Ntagazwa: CCM hii inatupeleka kubaya


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
ARCADO Ntagazwa

ARCADO Ntagazwa, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), ameshtua watu baada ya kujiondoa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mwanasiasa huyo alijiondoa CCM katikati ya mchakato wa kura za maoni kwa lengo la kupata wagombea nafasi za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Anasema aliyoona katika mchakato huo yalimkera, yakamchefua na alipotazama kero, rushwa, unyanyasaji wa wananchi unaofanywa na vyombo vya serikali ya CCM, waziri huyo wa zamani akaamua kujiweka kando.

Taarifa hizo ziliwashtua wanasiasa na wanachama wengi wa CCM hata viongozi wa serikali.

Juhudi za viongozi wa CCM, kuwasiliana na Ntagazwa ili kumshawishi arudi, kwa maelezo kwamba kulikuwa na juhudi za kurejesha jina lake agombee ubunge katika Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo ziligonga mwamba.

Akiwa katika ofisi za kampuni ya Hali Halisi inayochapisha magazeti ya MwanaHALISI na Mseto, wiki iliyopita, alipigiwa tena simu akiambiwa kulikuwa na mpango wa kurudisha jina lake katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) uliofanyika Dodoma.

Ntagazwa alijibu, “Waambie I have cut my umbilical code with CCM – nimekata kitovu kinachoniunganisha na CCM.”

Ntagazwa amekuwa mbunge wa Jimbo la Muhambwe tangu mwaka 1980 hadi alipoangushwa na mbunge aliyemaliza muda wake Felix Tibendakijiko.

Kati ya 1983 na 1985 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi (1985—1987), Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii (1987—1990), na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira na baadaye Muungano.

Katika kinyang’anyiro cha mwaka huu kilichoshirikisha wanachama wote wa CCM kutoa maoni yao kwa njia ya kura, mchakato uligubikwa na kile alichokiita “rushwa kupita kiasi na upendeleo.”

“Binafsi nachukia rushwa, vitendo vya rushwa havifai; rushwa ilitawala sana kura za maoni,” alisema katika mahojiano na gazeti hili.

“Kule kwetu wapigakura walichukuliwa kutoka Burundi, bahati nzuri wengine wamekamatwa na kesi ipo. Hivi leo tumefikia hatua ya kuwaingiza Warundi waje kutuamulia mtu anayefaa kuwa kiongozi?” anahoji.

Shutuma za Ntagazwa zinakwenda kwa watendaji zaidi ndani ya chama na serikali kwamba wanaipeleka nchi pabaya.

“Ukisoma kitabu cha madhumuni, malengo na ahadi za mwanachama wa CCM, huwezi kuwa na ugomvi na chama hicho wala viongozi wake; kila kitu ni kizuri, upungufu uliopo ni wa kibinadamu.

“Lakini ukiangalia yanayotendwa sasa au yanayofanywa na watendaji, mengi hayafai. Kwa mfano, moja ya ahadi za chama inasema ‘rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa.’ Zamani tulikuwa tukiapa chini ya kiapo, lakini hali sasa ni kinyume chake,” anasema.

“Mtu anayekubalika kuwa kiongozi ni kwa nguvu ya rushwa, kwa hiyo haki ya mpiga kura haipo! Huyu hawezi kuwa kiongozi,” anasema na kusisitiza kwamba hicho ndicho kilichosababisha yeye kukata kitovu kinachomuunganisha na CCM.

Ntagazwa, ambaye ana shahada ya sheria aliyohitimu Chuo Kikuu cha Makerere, anasema mtu anapoangalia malengo na matendo ya CHADEMA, ataona kwamba yanashabihiana sana na malengo na matendo ya CCM wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, na siyo CCM ya leo.

Anasema hali hii si ishara nzuri kwa nchi kwani kuna kikomo cha uvumilivu.

“Binadamu akiona hakuna haki anaweza kufanya lolote. Nchi za Rwanda na Burundi zilifikia hapo zilipo baada ya wananchi kuona hawana haki, wala hawakufikishwa hapo na vyombo vya habari kama inavyodaiwa,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kwamba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anachukia pia rushwa kutumika katika kujipatia uongozi, lakini anashindwa kutokana na mfumo kugubikwa na rushwa.

Anasema mfumo uliopo sasa ndani ya CCM wa kujali pesa kupata uongozi umewafunika wengi kiasi kwamba matamko yote yanaonekana kelele tu.

“Mfumo huu wa kujali pesa unatupeleka pabaya,” anaonya.

Anasema alipokuwa mjumbe wa siasa alikuwa anaziona kasoro za uendeshaji. Aliwahi kumwandikia barua Yussuf Makamba, kumpongeza kwa kazi nzuri, lakini kuhoji vinapofanyika vikao katika ngazi za juu ajenda zinatoka wapi.

Hoja yake ilitokana na ukweli kwamba utaratibu wa ajenda haufuatwi; ajenda zinatakiwa kutoka chini; watu wazungumze, wajadili kero na matatizo yao kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Nilisema hivyo kwa sababu vikao vya chini havifanyiki; sasa ajenda zinatoka wapi?” anahoji.

Mbali ya kukerwa na mfumo ndani ya chama, Ntagazwa anakerwa pia na unyanyasaji wananchi unaofanywa na vyombo vya dola.

Akitoa mfano wa unyanyasaji anasema mwaka 1981, bunge lilitambua kwa sheria pori la Moyowosi (Moyowosi Game Reserve); ukawekwa utaratibu maalumu wa watu kuingia, kuvuna, kurina na kuwinda. Utaratibu huo mzuri ulitumika hadi mwaka 2005.

“Januari 2009 nilisononeka sana kusikia watu wasiopungua 20 wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa hifadhi kwa maelezo ya kuwa kwenye pori hilo kinyume cha sheria. Uongozi wa serikali ya mkoa umearifiwa lakini hakuna kilichofanyika,” anasema.

“Kilichonisikitisha zaidi ni mtu mmoja aliyekamatwa na askari na kukatwa sikio, eti ili iwe utambulisho ikitokea akatoroka. Sheria inataka mtu akikamatwa apelekwe mahakamani siyo kumpiga wala kuua, lakini askari wanafanya kinyume. Hawa ndio askari wa serikali ya CCM,” anasema.

Alipoulizwa kama atawania ubunge katika jimbo hilo kupitia chama chake kipya, Ntagazwa alisema ni ikiwa atapitishwa.

“Miaka yote watu wamekuwa wananiomba nigombee; nia ya kuwatumikia watu ipo, nikipitishwa na chama changu nitagombea,” anasema.

Alipoulizwa kama hali hii haitokani na hasira tu au wingi wa furaha ya ushabiki wa watu, alisema amefanya uamuzi akiwa timamu.

Ameonya kwamba hali hii isifananishwe na mwaka 1995 kulipokuwa na ushabiki wa NCCR-Mageuzi chini ya Augustine Mrema; na kwamba anapotazama malalamiko ya wana CCM kila kona ya nchi, anaona chama hicho kinaweza kuondoka safari hii.

Maelefu ya watu wanaojiunga na CHADEMA kwa sasa, ni baada ya kutoridhishwa na mchakato wa kura za maoni za kupata wagombea udiwani na ubunge, isipokuwa kwa kutumia nguvu ya pesa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: