Njelu Edward Kasaka: Sasa natamani tena ubunge


Steve Mwasubila's picture

Na Steve Mwasubila - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

NJELU Kasaka anautaka ubunge wa jimbo la Lupa, mkoani Mbeya ambalo alishikilia kwa miaka 15 mfululizo kabla ya kung’olewa mwaka 2005.

Katika mahojiano aliyofanya wiki iliyopita na MwanaHALISI, Kasaka anasema, “Mimi ndiye mwana CCM pekee nitakayeshindana na mbunge wa sasa.”

Kujitokeza kwake kumeanza kumjengea uhasama na mbunge anayemaliza miaka mitano Oktoba mwaka huu, Victor Mwambalaswa.

Ni Mwambalaswa huyo anayetuhumu anaowaita “wapinzani wangu” kwamba wamemwaga jimboni kiasi cha Sh. 60 milioni ili kumng’oa asirudi bungeni.

Mwambalaswa alishinda ubunge wa Lupa mwaka 2005 baada ya kufanikiwa kumtupa Kasaka katika kura za maoni.

Kasaka aliamua kuhamia Chama cha Wananchi (CUF) na kugombea ubunge hapo. Hata hivyo, mizengwe iliyowekwa na CCM ilimkwamisha kwani chama hicho kilimwekea pingamizi kuwa angali ni kada wao.

Baada ya kung’ang’ana CUF, alishindwa uzalendo na kulazimika kurudi CCM. Sasa anakuja na nguvu mpya kisiasa akilenga kurudi bungeni.

Kasaka anataka kwenda kujichanganya tena na baadhi ya wanasiasa aliokuwa nao pamoja katika kundi la G-55 walioongoza kampeni ya kuitaka jamhuri ya Tanganyika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Bado mapema anakanusha tuhuma zilizotolewa 28 Desemba mwaka jana kuwa anahusika na fedha zinazodaiwa kumwaga jimboni ili kumtoa Mwambalaswa.

Anakiri kwamba anafahamiana vizuri na Edward Lowassa, ambaye anatajwa kuwa amefanikisha kumwagwa kwa fedha jimboni Lupa, lakini Kasaka anasema tuhuma hizo ni za kupuuzwa.

Kwanini zipuuzwe? “Tangu kipindi cha utumishi wangu kama mbunge nimekuwa na uhusiano mzuri na kila mbunge na hata ukiwauliza wabunge niliofanya kazi nao watakuthibitishia hili. Mahusiano yangu na Lowasa ni ya kawaida kama kwa wabunge wengine,” anasema Kasaka.

Kasaka anajinasibu kwamba kutaka kurejea kwake jimboni kutokana na kuombwa na wananchi wa Lupa kwa kuwa wanatambua mchango alioutoa alipokuwa mbunge wao.

Ameweka malengo akipata ubunge. Mojawapo ni kuinua kilimo jimboni kupitia kaulimbiu ya Kilimo Kwanza na msisitizo mkubwa anasema itakuwa ni kilimo cha tumbaku ambalo ni zao kuu la biashara katika wilaya ya Chunya.

Kadhalika, anasema ataweka mazingira mazuri ya kuendeleza zao la ufuta na alizeti ambayo ni mazao mengine ya biashara yanayotegemewa sana na wananchi wa Chunya.

Kuhusu nini hasa kilichomsukuma kutaka kuwania tena ubunge, Kasaka anasema, “Mchango wangu wa mawazo na kiutendaji kwa wananchi wa Lupa, bado unahitajika pia wameonyesha nia ya kunihitaji hivyo nimeona si vyema kuwaangusha.”

Kasaka anajivunia uwezo wake kiuongozi akisema staili yake ya uongozi bado ingali tunu kwa wananchi wa jimbo hilo.

Anasema, “watu wananikumbuka kwa msimamo wangu imara katika kujadili masuala mbalimbali ndani na nje ya bunge.”

Katika moja ya miradi mikubwa ya maendeleo ambayo sasa inaendelea kutekelezwa wilayani Chunya, anasema ni ujenzi wa barabara ya Mbeya-Chunya kwa kiwango cha lami.

Kasaka anasema ujenzi huo ulioanza mwaka 2007, aliutilia hima na anasema alitoa matamshi mazito bungeni katika jitihada zake za kuishinikiza serikali wakati wa mijadala ya makadirio ya matumizi ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2005/2006.

Kasaka aliyewahi kuwa naibu waziri wa kilimo na ushirika katika serikali ya awamu ya pili chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, alikuwa mmoja wa wanasiasa mahiri waliokuwa na mvuto mkubwa kwa umma.

Yeye aliingia katika siasa tangu enzi za Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) mwaka 1973 na akawa miongoni mwa waanzilishi wa CCM mwaka 1977.

Aliwahi kutumikia chama hicho kama Katibu Mwenezi Wilaya ya Chunya, Mjumbe wa Kamati ya CCM Mkoa kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 1997, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kasaka aliwahi kuwa mkuu wa mkoa Iringa kipindi cha mwaka 1998 hadi 1999 na baadaye kuteuliwa kushika wadhifa huohuo kwa mkoa wa Tabora waka 2000.

Kuwa kwake mtaalamu wa masuala ya kilimo kumempatia hadhi ya kuingia katika bodi mbalimbali. Alikuwa mjumbe wa Bodi ya Magavana wa Shirika la Maendeleo ya Chakula na Kilimo (IFAD) lenye makao makuu yake Rome, Italia 1995/1998.

Alikuwa mjumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) 1993/1995; Mwenyekiti wa Hoteli ya Tembo Resort iliyoko Songwe, Mbeya 1993/1995; Mjumbe Bodi ya Wakurugenzi ya Mbeya Cement 1993/1995; Mjumbe Bodi ya Wakurugenzi ya Mbeya Textile 1994/1995.

Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge 1991/1994; Mjumbe wa Bodi ya Kiwanda cha IMAC Iringa 1988/1990.

HISTORIA NA ELIMU

Njelu Mulugala Kasaka alizaliwa 2 Februari 1942, Chunya mkoani Mbeya.

1974 alihitimu Shahada ya Uchumi (Viwandani) – Chuo Kikuu Dar es Salaam; 1978: Stashahada ya Uchumi – Chuo Kikuu Colorado, Marekani; 1980: Shahada ya Uzamili ya Uchumi (Kilimo) – Chuo Kikuu Kentucky, Marekani.

MAFUNZO MBALIMBALI

Utayarishaji Miradi – Chuo cha Usimamizi wa Fedha Dsm (Juni 1974); Ufadhili wa viwanda vidogo – Chuo Kikuu cha Hyderabad (SIETI), India (Okt/Nov 1974); Mbinu za Maendeleo ya Kilimo – Chuo Kikuu cha Taifa Washington, Marekani (Ago-Sept 1978).

1979 Mei-Juni: Ufadhili na Uongozi wa miradi ya wakulima wadogo – Makao Makuu ya Wizara ya Kilimo, Washington, Marekani; Okt-Des1986: Huduma za Benki katika Biashara – Benki ya Ushirika Kenya (KCoB)

UONGOZI

1990: Meneja Mkuu CRDB Makao Makuu Dsm; Meneja CRDB Mkoa Dsm – 1981/1984; Meneja CRDB Mtwara – 1976/1980; Meneja Mradi CRDB Kilimanjaro 1974/1975.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)