Nyumba ya Kikwete inaungua


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 November 2009

Printer-friendly version
Gumzo
Rais Jakaya Kikwete

KAMATI ya rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi iliyoundwa kutafuta "kiini cha uhasama" miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), imezidisha nyongo.

Chama kimegawanyika. Bunge limeparaganyika. Serikali imetumbukizwa katika mgogoro na rais ametajwa kuwa sehemu ya tatizo.

Utaratibu wa kamati ya “kutafuta kiini cha tatizo,” kuruhusu wabunge "kuvuwana nguo hadharani," ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa ufa. Kamati ilipewa jukumu la kutafuta kiini cha tatizo, lakini inaonekana imezidisha mgogoro.

Baadhi ya wabunge wametumia udhaifu huo wa kamati kushushia tuhuma wenzao. Wapo waliomtaja Spika wa Bunge, Samwel Sitta kuwa ndiyo kiini cha tatizo.  

Mbunge wa kuteuliwa Kingunge Ngombale-Mwiru ni miongoni mwa waliotuhumu Sitta, kwamba “anahujumu serikali.”

Ngombale alirudia madai yake aliyoyatoa katika mkutano wa NEC, kwamba Sitta anaendesha Bunge kibabe. Anapendelea baadhi ya wabunge waliopachikwa jina la “mitume 12.”

Wengine wameshusha tuhuma ambazo zimemgusa hata rais aliyepo madarakani. Mfano hai ni madai ya Waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba kwamba kelele za kupinga ufisadi zinazotolewa na mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, zinatokana na chuki na uchu wa kukosa madaraka.

Simba amesema Kilango alitaka kuwa Fest Lady, lakini baada ya mumewe kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 na Kikwete, ameamua kuhujumu serikali.

Hakuishi hapo. Alisema, “Kilango na mumewe” wamekuwa wakifadhiliwa na mtuhumiwa mkuu wa ufisadi nchini Jeetu Patel; “ndani ya CCM hakuna asiyefisadi.”

Alidai kuwa Patel alitoa Sh. 200 milioni kufadhiri harakati za urais wa Malecela na sherehe ya harusi ya wanandoa hao wawili.

Kwanza, kauli ya Simba kwamba ndani ya CCM hakuna asiyefisadi, imeongeza chuvi kwenye kidonda. Kauli hiyo, inaweza kutumiwa na wapinzani wao kujenga hoja kwa wananchi kuwa hiki si chama cha siasa, bali genge la wahalifu.

Kauli ya Simba inafunga mdomo Kikwete. Sasa itakuwa vigumu tena kusema kwamba chama chake na yeye mwenyewe si sehemu ya ufisadi uliyopo nchini.

Pili, kauli ya waziri inaweza kutumiwa na wapinzani wa serikali kujenga hoja kuwa Rais Kikwete anaendesha serikali kwa chuki za uchaguzi. Hatua ya kufikisha mahakamani Patel imetokana na msimamo wake wa kuunga mkono Malecela.

Hili linapata nguvu hasa baada ya serikali kushindwa kufikisha mahakamani kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Pamoja na lundo la ushahidi kuanikwa hadharani kuhusu Kagoda, lakini serikali imeshindwa kuchukua hatua. Anayetajwa kumiliki Kagoda ni mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Hivyo kauli ya Simba inaweza kuonekana machoni mwa wengi kuwa kutofikishwa mahakamani Rostam kumetokana na yeye (Rostam) kuunga mkono Kikwete na kufikishwa kwa Patel kumetokana na kuunga mkono Malecela.

Ikifika hapo, hadhi ya serikali ya kusimamia sheria bila upendeleo, itakuwa imepotea.

Tatu, wanachama wa CCM na wananchi wengine wanawezachukulia kauli ya Simba kuwa uhasama uliyopo miongoni mwa wabunge umetokana na kinyongo cha urais kwa Malecela.

Hali hiyo inachochea uadui zaidi. Inamuweka Malecela katika wakati mgumu wa kukitumikia chama chake. Na kwa kuwa Malecela ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) inaongeza ufa mwingine ndani ya chama.

Lakini Simba anajua mchango wa Malecela ndani ya chama chake. Anajua jinsi alivyojitoa usiku na mchana kuhakikisha CCM inashinda katika maeneo yote ambayo amesimamia chaguzi ndogo.

Simba anajua kuwa hii haikuwa mara ya kwanza Malecela kufutwa katika hatua za mwanzo za kinyang’anyiro cha urais.

Mwaka 1995 ilikuwa hivyo pia. Sasa kama hoja ni Malecela na urais, mbona mwaka 1995 hakufanya hivyo?

Mwingine ambaye ameongeza ufa, ni Mahanga aliyenukuliwa akituhumu Kamati Teule ya Bunge, iliwasilisha “ripoti feki.”

Tofauti na Simba, Mahanga alisema kiini cha mgogoro huo ni Spika Sitta aliyeutaka uwaziri mkuu.

Alisema Sitta alianza maandalizi ya kuwa waziri mkuu mapema. Siku moja kabla Edward Lowassa kutangazwa kushika nafasi hiyo, Sitta alieleza hilo mmoja wa marafiki zake.

Mahanga alitetea Lowassa kana kwamba Lowassa ni “nabii.” Kwamba Richmond aliyoipa mkataba wa kufua umeme wa dharula, haikuwa kampuni ya mfukoni.

Mahanga ameficha ukweli kwamba wabunge wa Bunge la Muungano waliapishwa 28 Desemba 2005. Siku iliyofuata (29 Desemba 2005) walimchangua Sitta kuwa Spika wao.

Tarehe 30 Desemba 2005, rais aliteuwa waziri mkuu na kutangazwa na Spika Sitta. Hii ni siku sita baada ya Bunge kumchagua Sitta kuwa spika.

Katika mazingira hayo, Sitta asingeweza kueleza mmoja wa wabunge wa mkoa wa Shinyanga siku moja kabla ya Lowassa kutangazwa kuwa waziri kuwa yeye ndiye atashika nafasi hiyo.

Hapa Mahanga amepotosha. Hata waliomtuma wanajua hilo. Hata wajumbe wa kamati ya Mwinyi wanajua kwamba siku moja kabla ya Lowassa kutangazwa kuwa waziri mkuu, tayari Sitta alishakuwa Spika.

Ilikuwa ni jukumu la kamati kuchuja maneno. Kukemea wanasiasa wanaopotosha ukweli na wanaochochea uhasama.

Kamati ilitakiwa kupima maneno ya Mahanga na kumzuia ili asiendeleze kujenga ufa. Kamati ya Mwinyi inajua kuwa nchi kama hii ambayo rais ndiye mtendaji mkuu spika ni zaidi ya waziri mkuu.

Hivyo kwa vyovyote vile, Sitta asingehujumu serikali kwa kisingizio hicho. Wajumbe wa kamati wangemuomba Mahanga ushahidi mwingine.

Lakini kuendelea kunyamazia maneno ya aina hii, ndiko kulikosababisha wajumbe wengine kuamka vitini na kuporomosha matusi.

Miongoni mwao ni Andrew Chenge. Huyu alitumia nafasi hiyo kujitetea kutokana na kashfa mbalimbali zinazomkabili. Chenge alisema mikataba yote ambayo serikali imeridhia imepitia katika kikao cha baraza la mawaziri; yeye peke yake hakuwa na ubavu kuingiza nchi

Kikwete tuhuma; alikuwa mjumbe wa baraza la mawaziri wakati mikataba mingi ya kinyonyaji inasainiwa.

Alikuwa ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri wakati wa kupitisha mkataba kati ya Shirika la Reli la Taifa (TRC) na kampuni ya Reli ya India (RITES).

Chenge alikuwa anaficha udhaifu wake. Alikuwa hataki kukubali ukweli, kwamba wakati mikataba hii inasainiwa yeye ndiye aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali. Ni ushauri wake ulioingiza nchi katika mkenge.

Hata mkataba wa RITES ulisainiwa wakati Chenge akiwa waziri wa Miundombinu. Lakini amesimama imara kupinga ukweli huu.  

Ukiacha hayo yote, kamati ya Mwinyi imesaidia wananchi kujua sura halisi ya viongozi tulionao ndani ya CCM. Viongozi waongo, wanaoshindwa kusimamia kile wanachokiamini na wanaoweza kutumia hata uwongo kupotosha ukweli.

Lakini taifa limejua watu ambao Kikwete amebeba na kuingiza katika serikali yake. Watu alioamini kuwa watakubali kuwajibika kwa yaliotendeka wakati wa uongozi wao, kumbe ni chui aliojivisha ngozi ya kondoo.

Hatua ya Chenge kujivua na katika kashfa ya mikataba na vitimbwi vya Lowassa kutaka kujisafisha na zimwi la Richmond ikibidi hata kwa kumuingiza Kikwete mwenyewe, kunaonyesha kuwa Kikwete amezunguukwa na watu wa aina gani.

Kama alivyosema mbunge wa Singida Vijijini, Razalo Nyarandu, kwamba CCM kimefika hapo kilipo kutokana na kuacha misingi yake mikuu ya uongozi.

Haukuwa utamaduni wa CCM kuvuana nguo hadharani. Haukuwa utamaduni wa chama hiki, viongozi wake kukana ukweli na kusingiziana uwongo; kila mwanachama aliapa na kuhubiri tena kwa sauti kali “majungu na fitina kwangu ni mwiko.”

Lakini leo, majungu na fitina “ndiyo mtaji wa kubaki madarakani.” Kubwa linalosikitisha haya hayafanywi na kizazi cha sasa. Yanafanywa na kusimamiwa na viongozi wa kale wa chama hiki.

Katika mazingira haya nyumba ya Kikwete inayumba. Inatikisa na muda si mrefu inaweza kuanguka. CCM kimeshindwa kurudi katika misingi yake ya asili ya TANU ambayo imekataza rushwa kwa vitendo.

Kutokana na hali hiyo, kamati hii inatarajiwa kukutana na mengi. Hata kazi yake inaweza kujikuta inakataliwa.

Miongoni mwa wajumbe watatu wa kamati ni Mwinyi tu ambaye hana maslahi. Msekwa aligombea nafasi ya uspika na Sitta na Kinana anatajwa kutamani ukatibu mkuu wa CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: