Abdi Kassim (Yanga), Abdulrahim Humoud, Uhuru Selemani (Simba), Idrisa Rajabu (Sofapaka), Henry Joseph (Kongsvinger, Norway).

Washambuliaji ni Daniel Mrwanda (Dt Long, Vietnam) Nizar Khalfan (Vancouver White Caps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam), Mussa Hassan Mgosi (Simba), John Bocco (Azam) na Jerry Tegete (Yanga).

Ngassa ndiye alifunga bao la kusawazisha katika mechi ya kirafiki dhidi ya Harambee Stars na ndiye alifunga bao la kusawazisha katika mechi dhidi ya Rwanda kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Jabir Aziz ndiye alifunga bao katika kipigo cha mabao 5-1 ilhali Erasto Nyoni alipachika bao lililoinyamazisha Burkina Faso mbele ya mashabiki wake mjini Ouagadougou. Burkina Faso ilichapwa 2-1 mjini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Stars iliyokuwa ikinolewa na Mbrazil, Marcio Maximo iliwahi kulazimisha sare dhidi ya Cameroun na Senegal nchini japo ilifungwa ugenini.

Sasa Poulsen anasema, "Nataka wathibitishe kwamba wanataka kuwa katika kikosi cha taifa. Nitawataka wajitume zaidi.”

Kocha mkuu wa Algeria, Rabah Saadane ametaja kikosi chake kitakachoikaribisha Taifa Stars mjini Blida Septemba 3, mwaka huu.

Wakati Stars ina nyota wane tu wanaocheza soka ya kulipwa Idrisa Rajabu (Sofapaka), Henry Joseph (Kongsvinger, Norway), Daniel Mrwanda (Dt Long, Vietnam) na Nizar Khalfan (Vancouver White Caps, Canada), kikosi cha Saadane kinaundwa na wachezaji 15 wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya.

Wengi wa wachezaji hao ni walioshiriki fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini mwaka 2010.

Amemwita kwa mara ya kwanza Mohamed Chakouri wa klabu ya Charleroi ya Ubelgij na amemrejesha Chadli Amri wa Kaiserslautern kuchukua nafasi ya majeruhi Medhi Lacen wa Racing Santander.

Nahodha Antar Yahia hatakuwepo kwa vile atakuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini.

Mwingine atakayekosekana ni Faouzi Chaouchi na Foued Kadir.
Mafanikio ya namna yoyote ya Taifa Stars katika mechi hiyo yatakuwa yameanza kujenga mazingira mazuri ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kufanyika Gabon na Equatorial Guinea mwaka 2012.

Baada ya mechi hiyo Taifa Stars itakwaana na Morocco na baadaye Jamhuri ya Afrika Kati ambazo zitakwaana Septemba 4, mwaka huu.

Jamhuri ya Afrika Kati, ambayo haina mazoea ya kushiriki mashindano ya kimataifa, imemteua Mfaransa, Jules Accorsi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa kwa mkataba wa miaka miwili.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 73 ndiye amepewa jukumu la kuiandaa timu hiyo kwa mashindano ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

"Tunahitaji matokeo mazuri kutoka kwake,” alisema Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika Kati Patrice Eduoard Ngaissona.

Kati ya timu hizo, ni Afrika Kati tu ambayo haipewi nafasi kubwa katika timu za Kundi D.

Tanzania ilifuzu kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980.

0
No votes yet