Nina ‘taarifa za Intelijensia’


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
IGP Said Mwema

KILA masika yana mbu wake. Ni msemo waliotohoa wahenga. Zipo dalili nyingi mbu wa ‘masika’ msimu mpya wa 2011 amekuja na jina la: “Taarifa za kiintelijensia.”

Chama cha Wananchi (CUF) kilipotaka kufanya maandamano jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita kwenda kuwasilisha rasimu ya Katiba mpya kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, kilikataliwa na Polisi.

Polisi walisema ni kwasababu, “taarifa za kiintelijensia” zimeonesha kutakuwa na uvunjaji wa amani.

Mara mbili, wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha, wamekataliwa kufanya maandamano. Sababu ikawa ni hiyohiyo.

Matokeo: damu ilimwagika Dar siku CUF walipoandamana na kufanikiwa kufikisha rasimu yao ya katiba wizarani. Waandamanaji walijeruhiwa pale Polisi walipojitahidi kuvunja maandamano yaliyoanzia Buguruni, makao makuu ya chama.

Pili, damu ilimwagika katika tukio la tarehe 5 Januari mjini Arusha; na safari hii kulitokea mauaji ya raia yaliyotekelezwa na Polisi waliojitahidi kuvunja maandamano.

Damu imemwagika kwa mkono wa dola kupitia utendaji wa Polisi katika matukio yaliyopaswa kubaki ni ya kisiasa – ya wananchi kudai haki za msingi. Ni suala la kisiasa lililohusu raia na vyama vyao likaingiliwa na Polisi.

Kuzuia watu wasiandamane kwa kigezo cha “taarifa za kiintelijensia” ni jambo linaloweza kukubalika. Lakini haliwezi kukubalika kila mara kama polisi wanavyotaka iaminike.

Intelijensia ni neno lililotoholewa kwa Kiswahili kutoka neno la kiingereza la Intelligence ambalo maana yake ni “ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa hasa zinazohusu ulinzi na usalama wa nchi.”

Katika maandiko ya kale ya Lao Zu, mwanafalsafa wa China anayefahamika sana kwa kazi yake iliyoitwa The Art Of War, kuna fumbo alilopenda kulitumia mara kwa mara katika dhana ya intelijensia, akisema, “You nick it in the bud.”

Alikuwa na maana, “kama kuna tatizo lolote, kazi ya wanausalama ni kulimaliza kabla halijakua (halijatendeka).”

Kwa mfano, kama wasoma ramli watamwambia mfalme kuwa kuna mtoto nuksi atazaliwa na mama fulani, kazi ya wanausalama ilikuwa ni kwenda kumuua mama wakati mtoto hajazaliwa.

Ndiyo maana miaka zaidi ya 2000 iliyopita, mfalme Herode wa Israel, aliua watoto wote waliokuwa na umri wa chini ya mwaka baada ya kuambiwa Yesu Kristo, aliyezaliwa chini ya mwaka mmoja tangu taarifa zifahamike, atakuja kuwa Mfalme wa Wayahudi.

Mfalme Herode alitaka kuliondoa tatizo likiwa changa (halijakua) ili lisijesumbua utawala. Kwa kutoa mfano huu, sina maana vyombo vya usalama viue wasumbufu.

Ninaelimisha umuhimu wa kuzuia tishio pale tu linapobainika na siyo kulisubiri lije ndipo lidhibitiwe. Kufanya hivyo kunapunguza matumizi ya nguvu za kupita kiasi ambazo madhara yake huzidi matarajio.

Katika matukio yale mawili – CUF wakiwa Dar na CHADEMA wakiwa Arusha – Polisi hawawezi kuishia kutoa taarifa za kutisha watu kwa kisingizio cha taarifa ambazo ni wao tu wanaozijua.

Polisi wangejiuliza kwanza ni kwa nini watu wanataka kuandamana? Athari gani za kiulinzi na kiusalama zitakuja wakiandamana? Muhimu zaidi baada ya hapo, ni kuangalia athari zitakazotokea iwapo watu watakatazwa kuandamana.

Utamaduni ulioanzishwa na Polisi na washirika wake katika kuchunga ulinzi na usalama, si ajabu ukawa ndio kufuli kwa wananchi wanaotaka kutumia haki za kikatiba kukusanyika na kuandamana, matukio ya kisiasa yanapohusu wafuasi wa vyama.

Ni kawaida Polisi kuruhusu bila ya shida maandamano yanapokuwa ya kumpongeza rais, kupinga unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na watu binafsi au kufurahia ushindi kupitia labda Simba, Yanga au timu za taifa.

Imeshuhudiwa mara kadhaa Polisi wakivunja maandamano ya watoto wa shule ya msingi wanaolaani kuuawa kwa mwenzao kutokana na ajali ya gari na dereva mhusika kukimbia.

Polisi walivunja mkusanyiko wa wanawake wanufaikaji wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) wanaolalamika kutopatiwa mikopo inayotokana na amana zao; na imeshuhudiwa Polisi wakivunja mkusanyiko wa wanavyuo waliofika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kudai haki waliyonyimwa kwa miezi mitatu.

Utamaduni huo si mzuri katika jamii inayoamini katika utawala wa haki na demokrasia. Haki ya kuandamana imetolewa na katiba ya nchi kama miongoni mwa haki za msingi za binadamu.

Polisi wamewahi kupima hisia za wananchi kila wakikataliwa kuandamana? Ni wapi wamezieleza bayana taarifa za kiintelijensia? Au lini walikamata wahatarishi wa amani kabla ya tukio?

Kuendelea kwa utamaduni huu, kunaashiria kuanza kukaribisha mitizamo ya uongozi kandamizi. Chini yake, dola hupuuza haki za raia na kukandamiza raia wanapozidai.

Madai ya haki yanapokandamizwa kila mara, kinachofuata ni wakandamizwaji hao kutafuta mbinu nyingine. Ni hapo wadai haki – ambao sasa hujitambua kama wanyonge – hubeba mabomu ya kujilipua na kuhujumu dola inayowakandamiza.

Uongozi unaokandamiza raia hauna mwisho mwema. Utaishia na kujiapiza, “katu hatukubali.” Kiapo hicho huenda mbali mno. Watawala – siyo viongozi tena – wataapa hawataondoka madarakani hata wakilazimika kikatiba. Ndio udikteta wenyewe huo.

Haya si mageni duniani. Si mageni hata barani Afrika. Yametokea Zimbabwe. Kenya. Yanaonekana Ivory Coast. Kote huko, watawala wamejiotesha madarakani na wanatumia vyombo vya dola – Polisi, Usalama wa Taifa na Jeshi kujichimbia madarakani.

Inaonekana watawala wa Tanzania hawaamini wanakosea. Hawaamini kinachofanyika nchini sasa ni kukandamiza raia wasidai haki zao. Wala hawaamini kuwa madaraka ni jambo la kupata na kuachia kutegemea na ridhaa ya wananchi.

Kutoamini ukweli huo kwenyewe ni dalili za udikteta ndani ya akili za watawala na vyombo vyao.

Jaribu kumbana paka hadi kwenye kona. Nini kitatokea? Paka atataka kujiokoa. Wala hatakuwa na kosa kwa mbinu atakayotumia kujiokoa. Maisha yake ni muhimu sana. Raia anataka haki. Afanyeje?

Badala ya vyombo vya ulinzi na usalama kurahisisha haki, vinaikwaza. Vinatumia visingizio vya “Taarifa za kiintelijensia.” Waachie haki na wao wazuie kuvunjika kwa amani. Siyo kuizuia.

Tamko la “taarifa za kiintelijensia” litaanza kuchukuliwa kitu cha kawaida. Hata siku kutapokuwa na hatari ya kweli kiusalama, na raia wakionywa, watasema tu, “ah mambo ya kawaida.” Hii ni hatari.

Katika nchi zilizoendelea, watu hawauani wala kuumizana ovyo kama inavyotokea kwetu.

Polisi na Usalama husaidia kurahisisha raia kupata na kutumia haki zao. Wanaelimishana namna nzuri ya kuzitumia. Elimu inatolewa kwa nia njema siyo kisanii. Dola ni ya wananchi na hakika wananchi ndio wanaoiweka.

Nani angevunja amani wana-CUF wakimpeleka kiongozi wao, Julius Mtatiro, ofisini kwa Waziri wa Sheria na Katiba na kumkabidhi rasimu ya katiba? Lipi baya lingetokea CHADEMA Arusha wakikutana ili kumpongeza mbunge wao, Godbless Lema?

Ninahofia siku moja IGP Said Mwema, anaweza kufika MwanaHALISI na kuamuru, “Msichape gazeti wiki hii maana taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kutakuwa na uvunjaji wa amani.” Ni ukandamizaji tu uleule.
mwisho

 

Picha: Jakaya Kikwete

Busara gani ya Kikwete baada mauaji

Na Joster Mwangulumbi

KATIKA jamii za Kiafrika kuna imani na upo ushahidi kuwa wachawi ni wanafiki. Huwa na tabia ya kulia sana kwenye misiba ya watu.

Huweza kujigaragaza sana, kujibamiza na kububujika machozi ndoo nzima au kutoa maneno ya kuihurumia sana wafiwa. Yote ni katika kujenga mazingira ya mchawi kutoshitukiwa kuwa ndiye mhusika wa kifo. Huweza pia kutoa rai siku nyingine ashirikishwe katika kumtibu ili kuokoa maisha.

Katikati ya maombolezo ya vifo kadhaa vya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vilivyofanywa mjini Arusha, na salamu za pole kwa viongozi wa CHADEMA, rais Jakaya Kikwete amejitokeza kuonyesha “masikitiko.”

Anasema tukio la kuua wanachama wa CHADEMA lililofanywa na polisi wake, lilikuwa la “bahati mbaya” na halitarudiwa.

Ni kauli isiyo tofauti na ya washirikina. Rais alijua ni mara ya pili katika kipindi cha takriban wiki tatu polisi wake wamepiga wafuasi wa CHADEMA.

Kikwete, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini anajua hakuna shambulizi katika ngazi ya juu ya kitaifa bila yeye kuliidhinisha. Kwa hiyo, kama amri ya kuua ilitolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), rais lazima atakuwa ameidhinisha.

Ikiwa Kikwete atadai hakuwa na taarifa, anathibitisha kuwa hasomi magazeti, hasikilizi taarifa za habari na mijadala kupitia redio na televisheni, na hana watu wa kumpa taarifa ikulu. Kama anapewa taarifa, basi si msikivu.

Rais anajua wazi kwamba tangu umalizike uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, mikutano yote ya wabunge wa CHADEMA na viongozi wake wa kitaifa imepigwa marufuku na Polisi, lakini ile ya wana CCM inaendelea kila siku.

Kikwete anajua wazi kwamba kumekuwa na mvutano mkali wa upatikanaji wa mameya katika halmashauri zote ambazo CCM ina idadi ndogo ya madiwani kulinganisha na wale wa vyama vya upinzani.

Anajua fika kwamba ili CCM ishinde Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imehusika kupindisha taratibu.

Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika wameshiriki kupindisha taratibu. Siku ya uchaguzi wa meya Arusha, polisi walipiga madiwani wa CHADEMA na mbunge wao, Lema, ambaye ni mjumbe wa mkutano wa uchaguzi, hadi akalazwa.

Kwa nini wakati haya yanatokea, Kikwete hakusema kitu wala hakukemea? Alikaa kimya kama vile hakuna kilichotokea. Badala yake aliacha IGP Said Mwema aelekeze cha kufanywa na wapiganaji wake. Mauaji ni matokeo ya maelekezo hayo.

Kama Kikwete hajui haya yote, watu wana kila sababu ya kutilia shaka uwezo wake; maana upindishwaji wa kanuni Arusha ndio uliosukuma CHADEMA kudai haki yao kwa nguvu.

Kwa hiyo, anaposema atahakikisha matukio kama haya hayatokei tena, anataka kuwaambia watu kuwa amepata busara baada ya kuruhusu mauaji? Kwamba bila mauaji asingepata busara hii?

Mapema kabisa, Edward Lowassa, baada ya kupima hali ya jiji la Arusha, alishauri CCM wakae na CHADEMA ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi wa meya. Makamba alikataa na akamkejeli Lowassa ambaye ushauri wake ulikuwa umejaa busara na hekima kwa nia ya kuepusha maafa – nadhani hii ndiyo sababu baadhi ya watu (ukiacha kuhusika kwake katika kashfa ya Richmond) – wanamlilia alikuwa waziri mkuu wa vitendo.

Kwa vyovyote, Kikwete hakutaka kusikia wala kusoma ushauri wa Lowassa ila alifurahia majibu ya Makamba; akatuma polisi kudhalilisha, kusasambua, kupiga, kujeruhi na kuua raia anaowaongoza.

Sasa anaposema mauaji ya Arusha ni ya bahati mbaya ni unafiki na hata Jumuiya za CCM zinapolaani CHADEMA kwa wanachodai kwa kukiuka amri halali ya polisi, ni upuuzi mtupu. Damu iliyomwagika Arusha itakuwa juu ya mabega yao; Makamba; Mkuchika; IGP Mwema na bila shaka yoyote Waziri mkuu, Mizengo Pinda na Kikwete.

CCM iliandaa mauaji haya. Tazama, Polisi Mkoa wa Arusha waliruhusu maandamano na mkutano kufanyika viwanja vya NMC. Siku moja kabla, viongozi na wabunge wakiwa wamefurika, jioni ya siku ya mkesha wa maandamano na mkutano, IGP Mwema anatoa amri kusitisha maandamano ya amani halafu akapeleka mamia ya askari kutoka Moshi.

Awali polisi walitembea sambamba na waandamanaji kwa takriban kilomita mbili kwa amani lakini wakati msafara ukikaribia viwanjani NMC, wakatokea askari wengine na kuanza kupiga watu hadi kuwaua kwa risasi za moto.

Wakati wa Kikwete kuingilia kwa nia ya kuokoa uhai wa raia, ulikuwa ule – majuto ya sasa ni unafiki.

IGP Mwema anasema walipata habari za kiintelijensia kwamba kutakuwa na vurugu. Mbona watu wameona vurugu zikianzishwa na polisi? Mbona Polisi hawakushika wapangaji wa vurugu hizo kabla ya maandamano?

Ni upolisi gani huo wa kusubiri mipango ya vurugu itekelezwe ndipo ukamate mtu? Polisi makini hushika wapangaji na kuwashitaki mahakamani kwa ushahidi walioupata katika uchunguzi wao kabla ya utekelezaji wa mipango ya vurugu.

Kusubiri mipango itekelezwe, si ni kuruhusu kwanza watu wafe ndipo polisi ihangaike? Matokeo ya kesi kama hiyo ni watuhumiwa kuachiwa kwa sababu hakuna ushahidi wa maana uliopelekwa mahakamani. Utendaji mbovu wa polisi ndio chanzo cha maovu mengi nchini. Si ni polisi ambao Januari 2006 waliua vijana watatu wa Mahenge mpamoja na dereva wao wa teksi mkoani Dar es Salaam na kudai kuwa waliua majambazi? Mbona ilithibitika kuwa wale hawakuwa majambazi bali wafanyabiashara wema wa madini?

Tume ya Jaji Mussa Kipenka ilithibitisha kuwa polisi waliwaua vijana wale kwa kuwapiga risasi kikatili halafu wakajipongeza. Huu ndio utendaji wa polisi wetu.

Polisi wanatumiwa. Kama hawatumiwi na viongozi wa serikali kwa nini wameshindwa kuzuia wizi na uporaji fedha unaofanywa na viongozi wakuu kupitia kampuni za Richmond/Dowans, Meremeta, Kagoda, Deep Green na madini? Intelijensia gani inayojua masuala ya siasa tu?

CCM hupata busara baada ya kuua. Mwanzoni mwa miaka ya 1990 polisi walipiga watu waliokuwa wanadai demokrasia, lakini serikali iliishia kuruhusu vyama vingi.

Mwaka 1998 polisi waliwaua Waslamu pale Mwembechai, lakini serikali ikaishia kuridhia matakwa yao. Mwaka 2001 polisi wakishirikiana na askari wa vikosi vingine vya serikali walichinja wafuasi 21 wa CUF Zanzibar lakini serikali iliishia kuridhia katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kuiongoza CUF kuingia serikalini.

Baada ya kushuhudia polisi wakitii amri ya kupiga na kuua watu walioinyima CCM kura, rais Kikwete anaishia ‘kumwagiza’ Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha akutanishe viongozi wa CCM na CHADEMA. Suluhisho baada ya kuua!

Kikwete apokee ushauri wa maswahiba zake maaskofu waliomwita ni chaguo la Mungu, atengue matokeo ya umeya Arusha na ipangwe tarehe ya uchaguzi mpya. Pinda amshauri hivyo Kikwete kuepusha umwagaji mwingine wa damu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: