Nini kilisukuma Ocampo kugusa vigogo?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version
LUIS  Moreno Ocampo

BAADA tu ya matokeo ya uchaguzi wa rais wa Kenya kutangazwa, kikosi cha mauaji kilianza kutekeleza mipango yake. Ni mtandao uliolenga kushambulia wafuasi wa chama cha People National Union (PNU), maeneo ya Wilaya ya Uasin Gishu na Nandi.

Mashambulizi hayo yalianza 30 Desemba 2007 na kukoma mwisho wa wiki ya kwanza ya Januari 2008.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na makachero wa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague, Uholanzi, chini ya Mwendesha Mashitaka wake, Luis Moreno Ocampo, maeneo yaliyolengwa ni pamoja na mji wa Turbo, Eldoret, Kapsabet, Milima ya Nandi kwa nia ya kuwafukuza eneo la Bonde la Ufa.

Mauaji ambayo ndio chimbuko la wito wa Ocampo, yalitekelezwa zaidi eneo la kilomita 25 kutoka nyumba inayomilikiwa na kiongozi mwandamizi wa Orange Democratic Movement (ODM), William Ruto iliyopo Sugoi, wilayani Uasin Gishu ambako mikutano ya kupanga mauaji ilifanyika.

Mashambulizi ya wanamtandao yalifanywa kwa staili moja. Watekelezaji walikusanyika mahali walipangiwa na kukutana na waratibu wa mpango.

Mauaji yalifanywa kwa mpangilio; wakati wengine walikwenda kwa miguu, wengine walitumia malori.

Mwandishi wa habari na mkurugenzi wa kituo cha redio cha Kass FM, Joshua Arap Sang, alieneza ujumbe uliorekodiwa mahsusi kwa ajili ya kuwapa taarifa “wauaji” kuhusu maeneo yaliyolengwa.

Walioitwa katika mahakama ya kimataifa kujibu tuhuma za kuchochea mauwaji, ni pamoja na William Ruto, Joshua Sang na Henry Kiprono Kosgey, waziri wa ukuaji wa viwanda katika serikali ya pamoja.

Wengine ni naibu waziri mkuu na waziri wa fedha, Uhuru Mugai Kenyatta, katibu wa baraza la mawaziri, Francis Kirima Muthaura, na mkuu wa polisi mstaafu, Mohammed Hussein Ali.

Wito wa kuitwa katika mahakama hiyo ulitangazwa na Ocampo mwenyewe 15 Desemba 2010.

Msimamo wa ICC ni kwamba kwa kuzingatia ushahidi uliokusanywa, na bila ya kuathiri taarifa nyingine za kijinai ilizonazo, zipo sababu za kutosha za kuamini kuwa wakati wa uchunguzi wa awali, kipindi cha kuanzia 27 Desemba 2007 hadi mwisho wa Januari 2008, Ruto, Kosgey na Sang, walitenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Kwanza, waliua kinyume cha Ibara 7(1)(a) ya Sheria ya ICC; Pili, walifukuza au kulazimisha watu kadhaa kuhama makazi kinyume cha kifungu 1(d) cha sheria hiyo.

Tatu, ICC inasema Ruto, Kosgey na Sang walitesa na Nne, walisababisha usumbufu kwa mitizamo ya kisiasa, kinyume cha Ibara ya 7(1)(h) ya Sheria ya ICC.

Vilevile, upande wa mashitaka unaona zipo sababu za kutosha za kuamini kwamba mahitaji ya kuhusika moja kwa moja au kinyume chake kwa watuhumiwa hao yametimia.

Mashitaka yote yanajumuisha vifungu G.2, G.3, na G.4 pamoja na kile kinachoitwa, “Fungu la Taarifa.”

Vifungu hivyo vinabainisha maelezo ya kina ya kuwepo mtandao, kufanya mikutano ya ndani na ile ya hadharani; kuendesha mashambulizi; na ushiriki wa Ruto, Kosgey na Sang.

Ndipo, Mwendesha Mashitaka wa ICC, alipohitimisha hoja yake kwa kusema, “Watajwa wote wafike mbele ya mahakama kwa kuzingatia Ibara 58(2)(A).”

Wasifu wa Watuhumiwa

William Samoei Ruto alizaliwa 21 Desemba 1966 kijijini Kamagut, wilaya ya Uasin Gishu, Mkoa wa Bonde la Ufa, Kenya.

Kwa kabila, Ruto ni Mkalenjin. Ameoa na ana watoto. Anamiliki angalau nyumba moja eneo la Sugoi, jimbo la Eldoret Kaskazini.

Alisomea elimu ya msingi kijijini Kamagut na sekondari ya Wareng, wilayani Uasin Gishu, na Kapsabet, wilayani Nandi. Baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi. Anazungumza kwa ufasaha lugha ya Kiingereza, Kiswahili na Kalenjin.

Alijiunga rasmi na siasa mwaka 1992 akiwa Chuo Kikuu Nairobi. Hapo, alikuwa mmoja wa waliokuwa vinara wa Umoja wa Vijana wa Chama cha KANU (Youth for KANU ’92, kundi lililomuunga mkono aliyekuwa rais wakati huo, Daniel Arap MOI katika uchaguzi mkuu.

Katika uchaguzi mkuu wa 1997, alichaguliwa mbunge wa Eldoret Kaskazini. Alitetea kiti hicho katika uchaguzi wa mwaka 2002 kupitia KANU. Mwaka 2007, alichaguliwa tena mbunge, lakini safari hii kupitia ODM.

Aliteuliwa naibu waziri wa nchi ofisi ya rais mwaka 1999 na mwaka 2002  aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani.

Ruto na wenzake kadhaa waliokuwa wapinzani wa katiba mpya mwaka 2005 chini ya serikali ya Mwai Kibaki, walianzisha ODM katika uchaguzi mkuu wa 2007 akiwa mmoja wa viongozi waandamizi. Mwaka 2006, alitangaza nia ya kugombea urais nchini Kenya.

Hata hivyo, ODM ilimteua Raila Odinga kugombea uchaguzi huo wa 2007. Alibaki mmoja wa viongozi watano wakubwa walioitwa Pentagon.

Aprili 2008, Ruto aliteuliwa waziri wa kilimo katika serikali ya ushirikiano. Aprili 2010, alihamishiwa wizara ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia hadi alipotimuliwa kazi Oktoba 2010.

Henry Kiprono Kosgey

Kosgey, Mkalenjin, alizaliwa mwaka 1947. Ana shahada ya kwanza ya sayansi (B.Sc. Hon), aliyoipata Chuo Kikuu cha Nairobi. Anamiliki nyumba eneo la Milima ya Nandi, jimbo la uchaguzi la Tinderet.

Alichaguliwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1979 kupitia chama cha KANU. Alitetea kiti chake mwaka 1983. Akapoteza uchaguzi wa 1987 lakini akarudi bungeni kuanzia 1992 na 1997.

Mwaka 2002 akachaguliwa tena kupitia tiketi ya KANU. Mwaka 2005, naye akapinga katiba mpya na mwaka 2006, akaungana na Ruto kuingia ODM kama viongozi wa ngazi ya juu. Mwaka  2007 akachanguliwa tena kuwa mbunge kupitia ODM. Kwa sasa, ndiye mwenyekiti wa ODM.

Kosgey amekuwa waziri wa usafiri na mawasiliano (1980/1985); waziri wa maendeleo ya ushirika (1985/1986); waziri wa utamaduni na Huduma za Jamii (1987/1988); Waziri wa Mazingira na Maliasili (1996/1997); Waziri wa Utalii (1998/1999); Waziri Sayansi na Teknolojia (1999/2001); Waziri wa Elimu (2001/2006); na tangu 2008, amekuwa Waziri wa Ukuzaji Viwanda.

Joshua Arap Sang

Sang, Mkalenjin, alizaliwa Kitale, wilayani Trans Nzoia, Mkoa wa Bonde la Ufa na kusomea Kitale mpaka sekondari hadi mwaka 1993. Alijiunga na Chuo cha Mawasiliano (KIMC) alikohitimu mwaka 2006.

Tangu mwaka 2005 amekuwa mtangazaji wa kituo cha redio cha KASS FM. Lakini kabla, alifanya kazi kituo cha redio cha Sayare, baadaye kituo cha redio cha Kikristo cha Husema hadi alipohamia KASS FM.

Kwa sasa, Sang ndiye mkurugenzi wa kituo mjini Nairobi ambako ndiko anakoishi.

Kampeni ya kupinga katiba mpya ilipoanza mwaka 2005, Sang aliendesha vipindi vya midahalo ya wazi na kuviita “Lene Emet” – “Ilivyo Kenya” au “Hivi ndivyo Dunia ilivyo” au “Nini maoni ya Nchi.” Alitoa maoni ya watu kwa mada tofauti. Kipindi hicho kinaendelea kurushwa.

Sang anashirikiana sana na Wakalenjin wanaoishi nje. Alihudhuria mikutano mikubwa iliyofanyika 2007 na 2008 chini ya uandalizi wa Taasisi ya Emo, waliyoanzisha Wakalenjin wa nje, ambako aliitwa “Mtangazaji mahiri wa KASS FM.”

0
No votes yet