Nini kinamuandama Dk. Mwakyembe?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 12 October 2011

Printer-friendly version

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe yuko nchini India anakopatiwa matibabu ya afya yake. Amelazwa kwenye hospitali maarufu nchini India ya Indraprastha Apollo iliyoko mjini Chinai.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ubalozi wa Tanzania jijini New Delhi na ndani ya hospitali hiyo, tayari madaktari wa Dk. Mwakyembe wamechukua vipimo mbalimbali kwa lengo la kufahamu kinachomsibu.

Hadi gazeti linakwenda mitamboni juzi Jumatatu, madaktari nchini India bado walikuwa wanaendelea kuchunguza afya yake.

Naye balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi ameeleza MwanaHALISI, “Dk. Mwakyembe amefika salama Chinai; madaktari wanaendelea na uchunguzi wao.” Aligoma kutaja kinachomsumbua mwanasiasa huyo kwa maelezo kwamba hajapata ripoti kamili ya daktari wake.

Naye daktari anayemhudumia Dk. Mwakyembe amesema, “…Bado tunaendelea na uchunguzi.”

Alipong’ng’anizwa kueleza angalau kwa ufupi kinachomsibu Dk. Mwakyembe, haraka alisema, “…Kimaadili hatuwezi kukueleza taarifa za mgonjwa wetu. Elewa tu kwamba vipimo vyake vinafanyiwa uchunguzi,” alisema kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Wakati hayo yakitendeka nchini India, hapa nyumbani kumezuka mjadala kuhusu hasa kitu gani kinachomuandama Dk. Mwakyembe.

Kabla ya kuondoka nchini, mke wa Dk. Mwakyembe, Linah Mwakyembe alinukuliwa akisema, “…Tatizo la mwili kuvimba, lilianza miezi mitatu iliyopita. Linakuja na kupotea. Lakini sasa naona kama hali inazidi kuwa mbaya.” Dk. Mwakyembe ameondoka nchini akiwa amevimba mwili mzima.

Mwanasiasa huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa wakati alipoteuliwa kuongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond, hajawahi kulalamika kuumwa isipokuwa amewahi kuripoti hofu ya usalama wake.

Tangu kusomwa bungeni ripoti ya Richmond, Februari 2008, Dk. Mwakyembe amekuwa akidai kufuatwafuatwa ikiwemo mbinu za kutaka kumuua kwa njia mbalimbali.

Tarehe 9 Februari 2011, Dk. Mwakyembe aliandika barua ya kurasa saba kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema akisema kuna genge la watu limepanga njama za kumuua.

Katika barua hiyo, aliyoipa kichwa cha habari, “Taarifa ya njama za kuondoa maisha yangu na ombi kwa jeshi la polisi kulinda haki yangu ya kikatiba ya kuishi,” Dk. Mwakyembe alitaja watu wengine saba kuwamo katika orodha ya wanaotakiwa kuuawa.

Waliotajwa na Mwakyembe kwamba wako mbioni kuuawa, ni pamoja na katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, mfanyabiashara mashuhuri nchini, Reginald Mengi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Melecela.

Kwa karibu miezi mitatu sasa, Profesa Mwandosya amekuwa akikabiliwa na tatizo la uti wa mgongo na anaendelea kutibiwa nchini India. Akiwa huko, amevumishiwa kifo mara mbili.

Kuhusu malalamiko yake kwa IGP Mwema, Dk. Mwakyembe anasema, “Pamoja na kwamba taarifa hii ni mpya yenye matukio ya takribani mwezi mmoja tu (wakati huo), naamini kwa dhati kuwa msingi wake – kwa maana ya wahusika na maudhui –hautofautiani na ule wa matukio mengine ya awali ambayo baadhi yake yalisharipotiwa polisi na vyombo vingine vya usalama kwa lengo la kuchunguzwa.”

Anasema pamoja na hayo, bado ana imani kubwa na jeshi la polisi kuwa litaifanyia kazi taarifa hiyo bila kujali nguvu ya ukwasi na ya kisiasa ya watuhumiwa.

Msingi mkuu wa yeye kuamua kuviarifu vyombo vya dola, anasema Dk. Mwakyembe, ni taarifa alizozipata kutoka Songea, 22 Januari mwaka huu kuhusu kundi la watu saba lililoingia mjini Songea usiku wa 21 Januari kwa gari linalodaiwa kuwa ni la wizara yake.

Gari hilo aina ya Land Cruiser lilikuwa na namba za usajili STK 6868, lakini baadaye namba ilibadilishwa na kusomeka STK 6869.

Pamoja na kuthibitisha kupata barua ya malalamiko ya Dk. Mwakyembe, IGP Mwema alisema ilikuwa wanafanyia kazi malalamiko hayo. Hakutoa taarifa zaidi bali alielekeza aulizwe Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai wa Polisi (DCI), Kamishna Robert Manumba kwa maelezo zaidi.

Hofu ya Dk. Mwakyembe kutishiwa maisha yake, ilikuja chini ya miaka miwili tangu apate ajali ya gari iliyomtikisa taya lake ingawa hali yake iliimarika.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Ihemi, mkoani Iringa akiwa kwenye gari lake aina ya Toyota Lancruiser, Na. T 362 ACH. Alikuwa akitokea Mbeya kuja Dar es Salaam. Yeye alipata mshtuko wa shingo, huku dereva wake, Joseph Msuya, akipata michubuko mwilini.

Ajali hiyo ilizusha lawama nyingi kwa jeshi la Polisi baada ya kuwatuhumu kwa uzembe trafiki wawili waliokuwa wamepita eneo la tukio huku Dk. Mwakyembe akiwa hajasaidiwa.

Mmoja wa trafiki hao alilalamikiwa kuwa alivunja moyo wasamaria waliotaka kutoa msaada kwa kuwaambia, “Msaidieni huyo dereva kwani Dk. Mwakyembe ameshafariki.”

Tuhuma hizo zilipata nguvu pale kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi alipovieleza vyombo vya habari kuwa ajali hiyo ilitokana na “uzembe wa dereva” wa Dk. Mwakyembe.

Kamanda Nyombi alisema gari la Dk. Mwakyembe lilianguka kwasababu ya mwendo wa kasi uliomfanya ashindwe kumudu usukani baada ya kupitwa kwa ghafla.

Maelezo hayo yamepingwa na Dk. Mwakyembe akisema kuwa yalitokana na taarifa zisizokuwa sahihi na ambazo hazikuzingatia hali halisi ya tukio la ajali lilivyotokea.

Polisi wa Usalama Barabarani hawakusimamisha na kutambua lori hilo ambalo Dk. Mwakyembe na dereva wake walisema ndilo lililosababisha ajali. Walituhumu polisi kwa kutoa taarifa wakati hata uchunguzi wa kina haujafanywa.

Polisi hawakusema kama walilinasa lori hilo au iwapo walimhoji dereva wake kama sehemu ya uchunguzi.

Mwenyewe Dk. Mwakyembe alimtetea dereva wake akisema kuwa ufundi wa kazi alioonesha uliwanusuru na maafa.

Katika kipindi cha maandalizi ya ripoti ya Richmond kuwasilishwa mbele ya mkutano wa Bunge, taarifa zinamnukuu Dk. Mwakyembe akisema walikuwapo watu waliotaka kumhonga Sh. 50 milioni ili kuficha ukweli.

Baadhi ya wajumbe wa kamati, akiwamo Lucas Selelii ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Nzega (CCM), walidai kwamba kilitengwa kitita cha Sh. 10 milioni kwa kila mjumbe ili kuwalainisha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: