Makamba kumkana Kikwete?


Andrew Bomani's picture

Na Andrew Bomani - Imechapwa 21 April 2010

Mtazamo
Yusuf Makamba

KATI ya mwaka 1988 na 2001, jina la John Joseph Kamotho lilipamba vichwa vya habari vya magazeti nchini Kenya. Alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha African National Union (KANU).

Katika kipindi hicho, KANU ndiyo chama kilichoshika hatamu za uongozi; kwa wananchi wengi wa Kenya, KANU ndicho kilikuwa “baba na ndiyo mama.”

Kamotho alikuwa na sifa nyingi. Moja, alikuwa msomi, lakini pili alitenda kama Kasuku akishambulia kila mkosoaji wa serikali, chama chake na Rais Daniel arap Moi.

Ni ukasuku huo, unaotajwa kuchangia kumwangamiza kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 1992 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vyingi nchini humo.

Pamoja na kuanguka huko katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la nyumbani kwao, bado Rais Daniel arap Moi alimteua Kamotho kuwa mbunge na akamtunuku uwaziri.

Hata hivyo, kilichoshangaza wengi na hata kuacha midomo wazi, ni pale Kamotho alipomgeuka Moi, siku chache kabla ya rais huyo kustaafu mwaka 2002.

Kamotho aliondoka ndani ya chama cha Moi na kushusha rundo la tuhuma, shutuma na lawama, kwamba mchakato wa kumpitisha Uhuru Kenyatta, kuwa mgombea urais kupitia KANU ambao yeye alishiriki kikamilifu kuusimamia, ulitawaliwa na mizengwe.

Hivi sasa, ni vigumu kumsikia Kamotho akitaja jema hata moja lililofanywa na utawala wa KANU.

Hapa nchini yupo Joseph Kamotho. Huyo si mwingine, bali ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba.

Makamba ameonyesha utiifu wa zaidi ya asilimia 100 kwa Rais Jakaya Kikwete. Anasema, “Kikwete ni mtaji wa CCM” na anashambulia kila anayemkosoa Kikwete kwa kuita “wehu.”

Makamba haishii hapo. Kama ilivyokuwa kwa Kamotho, anadhalilisha hata wazee wa chama chake – wanaomkosoa Kikwete na utawala wake – kwamba kauli wanazozitoa zinatokana na “wivu wa kushindwa na Kikwete” katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005.

Kama ilivyokuwa kwa Kamotho aliyekuwa ameumbwa na Moi, Makamba naye ameumbwa na Kikwete.

Kwanza, alimteua kuwa mbunge na kisha akampa ukatibu mkuu wa chama chake. Tangu alipopewa kazi hiyo, jukumu kubwa alilonalo, si kutetea chama kwa kusimamia maadili ya wanachama na viongozi, bali ni kumsifu na kushambulia wanaokosoa chama na serikali.

Inawezekana hiyo ndiyo kazi ambayo Makamba amekabidhiwa na Kikwete.

Hii ni kwa sababu, tayari Kikwete mwenyewe amenukuliwa akitaka viongozi waliostaafu kuacha kuzungumzia masuala ya kitaifa kwa madai kuwa walikuwa na wakati wao.

Marehemu Rashid Kawawa alitajwa na Kikwete kama mfano wa viongozi wastaafu walioheshimu viongozi waliopo madarakani.

Muda si mrefu, kwa hulka na mwenendo wa Makamba wananchi watarajie Kikwete kukanwa kama ilivyokuwa kwa Moi aliyekanwa na Kamotho.

Wakati wa Makamba kumkana Kikwete hauko mbali. Ni pale Edward Lowassa atakapotaka kutimiza ndoto yake ya miaka mingi ya kuwa rais wa Jamhuri.

Hii ni kwa sababu Makamba ni swahiba mkuu wa Lowassa. Ushahidi ni kwamba Makamba huyu ndiye aliyetengeneza mikakati au njama za kufukuzwa ndani ya CCM, Spika wa Bunge Samwel Sitta ili kumwokoa Lowassa katika kashfa ya kuipa kampuni ya Richmond zabuni ya kufua umeme wa dharura.

Si hivyo tu, ni Makamba aliyesafiri usiku wa manane kutoka Kiteto ambako alikuwa anapigia kampeni chama chake, hadi Dodoma kwa lengo la kumuokoa Lowassa asifukuzwe katika kiti chake.

Kwa hiyo Lowassa akitangaza nia yake itabidi Makamba apande farasi mmoja; Lowassa au Kikwete na katika mazingira ya uswahiba wake na Lowassa, jibu liko wazi.

Hapo ndipo Makamba atakapomkana Kikwete, hasa ikiwa Kikwete atasita kumwachia Lowassa utukufu kwa kile kinachoitwa, “Wosia wa Baba wa Taifa,” Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hilo likifika na lazima litafika, Makamba atatenda kama alivyotenda Yuda Isikariote aliyemkana Bwana Yesu; atamkana Kikwete na kumkumbatia Lowassa.

Hivyo basi, ni jukumu la kila Mtanzania kufanya bidii kwa kuiacha nchi mahali pazuri zaidi.

Ni vema viongozi wastaafu wanaoshambuliwa na Makamba kutorudi nyuma, badala yake waendelee kupaza sauti zao juu kuliokoa taifa na ombwe la uongozi lililojitokeza sasa.

Hili ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakaribia uchaguzi mkuu. Hatua yeyote ya kunyamazia maovu yanayotendwa na serikali, kunazidi kumfanya Makamba kuwa mbogo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: