Nyumba ya Kikwete inavuja; naye amekaa kimya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version

UTAWALA wa Rais Jakaya Kikwete umegawanyika. Wengine wanasema umeshindwa kazi.

Mawaziri na watendaji wake si wamoja tena; wengine wamo kama hawamo na tayari wananchi wameligundua hilo, na wameanza kuhoji maswali mengi. Hebu nasi tuulize.

Tumuulize na Rais Kikwete mwenyewe. Ziko wapi sifa na majigambo ya wapambe wa Kikwete waliyoyatoa kabla ya kuingia madarakani?

Wako wapi wanamtandao, waandishi wa habari na viongozi wa dini waliokuwa mstari wa mbele kumpamba Kikwete na kusema yeye ni "chaguo la Mungu?"

Iko wapi kauli mbiu ya "Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya," ambayo Kikwete na wapambe wake walihubiri Mashariki na Magharibi, Kaskazini na Kusini, mchana hadi usiku?

Wako wapi wale waliokuwa wanamfananisha Kikwete na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere?

Wako wapi wale waliotunga kitabu na kumuita Kikwete "Tumaini Lililorejea?" Yuko wapi Salma Kikwete aliyezunguka nchi nzima na kusema kuwa "chini ya utawala wa Kikwete, Tanzania yenye Neema inakuja?"

Kiko wapi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichowambia wananchi kinawaletea mgombea kijana ili kuleta nguvu mpya katika uongozi wa kitaifa?

Yako wapi maisha bora tuliyoahidiwa na Kikwete? Yuko wapi Kikwete aliyeahidi kumaliza mpasuko wa kisiasa wa visiwani Zanzibar na Pemba?

Ziko wapi sifa alizomwagiwa kwa kauli tamutamu katika siku za kwanza za uongozi wake? Ziko wapi ahadi kemkem za kampeni? Ziko wapi ajira milioni moja?

Iko wapi nguvu ya kupambana na rushwa katikati ya wimbi hili la ufisadi unaowahusu watawala wenyewe?

Au tuseme rais Kikwete ameyasahau haya yote? Ina maana hajui nchi inavyodidimia huku watawala wenzake wanatanua?

Au yale yalikuwa maneno ya 'kisisasa tu' yasiyo na maana kwa maisha halisi ya Watanzania?

Haya ni badhi tu ya maswali ambayo wananchi wanahoji: Wanasema rais Kikwete amewatupa mkono. Na kubwa linalozungumzwa hapa, ni suala zima la ufisadi na jinsi serikali inavyopambana nalo.

Wengi wao wanaona serikali kama vile inafanya usanii. Hakuna tena umakini ulioahidiwa. Madai ya wananchi yanapata nguvu zaidi kutokana na mikanganyiko ya kauli na utendaji kazi wa wasaidizi wa rais.

Kwa mfano, kila mmoja anajua kwamba fedha zilizokwapuliwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni mali ya serikali.

Lakini Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, ameliambia Bunge kwamba mabilioni hayo hayaihusu serikali wala umma kwani yalikuwa ya wafanyabiashara.

Mkullo alitoa kauli hiyo wakati akifanya majumuisho ya hotuba yake ya bajeti bungeni mjini Dodoma, wiki mbili zilizopita.

Na hata pale alipofanya kile alichoita, "ufafanuzi wa alichokisema," Mkullo aliendelea kung'ang'ania kwamba "fedha za EPA hazikuwa za umma."

Wala Waziri Mkullo hakujihangaisha kujihoji: Kama fedha hizi si za serikali, kwanini bosi wake aliunda Tume na kutumia mabilioni ya shilingi ya wananchi kwa kitu ambacho si cha serikali?

Kwa nini serikali imeagiza kufanyika ukaguzi tena kwa kutumia makampuni ya nje? Je, serikali ya Tanzania inakerwa nini na mali ya watu binafsi tena raia wa nchi nyingine?

Si hivyo tu, Mkullo hakujiuliza: Kama fedha hizi si za serikali, kwa nini makampuni yaliyofanya ukaguzi Dolleite & Touche na Ernst & Young, yalilipwa na serikali tena kwa kutumia fedha za wananchi?

Je, nini kimesukuma serikali hadi kuamua kutumia nguvu na rasilimali zake kwa jambo ambalo si lake? Kuna nini EPA?

Bila shaka kama Mkullo angejiuliza maswali hayo, asingetoa majibu aliyoyatoa. Angesema wananchi wavute subira, ili kazi inayofanywa na tume ya rais ikamilike.

Vinginevyo, Mkullo aseme kuwa alitumwa na Kikwete kusema aliyoyasema ili kuchokoza hisia za wananchi; aseme kwamba serikali ina mkakati madhubuti wa kuficha ufisadi ndani ya EPA.

Angalau Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na kwamba ametoa majibu ya jumla mno, ametoa wito kwa wananchi kuvuta subira.

Ameahidi serikali kuweka wazi uchunguzi wake - ingawa imeficha taarifa ya uchunguzi uliotangulia.

Lakini wapo wanaosema hivyo ndivyo serikali ya Kikwete inavyofanya kazi zake. Kwamba kila mwenye mamlaka ya kusema anasema na anatenda atakacho.

Ndiyo maana kauli ya Mkullo inapishana kwa mbali na kauli ya Kikwete mwenyewe aliyoitoa kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Akiongea na waandishi wa habari, Ikulu 8 Januari 2008, Luhanjo alisema kwamba serikali haiwezi kuendelea kuona fedha zake zinakwapuliwa na wajanja wachache, huku yenyewe ikiendelea kuuchapa usingizi.

Hakika, hata kama fedha za EPA zingekuwa si za serikali, bado ni jukumu la serikali kulinda fedha za wananchi wake.

Kitendo cha kutofahamika kwa wadai halali wa fedha hizo, hakiwezi kuhalalisha uporaji huo. Kutokana na hali hiyo, serikali ilikuwa na njia mbili tu za kufanya.

Moja, kurudisha fedha hizo kwa wale waliozikopa ambao ndiyo walioziweka NBC, au kuzibakiza BoT na kuzigantaza kuwa ni fedha za umma.

Kushindwa kwa serikali kufanya hivyo, na badala yake ikaamua kuzikwapua fedha hizo na kuzigawa kwa washirika wake kwa malengo inayoyajua yenyewe, hakuwezi kunyamaziwa.

Pamoja na madai kuwa sehemu kubwa ya fedha za EPA ilitumika kwenye kampeni za CCM na Kikwete, serikali haikupaswa kusema ilichosema.

Kwa vyovyote vile kauli ya Mkullo, imelenga kupunguza au kuondoa uzito wa jinai katika wizi huo. Hilo ndilo lililolengwa.

Lakini bado ukweli unabaki palepale, kwamba waliochotewa fedha hizi walitumia nyaraka za bandia. Walifanya jinai. Na hili linafahamika wazi.

Yapo mengine mengi ambayo wasaidizi wa Kikwete wanayapotosha, tena kwa makusudi.

Hata Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, pamoja na kupewa dhamana ya kuzungumza kwa niaba ya Rais Kikwete, hana msaada kwake.

Salva wala hajisumbui kutoa majibu yanayokidhi mahitaji ya wakati. Anaishia kupiga soga. Mifano ya kauli zake ipo mingi.

Michache ni mahubiri ya majuzi, kwamba eti ushirikina unaotajwa na vyombo vya habari kufanyika bungeni, unatishia wawekezaji kutoka nje.

Sijui ni lini, watawala wetu wameanza kuamini ushirikina. Na wala haijafahamika kama wawekezaji wa kigeni, wanaamini ushirikina.

Wala Salva hazungumzii mipango ya serikali katika kuinua uchumi. Hazungumzii mkakati wa serikali katika kupambana na rushwa na ufisadi, ingawa mipango hiyo imefungiwa katika makabati na sasa iko hatarini kutafunwa na mchwa.

Wala Salva hasemi chochote kuhusiana na ahadi za Kikwete alizozitoa kabla ya kuingia madarakani.

Hasemi kuhusu kilimo, hazungumzii wakulima wa korosho na ukopwaji wa mazao yao. Hazungumzii njaa inayotishia taifa.

Hayo hasemi, badala yake anaishia kuhubiri ushirikina. Sijui Salva alikuwa wapi wakati ule kijana anayetuhumiwa kukata vichwa vya watu, alipokuwa anadaiwa kufanya matendo hayo.

Hili ndilo jambo ambalo lilikuwa hadharani na linafahamika kwa wengi. Hata ndani ya chama cha Kikwete, CCM, hali ni hiyohiyo.

Wakati Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba akitoa wito kwa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kurudi katika meza ya mazungumzo, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), Francis Isack, alitangaza vita dhidi ya viongozi wa CUF.

Alifikia hatua hata ya kumuita mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa ni 'profesa wa mitishamba.'

Na kwa kuwa ndani ya CCM kila mmoja ana ndevu, hakuna aliyejitokeza kusahihisha hayo.

Sasa ikiwa serikali inaendeshwa kwa namna hii, wananchi washike nini tena? Je, ni kweli kuwa serikali ya Kikwete bado ina ubavu wa kupambana na rushwa na ufisadi ulioshamiri kila kona ya nchi?

Kama inaweza, mkanganyiko huu wa kauli unatokana na nini? Mbona hata ndani ya bunge kila waziri anakuja na jibu lake kwa swali lilelile moja?

Huyu anasema hivi, yule anasema vile. Je, ule utaratibu wa serikali kuwa na kauli moja na kufanya kazi kwa pamoja, umekwenda wapi?

Na haya yanafanyika mbele ya macho ya rais. Lakini bahati mbaya rais mwenyewe si tu kwamba yuko kimya, bali anashindwa hata kukemea wasaidizi wake.

Wapo wanaotania kuwa kushindwa kuchukuliwa hatua kwa mambo ya msingi kunatokana na Kikwete kuwa 'bize na safari za nje.'

Minong'ono ya mitaani inasema ukwapuaji katika EPA umewahusisha wengi. Hata Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anatajwa kufahamu kinagaubaga mkakati wake.

Rais Kikwete naye hatupwi mbali. Na hili linathibitishwa na mtiririko wa matukio ulivyokuwa.

Ukwapuaji umefanyika katika kipindi cha mwisho cha utawala wa Mkapa. Ni wazi kwamba Mkapa, akiwa mkuu wa nchi, lazima alijua. Ni kipindi hicho ambacho Kikwete alikuwa anatafuta madaraka.

Kuna kila dalili kwamba ndani ya ofisi ya rais kuna udhaifu mkubwa. Inawezekana, ama wasaidizi wa rais hawamshauri vema bosi wao, au bosi wao hashauriki. Na hili linathibitishwa na mambo mengi yaliyokwishafanyika.

Kwa mfano, inawezekana kabisa kuwa Kikwete na wasaidizi wake muhimu, hawakusoma taarifa kamili ya uchunguzi wa EPA.

Maana ripoti hii alikabidhiwa kwa rais tarehe 7 Januari 2008, na siku hiyohiyo akaondoka kwenda nje ya nchi.

Siku moja baadaye Luhanjo, alisoma sehemu ya ripoti hiyo kwa wananchi na kutangaza hatua ambazo rais amechukua.

Miongoni mwa hatua hizo, ni ile ya kumfukuza kazi gavana wa BoT, Daudi Ballali.

Rais Kikwete, kupitia kwa Luhanjo, alisema Ballali ameliabisha taifa na kwamba serikali imeamua kumfuta kazi.

Wakati Kikwete anatoa kauli hiyo, tayari Ballali alishajiondoa katika kiti chake. Na kibaya zaidi, sasa Ballali hatunaye tena duniani.

Umuhimu wa Ballali katika sakata hili unafahamika. Taarifa zinadai kwamba ni Ballali aliyekuwa akipokea vimemo na kushiriki mikutano ya kupanga jinsi ya ukwapuaji wa fedha hizo.

Ukweli au uwongo wa jambo hili amekufa nao Ballali mwenyewe.

Tukichanganya na taarifa tata kuhusu kifo cha Ballali, tunaona kwamba serikali imeshindwa kutaja wahusika na kuwachukulia hatua.

Serikali sasa ina mkakati wa kuanzisha porojo mpya kufukia hoja ya msingi na kulea ufisadi. Katika hali hii, wananchi wataendelea kujiuliza: "Huyu ndiye Kikwete tuliyeambiwa?"

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: