Nipate wapi moyo wa Kikwete niepuke presha?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

YUPO mzee mmoja kijijini kwetu alikuwa hasikii kabisa malalamiko yaliyokuwa yanatolewa dhidi ya mwanaye ambaye alikuwa kibaka mzoefu wa kijiji. Alikuwa mzee wa kushangaza kidogo. Ni kana kwamba Mungu alikuwa amemjalia kifua kipana cha kuhimili malalamiko kwa njia ya ajabu kabisa. Kutokujali.

Hali hiyo aliichukulia kama njia ya kukabiliana na kila lalamiko dhidi ya mwanaye. Siku isiyokuwa na jina ilifika; wakafika vijana nyumbani kwake na kumpa taarifa kwamba maiti ya kijana wake imekutwa kwenye mtaro wa maji. Baba wa watu alipiga kelele lakini hazikuwa na maana tena, kwani kijana wake alikuwa maiti.

Laiti angelijali zile kelele za awali dhidi ya mwanaye walau kwa kuchukua hatua ya kumkanya basi maisha ya mwanaye yangeliweza kusalimika. Hakufanya hivyo, na alichovuna ni mauti ya mwanaye.

Kwa muda sasa nimekuwa nafuatilia utendaji wa baadhi ya wasaidizi wa Rais Jakaya Kikwete; zipo kelele zimepalizwa kwa kiasi cha kutosha juu ya uwezo wao mdogo wa kutenda, juu ya udhaifu wao katika kuhimili changamoto katika wizara zao; zimepalizwa sauti kwa kila staili, lakini Rais wetu amekuwa na ujasiri unaofanana na yule mzee wa kijijini kwetu, hajigusi. Matokeo yake kila kitu sasa kinakwenda hali jojo.

Kati ya Januari na Februari mwaka huu kulikuwa na mgomo wa madaktari uliodumu kwa takriban mwezi mmoja, watu wamelalamika kuhusu uwezo wa Waziri Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya. Wametajwa kwa majina kuwa ni kati ya vikwazo vya kutatuliwa kwa changamoto za sekta ya afya nchini.

Madaktari walifika mbali zaidi wakati wa mgomo wao na kusema wazi, pamoja na matatizo yote ya kiuchumi yanayokabili nchi, viongozi hao wakuu wa wizara ni tatizo. Ni tatizo kwa sababu wamevaa miwani ya mbao, hawaoni; hawasikii kwa sababu wamejaza nta kwenye masikio yao, matokeo yake huduma za kitabibu katika hospitali kuu za umma zinazidi kwenda mrama na wao wakiangalia tu. Bosi wao naye kama yule mzee wa kijijini kwangu yuko kimya!

Kuna suala la elimu. Ukiitazama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, unaweza kupagawa. Hakuna kinachokwenda mbele, si kuimarika kwa sekta ya elimu, si kushughulikiwa kwa matatizo ya walimu kwa wakati, na hata wale wanaopata ajira mpya hali imekuwa ya kizungumkuti mno kupata malipo yao.

Mwaka baada ya mwaka ubora wa elimu unaporomoka. Mwaka 2010 kama ulivyokuwa mwaka 2011 kiwango cha wanafunzi waliofaulu kwa maana ya kuweza kusonga mbele katika mfumo wa elimu wa Tanzania ni asilimia 10 hivi – hawa ni wanafunzi waliofaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu.

Kwa bahati mbaya tulivyozoea kuishi kama mazuzu, tunaona ni kawaida tu kuwa na hali hiyo. Wasimamizi wa elimu wanakula raha zao; nani awajibike? Kiongozi wao mkuu naye wala hastushwi na kekele zinazopigwa. Kimya!

Hali ni hiyo hiyo katika uchumi. Hakika Waziri Mustafa Mkulo hajui anafanya nini pale Hazina. Hali ya uchumi inazidi kuwa tete, siku baada ya siku, thamani ya sarafu ya Tanzania inazidi kuporomoka, mfumuko wa bei hauelezeki. Mzee Mkulo yupo, katulia wana hana wasiwasi.

Ni hali hiyo hiyo kwa mkuu wa nchi, wala hatikisiki kwa kelele za wananchi, wanaharakati, vyombo vya habari juu ya njaa inayowakabilia wananchi, ugumu wa maisha. Ametulia.

Ni jambo la kushangaza wakati matatizo kama haya yanayoielemea nchi Rais anapata muda, nguvu na ujasiri wa kusafiri nje ya nchi kuhudhuria mikutano ambayo kwa kweli ukiipima sana manufaa yake ni kidogo sana kwa taifa, kwani ni mikutano ambayo hata kama angewakilishwa na wasaidizi wake hakika manufaa yake yangekuwa ni hayo hayo.

Katika mazingira kama haya mtu anapoitazama serikali yetu inavyoendesha nchi anafikia hitimisho moja kuwa, tumejaliwa rais mwenye kifua, jasiri asiyesumbuliwa na kelele zozote, na kwa kufanya hivyo ameweza kupuuza kila aina ya wito unaotolewa dhidi ya udhaifu wa wasaidizi wake. Amekuwa na kifua cha kuhimili kelele.

Kwa bahati mbaya, wakati amefanikiwa kuhimili kelele hizi, bila kuumiza kichwa, bila kumwajibisha yeyote, bila kufanya mabadiliko yoyote, na kwa maana hiyo bila kutenda kazi kama ambavyo wangependa wapenda mabadiliko, ameacha kila kitu kama kilivyo.

Kwa yule mzee wa kijijini kwangu ukubwa wa kifua chake katika kuhimili kelele dhidi ya tabia chafu ya mwanaye ilimletea matokeo mabaya kuliko ambavyo angeliweza kuwaza tangu awali; maafa.

Kwa Rais Kikwete amevumilia kila kelele na kufumba macho kana kwamba haoni, lakini akikubali kuona serikali yake ikiendelea kuwa madarakani kama moja ya serikali dhaifu kabisa kuwahi kuongoza nchi hii.

Wapo wanaoweza kujenga hoja kwamba serikali ya awamu ya nne si dhaifu hasa wanapotazama “vikesi” vya rushwa vilivyofunguliwa dhidi ya watu wachache kwa njia ya kuchagua na si kwa mfumo wa sheria kuchukua mkondo wake; lakini pia wanaweza kusadiki kuwa kwa kuwa kuna mchakato wa katiba mpya basi hii ni serikali nzuri.

Ni vizuri wenye mawazo haya wakaitazama nchi hii kiuchumi kwanza, wajiulize wakati awamu ya tatu inaondoka madarakani sarafu yetu dhidi ya sarafu ya Marekani ilikuwa imesimamia wapi. Je, mfumuko wa bei ulikuwa wapi; je, uwezo wa akiba ya fedha ya kigeni ulikuwa unamudu kuagiza huduma na bidhaa kutoka nje kwa muda gani?

Lakini la muhimu zaidi, ni lazima tuwapime watumishi wa umma na uwajibikaji wao kama kweli unafikia vigezo na matarajio ya wananchi kwa sasa. Kama chini ya awamu ya tatu tulikuwa na ubavu wa kujenga barabara za lami kwa vyanzo vya fedha za ndani bila kutembeza bakuli kwa wafadhili; na kama chini ya awamu ya tatu makusanyo mengi ya kodi yalionekana yalikokwenda, inatakuwa ni kipimo kizuri kujiuliza leo hii kwamba pamoja na ukweli kwamba sasa kodi inakunywa zaidi ingawa ni kwa kuwabana walipaji wale wale na si kupanua wigo wa walipa kodi, inakokwenda ni wapi kama walimu wanadai malimbikizo ya mishahara, madaktari wako kwenye mgomo na hata wabunge wameinunia serikali yao kwa kuwakatalia nyongeza ya posho?

Unapofikia hitimisho kama hilo, hakika unakuwa umemweleza kwa uwazi kabisa Rais wetu kuwa ni mtu ambaye hawezi kuugua ugonjwa wa moyo kutokana na shinikizo lolote kama yule mzee wa kijijini kwangu, lakini ataiacha nchi na maangamio itakapowadia Oktoba 2015.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: