Ninavyoutazama Utumishi wa Umma Z’bar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

ZANZIBAR, ambayo sasa inaongozwa kupitia serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba mwaka huu, ipo katika mitihani mingi.

Inatokana na ukweli kuwa serikali hiyo mpya inatarajiwa kuendesha mambo kwa ufanisi mkubwa. Kila hatua ya utekelezaji kazi za serikali, inapaswa kulenga maslahi ya wananchi wa Unguja na Pemba.

Baada ya kuidhinisha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kufuatia uamuzi wao wa kukubali mapendekezo ya mabadiliko hayo kwa ushindi wa asilimia 66.4 wakati ilipoitishwa kura ya maoni 31 Julai mwaka huu, umefika wakati sasa wananchi kuipima serikali yao kiutendaji.

Utumishi wa umma ni nguzo muhimu katika utendaji wa serikali. Utendaji bora umeleta matokeo mazuri kwa nchi zilizoendelea kiuchumi, lakini unaendelea kuleta matatizo makubwa kwa nchi zinazoendelea au zilizo masikini.

Ndio kusema kutokana na utumishi wa umma ndipo maendeleo ya nchi hupatikana au hukwama kupatikana.

Utendaji mzuri wa watumishi wa umma huchochea ufanisi katika kazi za serikali. Kinyume chake, husababisha mkwamo. Ufanisi unapokosekana katika kazi za serikali, kinachofuata ni rushwa kujitanua.

Utendaji wa serikali hupimwa kwa yale yanayotendwa na watumishi wa serikali yenyewe siku kwa siku. Ni vipi wanatekeleza wajibu wao? Kwa kiasi gani watumishi wanazingatia misingi ya utumishi wa umma? Misingi ya utawala bora ni muhimu katika kutumikia watu. Haya ni mambo muhimu kwa sasa.

Lakini kipimo kizuri zaidi cha utumishi wa umma ni tija. Ni kwa namna gani huduma zinatolewa. Muda unaotumika mtu kupata huduma, una maana kubwa katika dhana hii.

Utumishi wa umma umekuwa ukitajwa kama miongoni mwa vikwazo vikuu vya maendeleo Zanzibar. Kiwango cha ufanisi hakijaridhisha.

Urasimu mbaya – maana urasimu kwa jumla ni utaratibu wa kiserikali, bali ukitumika vibaya ndipo hukwamisha tija – umezidi. Matokeo yake, umechipusha rushwa na ufisadi. Ni mambo yaliyoota mizizi.

Unaposikia msimamizi wa mashine ya mionzi X-Ray ya kuchunguza ukubwa wa maumivu katika mwili, anahitaji “kushituliwa” ndipo afanye kazi; muuguzi anapodai kitu kidogo (KK) ili akuhakikishie kumfuatilia mgonjwa wako aliyelazwa.

Unapolazimika kutoa chochote ndipo upatiwe mita na mafundi wa kukuungia umeme; na unapolazimika kulisha makarani wa kitengo cha usajili wa kesi ndipo na yako isajiliwe, ujuwe rushwa imekua sana.

Na hizo ni rushwa zinazohusu watumishi wa ngazi ya chini na kati tu. Zipo rushwa kubwa zinazohusisha maofisa mpaka mawaziri. Wapo wanaochelewesha hatua kwa makusudi ili walipwe malipo ya haramu.

Hutokea ofisa akakalia barua mezani kwake bila sababu nzuri. Inapokuwa mwenye shida husika anasubiri maombi yake hapo ili aendelee mbele, hujikuta amelazimika “kuzungumza.” Wasiojali huamua kushibisha ofisa.

Mfanyabiashara anayetaka leseni au kibali cha kutumia ardhi anayokusudia kuwekeza ambaye maombi yake yamechukua muda mrefu kushughulikiwa anafanyaje? Lazima atoe KK ili suala lake limalizike vizuri.

Inapotokea muagiziaji bidhaa anasubiri maombi yake ya msamaha wa kodi lakini waziri mhusika anajishughulishashughulisha hivi, ilhali ndiye mwenye mamlaka ya kuamua, huyu mfanyabiashara afanyeje? Anatoa rushwa ili apate msamaha.

Pale mwenye meli ya uvuvi katika bahari kuu anapokosa leseni wakati mwenzake alishaipata, afanyeje? Atatoa malipo halali na na ziada kumlainisha ofisa mhusika. Rushwa kama kazi.

Mazingira hayo yanaleta vifo vya wagonjwa – wakiwemo majeruhi – hospitalini, yanavunja haki za binadamu magerezani, katika vituo vya polisi, bandarini na kadhalika. Ufanisi duni unatafuna utendaji katika sekta ya umma. Na hapa ndipo Zanzibar ilipo sasa.

Lakini lipo tatizo kubwa jingine katika utumishi wa umma Zanzibar na inawezekana limechangia mno ufanisi duni. Watumishi wengi hawana sifa za kazi wanazozifanya.

Utafiti wa kisayansi uliofanywa na Waingereza katika awamu ya sita ya serikali ya Amani Abeid Karume uligundua kuwa ni asilimia 20 tu ya watumishi wote wana sifa za kazi walizopangiwa.

Kwa lugha nyingine, watumishi 80 katika 100 wanajifanyia tu kazi kwa mazoea kwani hawana sifa za kazi hizo. Takwimu hizi zinatisha na kuilazimu serikali kutafuta dawa ya kudumu.

Wapo watumishi wengi waliopangiwa kazi mahali pasipohusika na taaluma zao. Mhasibu mmoja aliyejieleza mpaka akaanza kulengwa machozi mbele yangu, kwa uchungu, ana miaka miwili sasa hajapangiwa kazi baada ya kurudi masomoni.

Anaendelea kwenda ofisini na kurudi bila ya kufanya kazi aliyosomea maana hajapangiwa. Bado analipwa mshahara kila mwisho wa mwezi. Hasara iliyoje?

Hivyo wapo watumishi wana hamu ya kufanya kazi walizosomea, lakini wananyimwa nafasi. Wengine wamepangiwa kazi lakini hazifanyiki kwani wengi wamepangiwa katika sehemu moja. Haya ni matumizi mabaya ya nguvukazi.

Haya ninayadurusu makusudi ili kusaidia viongozi wakuu wa wizara mpya ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliyoundwa na Dk. Ali Mohamed Shein, rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi la serikali ya umoja wa kitaifaa.

Haji Omar Kheri ndiye waziri chini ya ofisi ya rais. Huyu ni kiongozi mzoefu katika Baraza la Wawakilishi akiwakilisha jimbo la Tumbatu. Amekuwa mnadhimu wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mjumbe katika Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Anajua wajibu.

Amekabidhiwa wizara nguzo kubwa kwa utendaji wa kiwango serikalini kote. Utumishi bora utaleta tija katika uchumi na ustawi wa jamii. Bali utumisho bomu utakwamisha yote hayo.

Asimamie eneo hili kwa kulea vema watumishi wote wa serikali akianzia na wale walioko Ikulu au ofisi kuu ya rais. Wengine wapo ofisi za makamu wawili wa rais.

Watumishi wengine wapo kwenye wizara huku wengine wakipatikana katika mashirika na taasisi za serikali zilizo chini ya wizara hizo.

Waziri Kheri, ingawa hana naibu waziri, amepewa jukumu la kuhakikisha utumishi wa umma unaleta tija siyo balaa. Unachangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Lengo la Rais Dk. Shein kuanzisha wizara hii, ninaamini, ni kutoa nafasi ya usimamizi wa karibu wa watumishi wa umma kwa ajili ya kuchochea tija katika shughuli za serikali.

Watumishi wajulikane idadi yao. Walipo. Vijulikane viwango vyao vya elimu na mahitaji ya kuendelezwa; wajulikane matatizo yao na mazingira wanayofanyia kazi.

Watumike vizuri. Wenye ujuzi waenziwe na wasiokuwa nao wasomeshwe. Haifai kufanya kazi kwa mazoea peke yake. Kazi zitaharibika, matumaini ya watu yatapotea. Uchumi utaganda, huduma za jamii zitakufa.

Kila mtumishi afanye kazi anayopaswa kuifanya. Aifanye kwa bidii na apimwe kwayo. Watumishi wawajibike na hili linalazimisha wizara hii kupanga upya watenda kazi waliopo. Ajira mpya iruhusiwe bali kwa uangalifu mkubwa.

0
No votes yet