Nyota ya Kanumba ilianzia Bugoyi


Mohamed Akida's picture

Na Mohamed Akida - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

KATIKATI ya umaarufu mkubwa, umashuhuri katika fani ya filamu na matarajio makubwa katika tasnia hiyo, nyota ya msanii Steven Charles Kanumba imezimika kama mshumaa uliopigwa na upepo mkali.

Eti dakika chache akiwa anajiandaa kutaka kutoka kwa matembezi ya usiku Jumamosi iliyopita na mdogo wake Seth Bosco, mauti yakamkuta ghafla chumbani kwake.

Kila mmoja akabaki anajiuliza amepigwa, amesukumwa, amepewa kitu cha kudhuru uhai wake? Je, ni kweli ugomvi na mpenzi wake, Elizabeth Michael “Lulu” ndiyo kisa cha mauti hayo?

Sisi hatuji, labda polisi, lakini ukweli amewaacha wazazi kwenye majonzi makubwa, marafiki wakilia, jamaa na ndugu wakisikitika huku maelefu ya wapenzi wa filamu zake wakiomboleza nchi nzima.

Umati mkubwa wa watu unaofurika nyumbani kwake Sinza, Vatican tangu ilipotangazwa kwamba mwigizaji huyo anayekonga nyoyo za watu kila anapoigiza, na wingi wa salamu za rambirambi kutoka kila kona Afrika na hasa Afrika Mashariki ni ushahidi kwamba tasnia ya filamu imempoteza mtu muhimu.

Kila mmoja atamkumbuka kivyake msanii huyo ambaye nyota yake ya ucheshi na uigizaji ilichomoza tangu akiwa mdogo alipokuwa anasoma Shule ya Msingi ya Bugoyi iliyopo kata ya Ngokolo mkoani Shinyanga.

Hapo ndipo nilisoma naye kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1996 nilipohamia mkoani Singida katika Shule ya Msingi Utemini. Baba yangu alihamishiwa kikazi Singida.

Hadi darasa la sita, Kanumba ambaye alifahamika kwa kifupi kama Steve, alishaanza kujizolea umaarufu kwa kushiriki vichekesho na michezo ya kuigiza shuleni pale.

Steve hakuwa rafiki yangu. Sababu hasa ya kutokuwa karibu naye ni makundi tofauti; mimi nilikuwa mchezaji mpira katika timu ya shule hivyo nilikuwa karibu zaidi na wavulana ilhali yeye, kutokana na ucheshi wake alivutia kwa wasichana.

Katika fani ya uigizaji shuleni, Steve alishirikiana sana na Blandina Chagula msanii mwingine maarufu katika uigizaji kama Johari. Kutokana na ucheshi wake na ushiriki katika uigizaji, Steve alifahamika sana shuleni.

Mara nyingi alikuwa akiteuliwa na walimu kuandaa igizo fupi au kichekesho na wanafunzi wengine kuburudisha wakati shule inafungwa.

Tangu nilipohama sikuonana na Steve hadi mwaka 2000 nilipomwona kwa mara ya kwanza akiwa mmoja wa waaigizaji wa Kaole Group kundi lenye maskani yake Kigogo jijini Dar es Salaam.

Nilishtuka lakini nilifurahi kuona mwenzangu kipaji chake kimelipa hadi kimemfikisha kiwango cha kuwa msanii mwenye mafanikio kuliko wengi tuliong’ang’ania kupata mafanikio katika soka.

Tangu wakati huo, Kanumba na Johari wamekuwa wakipamba vichwa vya magazeti mengi, redio na runinga kutokana na uigizaji, utunzi na uongozaji mzuri wa kazi zao.

Kanumba alipoona fani hiyo inalipa hakutaka kuganda Kaole, aliondoka na kuanzisha kampuni yake binfsi ya Filamu aliyoipa jina la ya Kanumba The Great ambayo alitumia kutunga na kuongoza siyo tamthiliya tu bali zaidi filamu.

Tunaweza kutofautiana kwa vigezo na mtazamo, lakini kwa maoni yangu, Kanumba hakuwa na mshindani katika fani hiyo nchini.

Kiu yake ya kutaka mafanikio zaidi ilimpeleka hadi Nigeria ambako alishirikiana na wasanii maarufu wa kule. Filamu ya Dar to Lagos aliyoshirikiana na Mercy Johnson ni mfano halisi.

Baada ya hapo alitengeneza filamu nyingi akishirikiana na mwigizaji nguli kutoka Nigeria, Ramsey Nouah ambaye pia aliwahi kumleta nchini mwaka jana wakati wakiandaa filamu ya Devil Kingdom iliyofanya vizuri sokoni.

Kadhalika wakati wa uhai wake Kanumba alishiriki kuigiza filamu na tamthiliya zaidi ya 12 kama vile Jahazi, Dira, Tufani, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Johari 2, Dangerous Desire 9, Dar 2 Lagos, Riziki na Cross my Sin.

Kampuni ya Kanumba The Great, kama ilivyo kwa kampuni zenye mafanikio, alikuwa akigusa na matatizo ya watu wengine.

Mathalani 25 Agosti 2011 akishirikiana na kampuni ya Steps inayosambaza kazi zake alikwenda Meeda Sinza kukabidhi msaada wa nguo na chakula katika kituo cha kulelea watoto yatima cha CHAKUWAMA.

Baadaye alikwenda katika kituo cha kulelea wazee wasiojiweza na watu wenye ulemavu wa macho na ukoma cha Nunge, Kigamboni. Nilifuatana naye kote huko wakati huu nikiwa kama mwandishi na siyo mcheza mpira kama nilivyo achana naye mwa 1996 kule Shinyanga.

Kupitia tasnia hiyo ya Filamu Kanumba, katika umri wake wa miaka 28, alifanikiwa kuwa na nyumba, kumiliki magari matatu ya kifahari, pamoja na kufahamika nje ya mipaka ya Tanzania, kutengeneza filamu na Wanigeria, lakini pia aliwahi kualikwa kama mgeni katika uzinduzi wa mashindano ya Big Brother Africa mwaka 2009 nchini Afrika Kusini.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)