Nigeria haina cha kusherehekea


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version

IJUMAA iliyopita, yaani tarehe 1 Oktoba 2010, Nigeria iliadhimisha miaka 50 tangu ijipatie uhuru wake kutoka Uingereza.

Lakini katika kipindi chote hicho, Nigeria imekuwa ikikumbwa na misukosuko mikubwa, mapinduzi matano ya kijeshi, vita ya wenyewe kwa wenyewe, misuguano ya kidini na ya kikabila, umasikini uliokithiri licha ya utajiri mkubwa iliyo nayo wa mafuta yasiyosafishwa, na ufisadi wa kiwango cha juu kabisa barani humu. 

Nigeria ni nchi yenye idadi kubwa ya watu kuliko nchi nyingine yoyote katika bara la Afrika – takriban watu milioni 150. Ni nchi ya saba duniani kwa kutoa mafuta kwa wingi, na mafuta yao yote yanapatikana katika eneo moja tu – Niger Delta – eneo ambalo mto Niger unaingia katika Bahari ya Atlantiki.

Masuala ya ukabila na udini yameitesa sana Nigeria. Kuna makabila makuu matatu – Wafulani kutoka kaskazini, Wayoruba wa magharibi na Waigbo wa mashariki.

Ukabila ndio uliingiza nchi hiyo katika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1967 wakati wa utawala wa kijeshi chini ya Jenerali Yakubu Gowon.

Jimbo la Mashariki (ambako ndiko kulikuwa unafanyika uzalishaji wa mafuta yasiyosafishwa) lilijitenga kutoka serikali kuu ya shirikisho la Nigeria (Nigeria Fedral Government) ambayo ilikuwa na serikali za majimbo matatu – Kaskazini, Magharibi na Mashariki — kwa kufuata makabila hayo.

Jimbo hilo lilitangaza Jamhuri ya Biafra chini ya kiongozi wao—Kanali Chukuemeka Odumegwu Ojukwu, wa kabila la Igbo. Serikali ya shirikisho ikatuma majeshi kuzima uasi huo, katika vita ya umwagaji mkubwa wa damu iliyoisha mwaka 1970 baada ya kushindwa majeshi ya Biafra.

Tanzania, Ivory Coast na Zambia, ailiitambua Jamhuri mpya ya Biafra. Hatua hiyo ya Mwalimu Julius Nyerere haieleweki hadi leo, hasa ikizingatiwa alikuwa championi wa kuleta umoja wa bara hili, na mapema miaka ya 1960, alilaani kujitenga kwa jimbo la Katanga la Congo (sasa jimbo la Shaba) kutoka kwa serikali kuu ya Kinshasa.

Ili kuondokana na matatizo ya ukabila, baada ya vita vya Biafra, serikali iligawa Nigeria katika majimbo 12 badala ya yale makuu matatu. Sasa hivi Nigeria ina majimbo 36.

Uisilamu nao ulileta misuguano mikubwa katika jamii nchini humo na hawa wako wengi katika maeneo ya Kaskazini ambako kuna majimbo ambayo hutumia Sharia. Misuguano mikubwa pamoja na vurugu za umwagaji damu imezuka baina ya Waislamu na Wakristu wa eneo hilo la Kaskazini, bila ya serikali kuu kupata ufumbuzi wowote.

Sasa hivi Wanigeria wengi wanasema hakuna cha kusherehekea kwani nchi inarudi nyuma badala ya kwenda mbele, hali ambayo inaweza kuelezea kwa nchi nyingine nyingi katika Bara hili.

Kuthibitisha hali ya wasi wasi ilivyo nchini humo, siku ya Ijumaa milipuko miwili ilitokea karibu na paredi ya maadhimisho ya uhuru mjini Abuja na kuua watu takriban ishirini na kujeruhi mamia.

Kikundi kinachotetea ukombozi wa jimbo la Niger Delta (Emancipation of Niger Delta Peoples Movement) kimedai kuhusika na milipuko hiyo, ambayo kwa namna ilivyotekelezwa, ilikuwa ni ya kwanza nchini humo ambayo haihusishi vikundi vya Kiisilamu.

Kikundi hiki cha wazalendo kilianzishwa mwaka 2006 na kuanza kushambulia mitambo ya makampuni ya uchimbaji mafuta na sehemu za kuhifadhia mafuta, na katika kipindi kimoja kilifanikiwa kusababisha upungufu wa utoaji wa mafuta yasiyosafishwa kwa asilimia 40 – kutoka mapipa milioni 2.4 kwa siku hadi mapipa milioni 1.3.

Aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo katika miaka ya 1980, Jenerali Ibrahim Babangida, ambaye anawania tena urais (safari hii kwa kura) katika uchaguzi wa mwaka ujao, amemshutumu rais wa sasa, Goodluck Jonathan kwa kuingiwa kiwewe na kujaribu kupotosha umma alipotangaza kwamba kikundi cha MEND hakihusiki na milipuko hiyo.

Rais Jonathan alitangaza kwamba anawajua ‘magaidi’ waliofanya kitendo hicho na siyo wale wa kikundi cha MEND.

Wachunguzi wa mambo wanasema Jonathan alikuwa analenga vikundi vya Kiisilamu vyenye uhusiano na Al-qaeda, lakini baadaye MEND wenyewe waliibuka na kutoa tamko rasmi kwamba ni wao waliotega mabomu katika tukio hilo katika azma yao ya kupinga unyonywaji wa mafuta katika eneo lao huku wazalendo wakibaki na umasikini mkubwa.

Isitoshe, kikundi hicho kilikuwa tayari kimetoa tamko kwamba kinapinga maadhimisho ya kusherehekea miaka 50 ya uhuru kwani hakuna cha kusherehekea. Tamko hilo liliungwa mkono na Wanigeria wengi ambao wanaona utajiri wa nchi yao umeshikwa na wachache.

Lakini kama ilivyo katika nchi nyingine duniani zenye utajiri wa mafuta (na hata zenye madini mengine) raslimali hiyo imekuwa kero tu, utajiri hauleti manufaa yoyote kwa wananchi walio wengi, hasa katika maeneo yanakozalishwa.

Tangu wakati nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1960, tawala tofauti za nchi hiyo zimekuwa zikiingia mikataba na makampuni makubwa ya nje kuchimba mafuta kwa kiwango walichotaka, na karibu miaka 50 baadaye wakazi wa eneo la Delta wamekuwa wakiandamwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uharibifu mkubwa wa mazingira katika ardhi yao bila ya wao kupata tija yoyote.

Utafiti uliofanywa na taasisi moja ya uchumi ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) unabainisha kwamba kuanzia mwaka 1970, jumla ya dola za Kimarekani bilioni 550 zimeingia katika hazina ya nchi hiyo, ingawa leo hii, asilimia 75 ya Wanigeria wanaishi chini ya dola moja kwa siku.

Wakazi wa eneo la Niger Delta yanakopatikana mafuta hayo wanaishi katika umasikini mkubwa, bila shule, hospitali na miundombinu bora wakati fedha kutokana na faida ya mafuta yao yanavimbisha akaunti za benki za makampuni makubwa ya mafuta na viongozi wachache wa nchi hiyo.

Wazalendo hao waliamua kupambana vililivyo na mamlaka za makampuni haya ya nje na yalipata msukumo mkubwa na mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanamazingira – Kenneth Saro-Wiwa katika miaka ya 1990.

Saro-Wiwa alikuwa kiongozi wa kabila la Ogoni, wenyeji wa eneo la Delta na alipokuwa akiongoza mapambano ya amani dhidi ya makampuni ya uchimbaji mafuta, serikali ya dikteta Sani Abacha ilimkamata na kumpakazia mashitaka ya mauaji ya machifu wanne wa kabila lake.

Alihukumiwa na mahakama maalum ya kijeshi, akapatikana na hatia na kunyongwa mwaka 1995. 

Pamoja na kuwa na mafuta mengi, kuna wakati, katika kipindi cha utawala wa dikteta Abacha, nchi ilikuwa inaagiza mafuta yaliyosafishwa kutoka nje kwa ajili ya matumizi ya nchini. Hii ilitokana na migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi wa viwanda vya kusafisha mafuta (oil refineries).

Kulikuwa na utani kuhusu nchi hiyo wakati wa utawala wa kidikteta Abacha: kwamba inasafirisha kwenda nje bidhaa (demokrasia) ambayo yenyewe Nigeria ilikuwa haina na inaingiza kutoka nje bidhaa (mafuta) ambayo tayari inayo.

Utawala wa Abacha ulikuwa unapeleka majeshi Sierra Leone kulinda amani na kusimika demokrasia (vitu ambavyo yenyewe Nigeria haikuwa navyo) na kuagiza mafuta ambayo inayo tele.

0
No votes yet