Nyumba ya Kikwete yazua utata


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete anatuhumiwa kuchukua nyumba ya mkazi mmoja wa Dar es Salaam na kuigeuza yake, MwanaHALISI limeelezwa.

Nyumba hiyo ipo kiwanja Na. 64, chenye eneo la futi za mraba 23,239 kwenye makutano ya barabara za Ursino na Migombani eneo la Mikocheni, Dar es Salaam.

Hii ni nyumba ambamo wamekuwa wakikaa maofisa wa ngazi za juu serikalini, lakini warithi wanadai Kikwete ameibomoa, kujenga upya na “kijimilikisha.”

Nyumba hii, kwa mujibu wa warithi ni mali ya Amirali Abdulrasul Alarakhia Dewji na Yusufali Kassamali Remtula Parpia, ambao wote ni marehemu.

Mmoja wa warithi ni Amirali Yusufali Parpia ambaye anawakilishwa na kampuni ya mawakili ya H.H. Mtanga & Co. Advocates ya Dar es Salaam.

Kwa kuwa nyumba hii imekuwa ikikaliwa na maofisa wa serikali; na kwa kuwa sechi kuhusu mmiliki wa kiwanja ya 22 Julai 2002 bado inaonyesha kuwa wamiliki ni walewale; warithi wanapanga kuifikisha serikali mahakamani kwa kubomoa nyumba yao.

Tayari mawakili wa warithi wameitaarifu serikali juu ya kusudio la kuifikisha mahakamani wakati wowote kwa kushindwa kujibu madai ya wateja wao.

Kwa mujibu wa kampuni ya mawakili, siku 90 ambazo waliipa serikali kujibu madai ya mteja wao zilimalizika Aprili 17, “Tunaweza kwenda mahakamani wakati wowote.”

Hivi sasa Rais Kikwete na familia yake wanaishi Ikulu, Magogoni, lakini kabla ya kupata madaraka ya urais mwaka 2005, alikuwa akiishi katika nyumba hiyo kwa takriban miaka 15 akiwa mtumishi wa serikali.

Nyaraka za karibuni zaidi zilizoko ofisi ya Msajili wa Hati wa serikali, zinaonyesha kuwa eneo hilo linamilikiwa na Amirali Abdulrasul Alarakhia Dewji na Yusufali Kassamali Remtula Parpia.

Hata sechi ya awali ya kiwanja hicho ya 22 Agosti 1982 iliwataja wamiliki kuwa haohao, Dewji na Parpia.

Bali sechi nyingine ya wizara juu ya kiwanja hichohicho ya 5 Novemba 2010 inasema, pamoja na mambo mengine, kuwa imeshindikana kupata rekodi zinazoonyesha mmiliki wa kiwanja hicho.

Barua ya Msajili wa Hati ya November 2010 na kusainiwa na Bumi F. Mwaisaka, inasema “…msajili amekuwa katika mchakato wa kutafuta nani hasa ni mmiliki wa kiwanja hicho…lakini tumeshindwa kupata rekodi muhimu kuhusu eneo husika.”

Malalamiko dhidi ya miliki ya “nyumba ya Kikwete,” yalianza kuchomoza Septemba mwaka jana pale kampuni ya uwakili ya H.H Mtanga ilipoandika barua kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo wa Serikali (TBA), Makumba Kimweri, kuuliza mazingira ya ujenzi mpya uliokuwa ukifanywa katika kiwanja Na. 64.

“Kwa masikitiko makubwa, tunaona ujenzi mpya ukifanyika katika eneo hilo bila ya kuwapa taarifa wamiliki wa eneo. Naomba utupe taarifa kuhusu ujenzi huo ili tujue la kufanya,” ilisema sehemu ya barua ya mawakili, Kumb. Na. MT/MISC/1/Amira/10/1 ya 8 Septemba 2010.

Kimweri akijibu hoja hiyo ya mawakili alisema, kupitia barua ya 29 Septemba yenye Kumb. Na. GB: 2/228/01/56, kuwa “ujenzi unaofanyika ni kwa maslahi ya serikali na hakukuwa na sababu ya kumtaarifu mteja wako.”

Kimweri anasema katika barua ambayo MwanaHALISI imeiona, “…kwa mujibu wa rekodi zilizopo, nyumba inayozungumziwa ilikuwa mali ya serikali tangu Juni 1961 na imekuwa ikitumiwa na maofisa wake waandamizi tangu wakati huo.

Kauli ya Kimweri inagongana na sechi ya serikali Na. 1871/2002 inayosema kiwanja kina miliki kwa miaka 99 kuanzia tarehe 1 Julai 1963 na kwamba ni mali ya wamiliki Dewji na Parpia.

Katika mazingira ambamo ofisi moja ya serikali inasema kiwanja ni mali ya serikali; huku nyingine ikisema ni mali ya Dewji na Parpia; na katika mazingira ambamo Kikwete anadaiwa kubomoa nyumba ya wadai na kuijenga upya, uwezekano wa serikali kufikishwa mahakani ni wazi.

Barua ya kampuni ya mawakili, Kumb. Na. MT/MISC/DEWJI/PHRPI/2011/1, ambayo inataarifu juu ya kusudio la kushitaki serikali, ilipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishina wa Ardhi.

Ubomoaji na ujenzi mpya wa nyumba inayolalamikiwa, ulifanywa baada ya Kikwete kuingia madarakani.

Warithi wa wamiliki wa eneo hilo wanadai kuwa tathmini waliyofanya inabainisha kuwa nyumba iliyobomolewa inafikia thamani ya Sh. 600 milioni.

Akizungumza na MwanaHALISI jijini Dar es Salaam hivi karibuni, mmoja wa mawakili wa kampuni hiyo, Abdallah Mtolea, alisema wanajiandaa kwenda mahakamani wakati wowote mwezi huu.

“Tumejaribu kufanya mawasiliano yote hayo na serikali kupitia Wakala wa Majengo wa Serikali lakini tunaona hatupati ushirikiano. Hili jambo linaweza kuzungumzika ikizingatiwa kuwa mheshimiwa rais (Kikwete) anatarajiwa kuishi pale mara atakapostaafu urais,” alisema Mtolea.

Baadhi ya majirani wa Kikwete waliozungumza na gazeti hili, wamesema Kikwete ameishi katika nyumba hiyo katika kipindi chake chote cha utumishi serikalini.

Kabla ya hapo, nyumba hiyo inadaiwa kukaliwa na waziri mstaafu, Edgar Maokola Majogo.

Hadi sasa hakuna hati zinazoonyesha kuwa nyumba au kiwanja husika ni mali ya serikali. Aidha, gazeti hili halikuweza kupata ushahidi wa Rais Kikwete kununua kiwanja hicho kutoka kwa wamiliki wanaotambulikwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.

Iwapo kesi hii itafunguliwa mahakamani, itakuwa kivutio kikubwa wakati huu ambapo masuala ya ufisadi yamekuwa ajenda muhimu ya upinzani na asasi za kijamii.

0
Your rating: None Average: 3.3 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: