Nyota ya Kaseja kung’ara tena Misri?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version

MASHABIKI wa soka wa jijini Cairo, Misri watakuwa na shauku ya kumwona tena Juma Kaseja Juma, kipa wa Simba aliyezuia mikwaju ya wapigajimahiri wa Zamalek katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Umahiri wa Kaseja langoni, mchezaji pekee mkongwe aliyebaki, ndio ulichangia miamba ya Tanzania Bara mwaka 2003 kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek tena kwenye ardhi yao na mbele ya maelfu ya mashabiki wao, Cairo. Kaseja alipangua penalti mbili.

Mchezo huo wa marudiano ulifikia hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti baada ya Simba kushinda kwa bao 1-0 mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam na Zamalek ikashinda kwa bao 1-0 jijini Cairo lakini Simba ilishinda kwa penalti 3-2.

Kaseja anatarajiwa kuiongoza Simba kurejea historia hiyo ya mafanikio, klabu hiyo itakapokutana Jumamosi ijayo na Wydad Athletic Club (WAC) de Casablanca ya Morocco kwenye uwanja wa Petrosport, Cairo.

Pambano hilo litazikutanisha klabu hizo mbili kwa mara ya kwanza huku zikiwa na historia tofauti ya mafanikio katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Safari hii zinakutana kwa mara ya kwanza kuandika ukurasa mwingine wa mafanikio katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumpata mbabe kati ya vibonde vilivyochapwa na mabingwa mara mbili mfululizo Afrika, TP Mazembe ya DR Congo.

Mechi hiyo ya mtoano itakuwa ya kujaza nafasi iliyoachwa wazi na TP Mazembe walioondolewa kwa ukiukwaji wa kanuni za usajili.

Timu zote mbili, Simba na WAC zilifungwa na TP Mazembe katika hatua tofauti. Simba ilinyamazishwa kwa jumla ya mabao 6-3 katika raundi ya kwanza ilhali WAC walinyolewa kwa jumla ya mabao 2-1 karika raundi ya pili.

Hata hivyo, ilibainika kwamba TP Mazembe ilimtumia Jamvier Besala Bokungu anayedaiwa kuwa mchezaji wa Esperance ya Tunisia. Kwa ukiukwaji huo wa taratibu, CAF imeamuru Simba na WAC kusaka mshindi wa kuingia robo fainali.

Timu itakayoshinda itaingia Kundi B la robo fainali lenye timu nyingine za Al Ahly ya Misri, Esperance  na Maloudia Alger ya Algeria. Kundi A lina timu za Al-Hilal ya Sudan, Enyimba ya Nigeria, Raja Casablanca ya Morocco naCotonsport Garoua ya Cameroun.

Mafanikio

WAC klabu iliyoanzishwa mwaka 1937 maarufu kama Wekundu na Weupe wa Casablanca kutokana na kuvaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe na mara moja moja za bluu, inajivunia ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika iliotwaa mwaka 1992. Haijatwaa tena.

Lakini ilisubiri hadi mwaka 2002 ilipotwaa ubingwa wa Kombe la CAF. Mwaka 1992 na 2002 ilikuwa mshindi wa pili wa Kombe la Super la CAF.

Simba haijawahi kutwaa mataji mawili hayo isipokuwa mwaka 1974 ilifikia nusu fainali ilipotolewa kwa penalti na Melhal el Kubra ya Misri wakati michuano hiyo bado ikiitwa Klabu Bingwa ya Afrika. Hatua nyingine ya juu kwa Simba kufikia ilikuwa mwaka 2003 ilipoitoa Zamalek ya Misri na kuingia hatua ya robo fainali ya ligi hiyo.

Mwaka 1993, Simba iliweka historia nyingine ilipoingia fainali ya Kombe la CAF lakini ilichapwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast mjini Dar es Salaam. Mafanikio mengine ya Simba yako katika ngazi ya kanda.

Kanda

WAC imeshiriki na kutwaa ubingwa mara kadhaa katika michuano ya nchi za Asia na Afrika mwaka 1994; ubingwa wa nchi za Kiarabu mwaka 1989 na ilishika nafasi ya pili katika mashindano hayo  mwaka 2008 na 2009.

Mwaka 1990 ilitwaa ubingwa wa Kombe la Super kwa nchi za Kiarabu.

Vilevile klabu hiyo iliwahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Mohamed V mwaka 1979; mara tatu ubingwa wa Kombe la Ligi ya Nchi za Afrika Kaskazini na Kombe la Super la Afrika Kaskazini.

Kwa upande wake Simba imetwaa Kombe la Tusker mara tano; na kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati inayosimamiwa na CECAFA mara sita

Mataji ya ligi

Tangu wakati ikiitwa Sunderland mwaka 1975, Simba maarufu kama Wekundu wa Msimbazi kutokana na jezi zao nyekundu, imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara (zamani Daraja la Kwanza) mara 17. Misimu iliyotwaa ubingwa huo ni 1965, 1966, 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007/2008, 2009/10.

Kwa upande wake WAC imetwaa mara 12 ubingwa wa Batola (Ligi Kuu ya Morocco); mara tano kombe la Ligi ya Morocco; mara tisa Kombe la Morocco.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: