Njia ya Chiluba, Muluzi bado yamsubiri Mkapa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 04 August 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

KUPAMBANA katika kufunika kashfa za ufisadi au kujaribu kutosa wale ambao waweza kuonekana kondoo wa kafara kumeshamiri kipindi cha utawala wa awamu ya nne.

Serikali ya rais Jakaya Kikwete imeshadhihiri ni majeruhi wa kashfa hizi kwa sababu moja tu: kwa makusudi iliamuliwa tangu awali kuwepo watakaolindwa kwa nguvu zote hata wafisidi nchi namna gani.

Bila kutaja kesi zilizo mahakamani kwa kuchelea kuingilia uhuru wa mahakama, yatosha tu kusema utaratibu wa kushughulikia kashfa kwa nia tofauti – ya kusafishana na nyingine ya kutosana na kuangamizana – kamwe hautaisaidia serikali.

Ukitafakari kwamba serikali kwa miaka mitatu na ushei sasa imetumia kila aina ya nguvu na mbinu kufunika baadhi ya watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi kama vile wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, huku ikijitahidi kuharakisha wengine kufikishwa mahakamani, unashindwa kujua nia ya vita dhidi ya ufisadi ni nini hasa.

Lakini ukiweka kando habari za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), jaribu kufikiria kinachoendelea sasa kuhusu mgodi wa Kiwira. Je, nia ni kurekebisha kasoro zilizotokea katika uuzaji mgodi huu mali ya taifa au ni mbinu nyingine ya kumsafisha rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, dhidi ya tuhuma za ufisadi?

Vita na harakati za serikali katika kusafisha uoza ndani yake inakuwa ngumu si kwa sababu ushahidi haupo, ila ni kwa sababu tu ya undumilakuwili upande wa serikali.

Wakati kila Mtanzania akijua kwa hakika kwamba makundi ndani ya chama tawala yamekifikisha chama pagumu, bado serikali kwa kutofahamu nia ya kulinda kundi hili na kuangamiza lile, imeendeleza sera za kubaguana katika kushughulikia ufisadi.

Kwa mfano, inakuwa vigumu mno wananchi wengi kuamini vita dhidi ya ufisadi ni mkakati makini wakati kampuni iliyochukua karibu asilimia 30 ya fedha za EPA, haijaguswa.

Hatari kubwa zaidi ni pale unapoona mkuu wa chombo mahsusi cha kusimamia mkondo wa sheria kutekelezwa kama Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), analalama tu badala ya kuchukua hatua kubana wenye Kagoda. Eti anaogopa serikali itaishia tu kukamata waliosajili kampuni hii huku ikiwakosa wale waliowatuma.

Inawezekana vipi kwa mfano chama kinachopambana na ufisadi na serikali inayotumia vyombo vyake kuchunguza mafisadi ili kuwashitaki na kwa wakati, viongozi wake wawe wanakaa meza moja na watuhumiwa wakuu tena wakiwatazama kama malaika wasio na hata chembe ya tuhuma?

Wapi umesikia ujasiri wa namna hii? Lakini ndani ya serikali hiyohiyo watu wenye tuhuma za kuungaunga kwa mshumaa wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ambazo hata ofisi ya DPP imeyumba kuzitolea ushahidi.

Tarehe 18 Machi, mwaka huu, katika safu hii niliandika uchambuzi uliokuwa na kichwa cha habari: "Muluzi aonja korti, Mkapa presha juu."

Uchambuzi huo ulitokana na kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa rais wa zamani wa Malawi, Bakili Muluzi, ili kujibu mashitaka 80 ya rushwa na kujipatia mali ya umma kinyume cha taratibu.

Muluzi, aliyeingia madarakani kama mfanyabiashara, muda wake wa kukaa madarakani ulipita kwa kasi, lakini alijaribu kubadili katiba ili agombee muhula wa tatu, alikwama.

Baada ya kukwama kwa sababu alikuwa na siri moyoni, Muluzi alitafuta njia ya kujinusuru, alimtafuta Bingu wa Mutharika kwa njia ileile ya Frederick Chiluba wa Zambia ya kumtafuta Levy Mwanawasa, ili amlinde. Siri yao ilikuwa ni ya kufunika kombe mwanaharamu apite.

Kwa bahati nzuri, marais hawa majirani zetu, Muluzi na Chiluba, baada ya juhudi zao za kubadili katiba kukwama na kudhani kwamba eti salama yao itapatikana kwa kumtafuta mrithi wa kuwalinda, walikwama na wameendelea hawajakwamuka.

Kwa hiyo fomula ya Chiluba ambayo Muluzi aliikopi na kuitumia kavukavu, imekataa kufanya kazi; ila kwa bahati nzuri, kwetu Tanzania bado marais wastaafu wanaendelea kufurahia maisha yao ya kupumzika baada ya kutumikia umma, lakini kila mmoja kwa hisia tofauti moyoni mwake.

Nilipata kusema wapo waandishi mahiri, ninaowaheshimu ambao walisema wazi wanamuomba radhi rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi. Kwa nini Mwinyi aombwe radhi?

Ni rais aliyezuliwa mengi mchana kweupe; alikejeliwa hata na watu wasioweza kupenga makamasi kwa kuwa tu aliruhusu uhuru wa kujieleza, alifungua minyororo ya uchumi, alifungua haki ya watu kujieleza kisiasa. Mwinyi aligeuzwa gunia ya kujifunzia kurusha ngumi kama ni kuazima lugha ya mabondia!

Wahenga walituasa kwamba ng'ombe hutambua thamani ya mkia wake siku ukikatika na nzi wanapoanza kumzonga. Hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya Mzee Mwinyi kuondoka madarakani na watu kuonja utawala wa mrithi wake.

Rais mbabe mwenye ubavu wa kufokea hata waliompigia kura, jasiri wa kutukana wananchi, mwenye kujiona mwelewa wa kila kitu hata utaalamu wa kugundua bomu la nyukilia.

Benjamin, mwanasiasa aliyeokwa ili umma uamini yu mtu safi, muadilifu na mbebaji mzuri wa dhamana ya uongozi kwa moyo wake wote. Ni kiongozi aliyejitoa katika muonekano wa ngozi ya kondoo, lakini baada ya kushika madaraka akaivua na kuonekana mbwa mwitu asilia.

Sasa baada ya kuacha madaraka, si tu hana tena ubavu wa kufoka, kutisha na kunyima magazeti pumzi ya matangazo; bali pia anakabiliwa na tuhuma kama za akina Muluzi na Chiluba.

Tawala zao zinashabihiana. Kila mmoja alijihusisha mno na harakati za kujinufaisha na familia yake. Mkapa na makampuni, Mkapa na Kiwira; Mkapa na ununuzi wa nyumba za serikali, Mkapa na ununuzi wa nyumba bila dhamana- urais ukiwa dhamana, Mkapa hapa Mkapa kule.

Kila uchao Watanzania wameelezwa mawaa ya Mr Clean wao! Hadi sasa Mkapa ana nafuu moja, kwamba katika vita dhidi ya ufisadi ameangukia kundi lile la kulindwa, kusafishwa na kufunika kombe mwanaharamu apite. Bado nguvu za dola zinatumika asifikie hatua ya Chiluba au Muluzi – ya kushitakiwa – bado anapumua kwa rehema ya makundi ya CCM na ndani ya serikali.

Ni kwa muda gani Mkapa atabaki salama; hakuna ajuae. Ila itoshe tu kusema atabaki salama kadri hali hii ya sasa; ya mvutano wa makundi ya kimaslahi ndani ya CCM, itabakia.

Ikitokea mizania kubadilika kwa vyovyote vile, au kwa sababu kundi moja limezidi kete jingine kwa kiwango kikubwa zaidi; bado Mkapa hatakwepa njia waliyopita Chiluba na Muluzi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: