Nini matarajio ya Jumamosi Pemba?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SIKU 38 baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kusitisha uandikishaji kwa ajili ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar, kazi hiyo inaanza tena Jumamosi 12 Septemba 2009.

Ilipositisha, ZEC ilisema imeshindwa na vurugu vituoni ambako walibaini watu wamegoma kufika kuandikishwa.

Vurugu hasa zilitokea jimbo la Ole, Wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini, wananchi waligoma wakitaka kwanza wenzao wote wapatiwe vitambulisho.

Nini chimbuko la vurugu? Nani wahusika wakuu? Je, tatizo limetatuliwa? Je, yapo mazingira ya utulivu sasa hata ZEC imerudi? Haya ni maswali muhimu kuyajibu.

Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, kilicholetwa kisheria na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kimethibitika kwa kila namna kuwa ndio chimbuko la matatizo ya watu kunyimwa kuandikishwa. Wote wasiokuwa nacho hawaandikishwi. Hadi sasa watu wengi wenye sifa bado hawajaandikishwa.

Je, tume inaporudi tena vituoni kuandikisha wapiga kura, itapata watu wa kuwaandikisha? Au inataka kusema kuwa tatizo la kitambulisho limekwisha?

Kwenye mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Tume, Khatibu Mwinyichande alisema, “Tulisimamisha uandikishaji baada ya watu waliokuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapigakura kutoingia (vituoni) na hivyo kuonekana kulikuwa na viashiria vya vurugu katika vituo vya uandikishaji.

Anasema busara ya tume kuahirisha uandikishaji kwa muda ili kutoa nafasi kwa wadau wa uchaguzi ikiwemo serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wananchi kwa pamoja kutafakari matatizo yaliyojitokeza.

Anasema “Tume ya Uchaguzi ina imani kipindi cha mwezi mmoja cha kusimama kwa zoezi hilo limetoa fursa nzuri kwa vyombo vinavyohusika kutatua matatizo madogo madogo yaliyokuwepo.”

Ni kauli isiyoonyesha uwajibikaji hata kidogo. Bali inathibitisha mgogoro mkubwa unaohusu suala la uimarishaji daftari la wapigakura.

Ukweli ni kwamba Tume ipo kwenye shinikizo nzito. Inalaumiwa na wananchi na huku inalaaniwa na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza dola.

Tume inajua kitambulisho kinatishia watu wengi kukosa kuandikishwa. Haina ufumbuzi kwa sababu Mwinyichande anasema, “hatuhusiki nacho.” Lakini bado inarudi vituoni kuandikisha wapiga kura na kuendelea na msimamo wake uleule kuwa asiyokuwa na kitambulisho hataandikishwa!

Taarifa kutoka kisiwani Pemba , tena kwa wananchi siyo wanasiasa, zinasema utoaji wa kitambulisho unadhalilisha. Masheha, viongozi wa ngazi ya chini kabisa kiserikali, hawatoi fomu kulingana na anayefika kwao kuhitajia kitambulisho.

Inaelezwa kwamba kati ya watu 300 wanaofika ofisini, wanaosajiliwa na kupigwa picha hawafiki 100.

Ni dhahiri mamia kwa mamia ya wananchi – zaidi vijana waliofikia umri wa miaka 18 – hawajapata kitambulisho. Hawataandikishwa. Sasa? Hawataingia kwenye daftari. Halafu? Hawatapiga kura muda ukifika.

Kitambulisho, kilichoanza kutolewa rasmi tarehe 1 Agosti 2005, baada ya sheria iliyokianzisha kusainiwa na Rais wa Zanzibar, kinatajwa katika Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 11 ya mwaka 1984 kama sharti la mtu kuandikishwa kuwa mpigakura.

Kifungu hicho kimejumuishwa katika sheria ya uchaguzi kwa lazima. Ni kifungu kinachopingana na Katiba ya inayotoa haki kwa kila Mzanzibari kushiriki uchaguzi, kwa kufuata masharti ya kuwa na kithibitisho cha umri (cheti cha kuzaliwa); uraia (pasipoti); na shahada ya kupigia kura - ile ambayo mtu alitumia kushiriki uchaguzi uliopita.

Wajumbe wa Chama cha Wananchi (CUF), walikipinga wakati wa kupitisha kwa kutoka ukumbini. Hawa walijua kitakachoendelea baada ya sheria kupitishwa.

Serikali haitaki kutenganisha kitambulisho na uchaguzi. Kwa hakika, mtandao wa kuhifadhia kumbukumbu za Wazanzibari wakaazi na wapigakura sasa ni mmoja.

Anatokea Hamza Hassan Juma, waziri wa SMZ anazungumza mfano wa Mohamed El Sahaf, Waziri wa Habari katika serikali ya Saddam Hussein wakati Marekani na rafiki zake walipoingia kijeshi nchini Irak, kusema sana hata ule unaoweza kuitwa “uongo”, anasema:

Hamza anasema, “Kitambulisho kitaendelea kutumika kama kigezo cha mtu kuandikishwa.” Anasema kitambulisho kilianzishwa kwa Muafaka wa CCM na CUF uliolenga kuondoa malalamiko ya kila baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar .

Hamza hata baada ya tume kusitisha uandikishaji kwa vurugu zilizofanywa na wananchi wanaodai kitambulisho kinatolewa kwa misingi ya itikadi ya kisiasa, kwamba asiyekuwa CCM ni haramu kupewa, anaendelea kukitetea.

Hamza, baada ya kusikia Tume itarudi kuandikisha Jumamosi, anasema, “Serikali itaimarisha ulinzi ili zoezi la uandikishaji lifanyike kwa amani.”

Yeye na viongozi wenzake katika SMZ wanakiri ni haki ya kila Mzanzibar mwenye sifa. Lakini kwa ile amri ya ndani, wanazuia “wasiokuwa wanaCCM kupawa.”

Anasema, “Wananchi wa Pemba wasishangae kuona zana za kijeshi mitaani… tunaongeza ulinzi ili uandikishaji uende salama.”

Kama alivyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Suleiman Nyanga kwenye baraza, Mkurugenzi wa Idara inayotoa kitambulisho hicho, Mohamed Juma Ame, anasisitiza wenye haki wamepata kitambulisho na kwamba tayari vitambulisho 503,589 vimetolewa kufikia mwezi uliopita.

Iweje SMZ ilalamike kwa hilo na iseme amani na utulivu havina tatizo Pemba , lakini iongeze zana za kijeshi na askari kwenye kambi? SMZ imeshikwa pabaya.

Bado watu wanalalamika hawapati kitambulisho. Mazingira yaliopo Pemba yanatisha. Vijana wengi wanashitakiwa kwa madai ya kughushi nyaraka za kupatia kitambulisho.

Zipo taarifa kuwa masheha wanapewa fomu zilizorudufiwa na kuwapa wananchi wanaoomba vitambulisho. Ni fomu hizi zinazoandaliwa na Idara ya Vitambulisho zinazowatia makosani. Wanakamatwa na kushitakiwa.

Mohamed anasema fomu za ofisi yake hazitolewi mkononi bali muombaji akifika ofisini, mhusika anatoa fomu na kuijaza kutokana na majibu ya maswali yake. Mwisho, hutakiwa kurudi siku nyingine kuchukua kitambulisho.

Nani mkweli? Kinachoonekana ni kwamba kitambulisho hakitolewi kwa haki; na kwa kuwa kuna vitisho dhidi ya wananchi wanaotaka kitambulisho; wengi wataachwa.

Kwa namna Wazanzibari wanavyoijua thamani ya kura, hakuna atakayekubali kukosa kuandikishwa. Watu watachukia. Watasema “hapana.”

Hapo uandikishaji utasimama tena au utaendelea kwa mabavu, huku watu wakiswagwa kwa vifaru na bunduki. Halafu SMZ waseme Marekani ilikurupuka. Ni jasiri tu anayetaka kwenda Pemba sasa.

Lakini Mohamed amenilalamikia. Eti nimemkosea kusema ametishia kukamata na kushitaki viongozi wa CUF wakati yeye si mamlaka ya kukamata. Angalau anakiri ametishia kumshitaki Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kwa alichodai amesema uongo. Namuomba radhi nikijua Polisi ndio wakamataji na wapelelezi, ila tuhuma itakuwa ameziwasilisha.

Akasema majuzi alifuatana na balozi wa Marekani na Norway na kuwafunulia “kila kitu” kuhusu vitambulisho, na “wameridhika.”

Bado Marekani wanasisitiza Pemba kuna hatari ya usalama na hawabadiliki. Watu hawapati vitambulisho na Tume inayolaumiwa na wakubwa kwa “kuwavumilia wapinzani” inarudi kuandikisha. Muda utathibitisha nani mkweli.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: