North Mara 'walioua' wajute


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 July 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

VIONGOZI wa ngazi za chini wilayani Tarime wanalia. Kilio chao kinatokana na kile wanachoamini kutendewa: "Ukatili na unyama."

Mtuhumiwa wao mkuu ni waendeshaji wa mgodi wa dhahabu wa North Mara – kampuni ya Barrick Goldmine.

Sikiliza asemavyo Afisa Mtendaji Kata ya Nyakunguru katika risala aliyosoma Diwani wa hapo, Moyo Suleiman, kwa wabunge na wataalamu mbalimbali waliokwenda kufuatilia malalamiko ya wananchi:

"Idadi ya vifo vya wakazi wa Kata ya Kibasuka imefikia watu 43, ng'ombe ni 401, mbuzi 567, kondoo 183 na mbwa 207."

Nini chimbuko la maafa haya? Mgodi katika uzalishaji wake, unatoa kemikali ambayo ni sumu ambayo inatiririka na maji kutokea mgodini na kusambaa kwenye mto Tigithe ambao unategemewa na wananchi kwa matumizi ya uzalishaji na majumbani.

Taarifa za awali za malalamiko ya wananchi kukumbwa na maafa kutokana na kadhia hii, yalisukuma Spika wa Bunge, Samuel Sitta kutuma timu kabambe ya wabunge ili kutafuta msingi wa malalamiko ya wana Tarime.

Walikwenda wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Maliasili, Mazingira na Ardhi inayoongozwa na mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM), na wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini inayoongozwa na mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo (CCM).

Wabunge hao waliandamana na kikosi kikubwa cha wataalamu na wadau wa sekta tofauti kama afya, mazingira, maliasili na maji. Kwa jumla, taarifa zinasema kulikuwa na watu wapatao 100.

Sasa taarifa zimeenea kwamba walichosikiliza na kushuhudia ni mambo ya ajabu na mazito yanayohitaji kutazamwa kwa uzito unaostahili.

Nilimsikia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki akisema wamiliki wa mgodi walidanganya serikali kuhusiana na kinachotokea, baada ya wananchi kuanza kulalamika.

Siku kadhaa baada ya wabunge kujionea "mambo mazito" wilayani Tarime, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anasema: sakata la mambo yanayokabili mazingira ya Tarime kuhusiana na mgodi wa North Mara, ni zito na linahitaji kuchukuliwa kwa umakini mkubwa."

Waziri Ngeleja, bila ya shaka katika hali inayoonekana anachunga kete ili asije akaharibikiwa na kitumbua chake atakapowasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake karibuni, anasema:

"Baada ya Serikali kutuma wataalamu wapatao 100 kule Tarime, na Bunge nalo kutuma wajumbe wa kamati mbili za kudumu, mambo mazito yalibainika. Sasa taarifa ya hali halisi itatolewa haraka."

Kila mtu anachukulia kuwa hiyo ni "kauli thabiti." Okay; umma unasubiri ripoti ya kitaalamu. Ila mpaka sasa upo ukweli kwamba "mgodi wa North Mara umesababisha maafa kwa watu na mifugo, pamoja na mazingira."

Ukweli huu hauna utata kwa sababu vyombo vya habari vimeonesha mambo ya kushtua kutokea maeneo yaliyoathirika na sumu; watu walioathirika; na mifugo iliyokufa na kuumia na sumu itakayojulikana aina yake baada ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Ernest Mashimba kuchunguza sampuli alizopata.

Uongozi wa Kata umetoa takwimu kuelezea uzito wa tatizo. Zinaweza kupingwa na wahusika wakiwemo Barrick wenyewe.

Takwimu ni kitu muhimu. Lakini kabla ya kupata taarifa ya kitaalamu inayoweza kuja kututhibitishia takwimu, kwa sasa tuamini walioona madhara kwa macho yao.

Wameona uharibifu wa binadamu maana wapo walioathirika ngozi – televisheni zimeonesha baadhi yao, wapo pia wanyama walioathirika ngozi, na mazingira ya karibu na mgodi na mle unamopita mto Tigithe yanaonekana yalivyoharibika. Ni ushuhuda muhimu kabla ya kuthibitishiwa vifo vilivyotokana na sumu itokayo North Mara.

Hizi si taarifa nzuri kwa vyovyote vile kwa viongozi na wamiliki wa kampuni ya Barrick. Hazipendezi hata ningekuwa mimi ni sehemu yao. Sishangai wanavyozikanusha na kuzipinga.

Msemaji wa Barrick, Teweli Teweli, anasema: Maji yanayodaiwa na wananchi kuvuja kutoka kwenye mgodi yalitoka kwenye kifusi cha mchanga wenye mawe yatoayo kemikali.

Anaendelea, "maji hayo yenye rangi hayana madhara yoyote kwa binadamu na wataalamu wa Idara ya Mazingira ya mgodi huchukua vipimo vya maji katika maeneo yanayozunguka mgodi na kuonyesha kuwa yapo salama kwa matumizi ya binadamu na wanyama."

Mwandishi Manyerere Jackton aliyefuatilia kwa karibu anachoita "mgogoro kati ya wananchi na mgodi" ameandika: kinachotokea ni matokeo ya udhaifu wa pande tatu – Serikali, Wananchi na Mgodi.

Analaumu kila upande umechangia mgogoro. Serikali haikusimamia uhusiano mzuri kati ya waendeshaji mgodi na wananchi. Lawama hizo anazitupa pia Barrick. Analaumu wananchi wamekuwa wakihujumu mgodi na mali zake.

Ni ugunduzi muhimu unaohitaji kuzingatiwa na kufanyiwa kazi ili kutuliza uhusiano mbaya wa paka na panya kati ya mgodi na wananchi.

Wananchi wana haki ya kulalamika. Mgodi ni mali yao na dhahabu mali yao pia; naamini hivi hata kama wageni wamepewa kuundesha. Ni maliasili ambayo muumba amewajaalia wana Tarime.

Wana haki ya kunufaika nao, siyo kuhujumiwa, kwa hakika kuuliwa, nao. Maafa yamewakumba wakazi wa kata za Kemambo, Kewanja, Kibasuka na Nyamongo. Wanahitaji kusaidiwa na kufidiwa.

Nini sasa hukumu ya muuaji? Sheria za Tanzania zinaelekeza kwamba adhabu ya muuaji ni kifo. Je, wamiliki wa mgodi wauawe nao kama walivyosababisha mauaji Tarime?

Ni mkondo wa sheria. busara inataka kuona serikali inasimamia mkondo wa sheria kufanya kazi. Busara ingependa kuona mgodi wa North Mara unakuwa mfano wa uzingatiaji sheria na utu.

Tanzania si mahali pa mtu yeyote kujaribia. Watanzania wanastahiki utu na kuheshimiwa kwa haki zao kama binadamu. Kuwatweza kwa namna yoyote ile hakukubaliki.

Haya tunayoyaona kwenye maeneo ya uwekezaji yanayoendeshwa na wageni, kama vile Gurumeti, hayakubaliki na lazima yakomeshwe.

0
No votes yet