Nyuma ya pazia la posho za wabunge


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version

SIKU 68 tangu Mizengo Kayanza Peter Pinda ateuliwe kuwa waziri mkuu kuchukua nafasi ya Edward Lowassa alikumbana na mtihani wa kwanza mgumu, kumkalisha chini waziri wake na kumwambia ajiuzulu.

Februari 12, 2008 Rais Jakaya Kikwete alimteua Pinda kushika madaraka hayo makubwa, lakini Aprili 20, 2008 alimkalisha chini aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na kumwambia ajiuzulu nafasi hiyo kwa kashfa ya kuweka nje ya nchi dola za Kimarekani bilioni moja.

Fedha hizo, kwa mujibu wa Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Rushwa ya Uingereza (SFO), ni mgawo wa fedha kutokana na ununuzi wa rada katika kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.

Alipoulizwa Chenge kama kweli aliweka kiasi kikubwa hicho cha fedha, alijibu kwa simu kutoka ziarani China kwamba hivyo ni vijisenti tu. Majibu hayo yaliwaudhi Watanzania na aliporejea tu nchini akitokea China ambako alikuwa katika msafara wa Rais Jaka Kikwete, aliambiwa ajiuzulu.

Pinda naye amefikia kuita Sh. 8.44milioni ambazo kila mbunge atapokea katika kipindi cha miezi miwili kama posho – siku za kazi 52 na wikiendi nane – ni kidogo na hazitoshi. Amelinganisha na kiasi gani wanachopewa kina nani?

Katika Bunge la Bajeti, wabunge hukaa takriban miezi miwili (siku 60) ambapo kila siku hulipwa posho ya safari ya Sh. 80,000 na kikao Sh. 70,000. Hivyo siku ya Jumapili hulipwa posho ya safari tu bila ya kikao. Hii ni mbali ya mshahara wa Sh. 2.5milioni kwa mwezi na posho ya mafuta na fedha za Mfuko wa Jimbo.

Pinda, ambaye itabidi aanze kujiuliza anakosea wapi sasa kuliko zamani, akijibu swali la mbunge wa CUF, aliyetaka kujua msimamo wa serikali juu ya posho, alisema Suala la kupunguza posho limekuzwa mno.

Serikali haiwezi kuondoa posho kwa matakwa ya mbunge mmoja
Hata posho zenyewe ni kidogo maana huishia kutoa nauli kwa watu wanaojitokeza kuomba msaada mbalimbali ikiwemo nauli.

Mbunge ambaye hataki kupokea aandikishe jina lake hazina ili ikatwe.

Hata CHADEMA wanaopinga posho hizi wanamezea sana mate.

Mjadala

Wananchi wa kawaida, wakulima ambao amejinasibu kuwa ni mtetezi wao, wafanyakazi wanaokabiliwa na mazingira magumu kama walimu, bila posho ya kutuliza akili zao hawawezi kukubali majibu haya.

Mjadala wa posho umekuja kutokana na pendekezo la serikali lililomo kwenye hotuba ya Bajeti juu ya kusudio la kupunguza baadhi ya posho. Kwa bahati mbaya sana posho za kuondolewa hazijaainishwa, lakini hotuba ya Bajeti ya Kambi ya Upinzani imependekeza maeneo.

Kama serikali isingekuwa imewasilisha hoja ya kukata posho katika baadhi ya maeneo, Waziri mkuu Pinda angekuwa na kila sababu ya kuisema kambi ya upinzani kwamba imekuza mno suala hilo.

Lakini wapinzani hawana haki ya kutoa mapendekezo juu ya namna nzuri ya kubana matumizi ya serikali yao? Kwani mambo mangapi mazuri wametoa na bado serikali imepuuza?

Kama ni suala la mazingira magumu nani hajui walimu wanavyolazimika hata kuuza ubuyu, karanga, maandazi darasani ili wapate senti za ziada? Nani hajui kwamba posho ya mbunge ya siku mbili tu ni mshahara wa mwalimu kwa mwezi?

Mwalimu anapewa kitu gani cha ziada ili wakienda watu hasa wazazi wanaohitaji msaada awapatie bila kuathiri mshahara wake kama ilivyo kwa wabunge? Mbona kwa miaka mingi, watumishi wanaofanya kazi katika mazingira magumu na muda mrefu kama walimu na wauguzi vijijini hawasikilizwi kilio chao?

Pinda asingeweza kuwa na majibu tofauti na hayo kwa sababu hoja hizo ndizo zilitumika kuombea posho kwa wabunge.

Nyuma ya pazia

Hata hivyo, kuna sababu zilizofichika ambazo Waziri mkuu hawezi kuweka wazi. Uamuzi wa kuwapa posho wabunge, wanajeshi na hata polisi ni mpango wa nchi nyingi duniani hasa za Afrika kupunguza uwezekano wa serikali zilizoko madarakani kukataliwa na kuondolewa.

Katika nchi ambazo demokrasia bado ni changa kama Tanzania, wabunge wote wa chama tawala, kazi  kubwa bungeni ni  kuunga mkono hoja na kudhoofisha hoja za upinzani. Wao hujiweka nafasi ya mawaziri kuzima hoja za wapinzani.

Wanadhani kuwa wakikosoa kwa uhuru wao watakuwa wamesaidia serikali kuondolewa madarakani; wanahofu wasipounga mkono wanaweza kukosa nafasi za uteuzi. Hivyo wanaipa tuzo serikali kwa kuipigia makofi kwa kila jambo ili nayo ilipe fadhila kwa kuwapa wabunge posho kwa kazi ambayo wanalipwa mshahara.

Ndiyo maana, wakati wafanyakazi wengi mishahara yao ni midogo na hawawezi kununua hata pikipiki, serikali hiyo hiyo imewapa fursa wanasiasa kukopa magari ya bei mbaya.

Ndiyo maana, wanajeshi wengi huteuliwa kuwa wakuu wa wilaya, mikoa na hata kupelekwa nje kuwa mabalozi. Hii inasababisha wanajeshi kukaa mkao wa kusubiri uteuzi wowote.

Ndiyo maana wanajeshi, polisi na askari magereza kote nchini wanaweza kupanda gari bure kama vile nchi hii wafanyakazi wanaokabiliwa na mazingira magumu ya kazi ni wao tu.

Hata marais wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, isipokuwa Mwai Kibaki (Kenya) – Pierre Nkurunziza (Burundi), Paul Kagame (Rwanda), Yoweri Museveni (Uganda), pamoja na kuwa wasomi ama wa sheria au uchumi ni wanajeshi. Na kwa utuki tu, Rais Jakaya Kikwete pia ni mwanajeshi.

Makamanda hawa wenye magwanda wameingia kwenye siasa; wanaandaa chaguzi za ‘kidemokrasia’, wapigakura wasio na demokrasia wanashiriki, matokeo yakitolewa magwanda hushinda iwe isiwe. Kwanini? Kwa sababu wanaosambaza maboksi ya kura na kuyarejesha ni hao hao wanajeshi.

Joseph Kabila alitwaa madaraka Januari 2011, akitokea kambini baada ya kifo cha baba yake Laurent-Désiré Kabila. Julai 2006 ulifanyika uchaguzi mkuu lakini matokeo yake yakawa chanzo kikuu cha mvutano na hata mpinzani wake Jean-Pierre Bemba kufunguliwa kesi katika mahakama ya kimataifa.

Mwanajeshi mwingine anayeingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Salva Kiir wa Sudan Kusini ambayo inatarajiwa kutangazwa nchi huru Julai 9, 2011.

Katika mfumo huu, kiongozi gani ataacha kufikiria kuwapa posho wanajeshi? Kwa kuwa wanaopitisha ni wanasiasa, mbunge gani ataacha kujifikiria kwanza?

Ni dhahiri, Pinda anapigia debe mfumo huu wa rushwa iliyowekwa kikanuni kwa taasisi hizi kuepusha serikali yake ‘kupigiwa’ kura ya kutokuwa na imani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: