Njama kumng'oa Kikwete zafichuka


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Mwanae Ridhiwani ashiriki njama
Watuhumiwa ufisadi wajipanga
Rais Jakaya Kikwete

KUNDI la watuhumiwa wa ufisadi limejipanga kumng’oa Rais Jakaya Kikwete ili asigombee urais mwaka 2010, MwanaHALISI limegundua.

Taarifa zinasema tayari baadhi ya marafiki wa Kikwete wameunda kile kinachoitwa, “One-term President (OP),” ikimaanisha “Kikwete rais wa kipindi kimoja.”

Suala la Kikwete kuwa rais wa kipindi kimoja lilikuwa mkakati wa baadhi ya washirika wa Kikwete katika kundi la mtandao wakati wa kampeni za urais za 2005.

Taarifa zinawataja Edward Lowassa na Rostam Aziz kuwa viongozi waandamizi wa mtandao waliokuwa wanaendesha mkakati huo. Aliyekuwa anaandaliwa kumwondoa Kikwete alikuwa Edward Lowassa.

Hivi karibuni mkakati wa kushika chama ndiyo ulifanikisha Jacob Zuma kumuondoa Thabo Mbeki kwenye urais nchini Afrika Kusini.

Zuma aliweka mkakati wa kushika chama mara baada ya kuondolewa katika nafasi ya makamu wa rais kwa kashfa za ufisadi na rushwa.

Mara baada ya kuondolewa katika nafasi yake, Zuma alijipanga kushika uongozi wa chama cha ANC ambapo alifanikiwa kumshinda Mbeki na baadaye kumfukuza urais.

Katika CCM, taarifa zinasema, kundi lililopanga kugombea urais mwaka 2010, limekuwa likipigania kuwepo “watu wake” katika nafasi za juu za uongozi katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC).

Baadhi ya wanaotajwa kuandaliwa ni wenyeviti wa mikoa: Deo Sanga (Jaa People- Iringa), Ernest Mabina (Mwanza) na Khamis Mgeja (Shinyanga).

Wengine ni John Guninita (Dar es Salaam), Nawab Mulla (Mbeya), Onesmo Ngole (Arusha), William Kusila (Dodoma) na Hypolitus Matete (Sumbawanga).

Haijafahamika kwa sasa nani ameandaliwa kumrithi Kikwete baada ya Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu kutokana na kashifa ya Richmond.

Hata hivyo, mpango wa kumg’oa Kikwete bado uko palapale, ingawa waaandaji wanaweza kubadilisha mbinu na mkakati ikiwamo hata kushirikisha watu wengine na kwa malengo tofauti.

Tayari wajumbe wa kundi hilo wamekutana katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Arusha kuweka mkakati wa kutekeleza azma hiyo. Wajumbe kadhaa wakiwamo baadhi ya mawaziri na wajumbe wa NEC walihudhuria mikutano hiyo.

Taarifa za kuaminika zinasema kikao cha karibuni kimefanyika siku chache baada ya kumalizika kwa kikao cha NEC mwezi uliopita.

Inaelezwa kwamba kwa sasa mkakati wa kundi hilo ni kusimika viongozi katika uchaguzi unaoendelea ndani ya jumuiya za CCM.

Uchaguzi huo unaendelea nchi mzima na unatarajiwa kufikia kilele chake mwishoni mwa mwaka huu.

Gazeti hili liliwasiliana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba na kumueleza kuwa kuna kundi linotaka kumdhoofisha Kikwete kwa mtindo wa Mbeki wa Afrika ya kusini na kwamba jina lake limetajwa.

Makamba aling’aka, “Sijui kitu. Nasema sijui kitu.” Alipong’ang’anizwa kwamba itakuwaje hajui wakati yeye ni katibu mkuu wa chama, Makamba alijibu kwa sauti kali, “Nakwambia sijui kitu.”

Mjumbe mmoja wa NEC ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini alipotakiwa maoni yake na gazeti hili alisema, “Inawezekana hata yeye (Makamba) haufahamu kwa undani mpango huu, lakini kwa hatua yake ya kutetea watuhumiwa, hasa Edward Lowassa na Andrew Chenge, anaonyesha anaufahamu.”

Taarifa zinasema naye mtoto wa Kikwete, Ridhiwani Kikwete anahusika kumdhoofisha baba yake. Zinasema Ridhiwani anatumiwa na baadhi ya wajumbe wa kundi hilo kufanikisha mpango huo.

MwanaHALISI limeshindwa kuthibitisha mara moja kama Ridhiwani anaufahamu kwa undani mpango wa kumuondoa baba yake ikulu, ijapokuwa kuna ushahidi wa kutosha kwamba anatumiwa.

Juhudi za kumtafuta Ridhiwani ziliambulia taarifa kwamba aliondoka Jumamosi kwenda nchi za nje.

Haikujulikana mara moja amekwenda nchi gani.

Katika kufanikisha mkakati huo, Ridhiwani amepewa kazi ya kusimika viongozi wa jumuiya za chama hasa UV-CCM.

Mgombea anayetajwa kusimikwa na Ridhiwani ni Beno Malisa ambapo katika kuhakikisha anashinda, Ridhiwani anahaha kusimika viongozi katika ngazi za chini.

“Wanataka kuhakikisha kwamba wenyeviti wote watatu (UWT, UV-CCM na Wazazi) wanakuwa wafuasi wao ili kurahisisha utekezaji wa mpango huo,” anasema kada mmoja wa CCM ambaye anaufahamu mpango huo.

Alisema, “Hii itawasaidia kupata wajumbe wengi wa CC, ili muda wa kuasi ukifika, iwe rahisi kutekeleza ajenda ya kumuondoa Kikwete na kumwacha bila wafuasi.”

“Hawa jamaa wana mkakati mkubwa bwana. Wameamua kumpeleka Ridhiwani mbele ili isionekane kwamba Beno atakuja kutumika vibaya dhidi ya Kikwete huko mbele,” alisema mjumbe mtoa taarifa.

Beno Malisa anatajwa kuwa ni mfuasi mkubwa wa Lowassa akihusishwa na mkataba wa kinyonyaji wa kitegauchumi cha UV-CCM.

Lowassa ni mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UV-CCM ambaye alipitisha mkataba na mwekezaji bila kushirikisha wenzake katika chama, huku Malisa akitajwa kuwa ni mshirika mkubwa wa mradi huo.

Madai makuu kutoka kambi ya Lowassa katika kundi hilo ni kwamba Kikwete hakufanya jitihada za kumtetea Lowassa katika sakata la Richmond.

“Wanaamini kwamba Kikwete alikuwa na uwezo wa kumuokoa Lowassa, lakini hakumtetea. Sasa tutamuonyesha kama tunaweza kumsulubu,” taarifa zinaeleza.

Katika sakata la Richmond, MwanaHALISI liliripoti kwamba Kikwete aliamua kumtosa Lowassa akisema “waachwe wabunge wenyewe waamue.”

Tayari orodha ndefu ya wajumbe wa NEC  imeandaliwa ambapo muda ukifika itatumika kufanikisha lengo hilo.

Guninita anatajwa kwamba mjenga mkakati akitumiwa na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM.

Ni Guninita aliyemtetea rais mstaafu, Benjamín Mkapa na kumkemea mbunge wa Vunjo (CCM) Aloyce Kimaro aliyedai kuwa  Mkapa alifanya kazi binafsi akiwa ikulu na hivyo kukiuka maadili.

Guninita alitoa utetezi katika kikao cha NEC na wabunge mjini Dodoma. 

Mwingine anayetajwa ni mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba ambaye alimmwagia sifa Rostam Aziz kwa kile alichoita “kunusuru” kampeni za uchaguzi mdogo wa Kiteto.

Rostam alifanikisha upatikanaji wa helikopta ili kupambana na Chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema) kilichoasisi mtindo wa kutumia helikopta katika kampeni za uchaguzi.

Aidha, Komba anatuhumiwa kutafuna mamilioni ya shilingi za CCM, kughushi nyaraka na kubadilisha magari ya chama hicho kuwa yake binafasi. Lakini hajachukuliwa hatua kutokana na kile kinachoitwa, “kutetewa na mafisadi.”

Naye mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba aliyekuwa mtetezi mkubwa wa Lowassa naye anatajwa kutumika katika kufanikisha mpango huo.

Serukamba alirejea kilio chake kuwa Lowassa “hakupewa nafasi ya kujitetea na kwamba bunge lilimhukumu bila kupitisha hoja kwenye chama.” Alisema katika uchaguzi mkuu ujao, wananchi hawatauliza juu ya Richmond, bali utekelezaji wa sera za CCM.

Wajumbe wengine wanaotajwa ni mawaziri wa zamani Andrew Chenge na Nazir Karamagi. Wengine ni Lawrence Masha (Mambo ya Ndani ya Nchi), Dk. Emannuel Nchimbi (Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Adam Malima (Nishati na Madini).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: