Nyaraka EPA zaibwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 January 2009

Printer-friendly version
Zimo za Kagoda, Deep Green
Jinamizi lazidi kutanda BoT
Benki Kuu

UWEZEKANO wa serikali na Benki Kuu (BoT) kufanikiwa kupata ushahidi wa kuwatia hatiani waliokwapua mabilioni ya shilingi ni mdogo kufuatia taarifa kuwa nyaraka muhimu zimeibwa.

Hata mafaili na taarifa nyingine juu ya kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyokwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni, zinaweza kupatikana tu kwa ngekewa, chanzo cha habari ndani ya BoT kimeeleza.

MwanaHALISI lina taarifa kuwa tangu mwaka 1996, wakati fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zilipoanza kuchotwa, hakukuwa na utaratibu maalum wa kuchukua fedha kutoka benki.

“Hakukuwa na utaratibu kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji fedha – Financial Management Manual. Zilikuwa zikitolewa tu. Wahusika walikuwa wakifanya wanavyotaka, kama kuandikiana vimemo,” kimeeleza chanzo cha habari hizi.

Utaratibu huu, kimeeleza chanzo cha habari, “haukubaliki katika taasisi za fedha na hautambuliki kimataifa. Ingejulikana hakuna kanuni za utawala wa fedha, benki ingepata aibu na shughuli zake kukataliwa.”

Ni katika mazingira haya kampuni ya Kagoda ilifanikiwa kuchukua fedha BoT na kuzipitisha  katika matawi saba ya benki ya CRDB jijini Dar es Salaam kwa mtindo wa “kuingiza na kutoa papo hapo.”

Hadi sasa serikali haijasema nani anamiliki Kagoda, yuko wapi. Haifahamiki pia iwapo kuna yeyote aliyekamatwa kuhusiana na kampuni hiyo.

Haijafahamika pia iwapo Kagoda, yenye utata wa miliki na usajili, ni moja ya walioiba fedha BoT ambao walizirejesha kukidhi matakwa ya rais ili wasishitakiwe.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akichokonolewa na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, wakitaka kujua iwapo kweli Kagoda “imeiweka serikali mfukoni,” alisema “serikali haiogopi mtu yeyote. Hakuna wa kuigopesha. Tunafuatilia haya na tutatoa taarifa.”

Hadi sasa, mwanasiasa na mfanyabiashara mmoja, Rostam Aziz ndiye amekuwa akitajwa kuwa na uhusiano na Kagoda.

Kabla MwanaHALISI halijafungiwa, lilikuwa limeoanisha mawasiliano kati ya Kagoda na BoT  yaliyoonyesha matumizi ya simu ya kampuni ya Caspian inayodaiwa kuwa mali ya Rostam Aziz.

Utoaji fedha kutoka akaunti ya EPA uliidhinishwa 30 Oktoba 1996 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Peter Ngumbullu.

Katika barua yake, Kumb. Na. TY/AG/BOT/INST/1/12, kwenda kwa gavana wa BoT, Dk. Idris Rashid, Ngumbullu alisema serikali imeagiza matumizi ya Sh. 100 bilioni kutoka akaunti ya EPA kila mwaka kwa kipindi cha miaka 50.

Utoaji holela wa fedha kwenye akaunti ya EPA – bila uhakiki wa wanaodai, viwango wanavyodai, mahali walipo na uhalali wa madai yao – uliendelea hadi mwaka 2007.

Taarifa za ndani ya BoT zinasema mwaka 2007 BoT ndipo walipotengeneza utaratibu wa dharura unaolingana na mwongozo wa utoaji fedha na kubuni nyaraka zinazoonyesha kulikuwa na utaratibu tangu 1997.

“Nakuhakikishia hakukuwa na nyaraka kati ya 1996 na 2007. Hii ni kwa kuwa hakukuwa na utaratibu. Kwa hiyo nyaraka zinazoonyeshwa ni za kughushi,” kimeeleza chanzo chetu.

MwanaHALISI iliongea na Gavana wa BoT, Profesa  Benno Ndullu kutaka kujua iwapo nyaraka zinazotumiwa na benki hivi sasa na kipindi cha miaka 10 hadi 2007 zilikuwa za kughushi.

Akiongea taratibu, kwa njia ya simu, Profesa Ndullu alisema hana taarifa juu ya nyaraka za kughushi ndani ya benki na kwamba anaona ni zilezile.

Kuhusu nyaraka zilizoibwa alisema, “Sina taarifa hizo. Kama unasema kuna taarifa za aina hiyo, nitafuatilia ili kujua ukweli.”

Profesa Ndullu aliteuliwa na rais kuwa gavana wa BoT, Januari mwaka jana, baada ya uteuzi wa Daudi Ballali kutenguliwa. Ballali alikuwa gavana wa benki tangu 1997. Ballali alifariki dunia.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, hata baadhi ya nyaraka ndogo na chache zilizokuwepo na ambazo hazikidhi utaratibu wa utoaji fedha, zimetoweka “katika mazingira tatanishi.”

Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi walioongea na mwandishi wa habari hizi walisema ni maofisa wa BoT walioghushi nyaraka na kurudisha tarehe nyuma ili kuweza kuonyesha kuwa utaratibu ulibuniwa na kuanza kutumika tangu mwaka 1997.

Lengo la kufanya hivyo, lilikuwa kuzuia wakaguzi wa nje kugundua udhaifu wa miaka 10; kuridhisha wafadhili pamoja na wananchi waliokuwa wameshupalia taarifa za utawala wa fedha BoT.

Mtoa taarifa hizi alisema ni jambo linaloeleweka kwa viongozi waandamizi wa benki hiyo kuwa uwekaji nyaraka za kughushi ulilenga kufunika uhalifu na kulinda baadhi ya wahusika wakuu.

Makampuni 22 yalighushi majina na madai na kujichotea Sh. 133 bilioni kutoka akaunti ya EPA katika kipindi cha 2005 na 2006.

Mbali na makampuni 22 yaliyotajwa, kuna makampuni mengine yanayodaiwa kuchota zaidi ya Sh. 400 bilioni kutoka BoT kinyume cha taratibu.

Miongoni mwa makampuni hayo ni Tangold, Deep Green Finance Limited, Meremeta na Mwananchi Gold Ltd.

Fedha nyingi zilizoibwa BoT zilicukuliwa kati ya Julai na Desemba 2005 kipindi ambacho kilikuwa cha kampeni na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Habari za ndani ya BoT zinasema bila kuwa na utaratibu, Gavana wa wakati huo, Dk. Daud Ballali, aliendesha BoT kama chombo binafsi.

Taarifa zinasema ukiukaji wa taratibu ulishika kasi sana muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Hapa ndipo Ballali aliamua kutumia hata watendaji wa ngazi ya chini kuidhinisha malipo.

Imeelezwa kwamba Ballali alichukia sana kuona faili la Kagoda likikabidhiwa kwa maodita wa Ernst & Young waliokagua akaunti yaEPA. Baada ya hapo aliagiza utengenezaji wa kabati maalum kwa ajili ya kuhidashi nyaraka nyeti likiwemo faili la Kagoda.

Taarifa zinasema funguo za kabati la “mafaili nyeti” zilikabidhiwa kwa mmoja wa wafanyakazi wa BoT ambaye tayari yuko mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi kwenye akaunti ya EPA.

Hata hivyo, ukosefu wa utaratibu wa kutoa fedha akaunti ya EPA bado unaisumbua hadi leo. Kwa mfano, tarehe 25 Julai 2005 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja alimwandikia Katibu mkuu wa Hazina barua yenye Kumb. Na. EB/AG/40/01/49.

Katika barua hiyo, Mgonja aliruhusu BoT kutumia kiasi cha Sh. 66 bilioni tu ili kukamilisha kiasi cha Sh. 100 bilioni kinachoruhusiwa baada ya maombi ya benki hiyo.

Alikuwa akijibu barua Kumb. Na. DESED/60/48/VOL/VI ya tarehe 18/7/2005 ambamo BoT ilikuwa inasema tayari ziliishatumika Sh.34 bilioni; hivyo ilihitajika ruhusa ya serikali ili kupata Sh. 66 bilioni ili kufikia kiwango cha Sh.100 bilioni kilichoruhusiwa.

Katika hali inayoacha maswali megi bila majibu, Gavana Ballali, siku nne tu baada ya barua ya serekali, kupitia kwa Mgonja, iliyoruhusu matumizi ya Sh. 66 bilioni, aliandika barua ya kuikana barua ya awali iliyoandikwa na maofisa wake na kuomba ruhusa ya matumizi ya Sh. 80 bilioni juu ya hizo 66 bilioni.

Katika barua yake ya tarehe 29 Julai 2005 yenye Kumb. Na. DCSED/60/48/VOL.VI/101, Gavana  Ballali anamkumbusha Mgonja mazungumzo yao kwenye simu. Anasema, “Kama tulivyoongea katika simu kuwa barua ya awali ilikuwa mkanganyiko mtupu.”

Ballali alimtaka Mgonja kuifuta barua hiyo ambayo kimsingi ndiyo iliyokuwa inafuata na kuzingatia utaratibu uliowekwa na serikali mwaka 1996.

Kwa mujibu wa barua hiyo Na. EB/AG/40/01/56 ya 9 Agosti 2005 Mgonja alifuta barua yake ya awali na kutoa ruhusa ya matumizi ya Sh. 80 bilioni bila kupata maelezo yoyote kuhusu fedha zinazodaiwa kuombwa kimakosa.

Utata wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa bado unaendelea hadi mwaka jana ambapo Profesa Ndullu anafafanua masharti ya mwaka 1995 yanayohusu matumizi ya fedha kwenye akaunti ya EPA.

Katika barua hiyo Kumb. Na. A10/48 TEMP ya 28 Februari 2008, Professa Ndullu anamwambia Mgonja kuwa masharti ya mwaka 1995 hayaendani na mfumo wa viwango vya kimataifa vya kutoa ripoti za fedha – International Financial Accounting Reporting Standards (IFRS) .

Lakini mtoa taarifa hizi anasema Ballali alikuwa na jeuri pia hata kataika mawasiliano na serikali. Mathalani, tarehe 8 Julai 2005 aliijibu serekali kwamba ni vigumu kutoa taarifa za matumizi ya fedha za EPA katika muda mwafaka kutokana na malipo kufanyika kwa maombi maalum na bila ratiba maalum. Katika barua yake kwa katibu mkuu hazina, Kumb. Na. DCSED60/48/VOL.VI/IOI, Ballali alisema  kompyuta za benki zilizohusika katika malipo zilikuwa zimeharibika na kwamba zitakapopona taarifa hizo zitafikishwa serekalini.

Mpaka sasa ni watuhumiwa wanne tu ambao wameshafikishwa mahakamani kwa upande wa BOT.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: