Obama, Sarkozy walivyomsengenya Netanyahu


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly version

NI jambo la kawaida kwa viongozi wa nchi wanapokutana kwa mazungumzo ya faragha kuanza kuwateta na kuwasengenya viongozi wengine ambao hawapo, iwapo masengenyo hayo yanabakia kuwa siri ya wanaokutana.

Lakini linakuwa jambo zito iwapo, kwa mfano viongozi wawili wa nchi wanapokutana kwa mazungumzo ya faragha kumsengenya kiongozi mwenzao ambaye hayupo na kumwita muongo wa kupindukia.

Uzito unazidi hasa pale nchi hizo tatu wanazoziongoza ni marafiki na washiriki wakubwa katika masuala mbali mbali ya kisiasa na ya kiitikadi duniani.

Na suala zima linakuwa kashfa pale misengenyo yao hiyo inaponaswa na vyombo vya habari na kuingia hadharani.

Hivyo ndivyo ilivyotokea wiki iliyopita pale Rais wa Marekani, Barack Obama na mwwenzake wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy walipokutana nchini Cannes, Ufaransa kwenye mkutano wa nchi 20 tajiri duniani (G20).

Wawili hawa wanaongoza nchi ambazo ni mihimili mikuu wa nchi za Magharibi, kiuchumi na kijeshi. Kwenye vikao vya mkutano huo wa G20, Obama na Sarkozy walikutana kwa mazungumzo na waandishi waandamizi wa habari wa Kifaransa.

Baada ya mkutano na waandishi wa habari viongozi hao waliamua kuongea wenyewe kwa faragha, hivyo wakawataka waandishi hao wa habari waondoke kutoka chumba walichokuwa wamekutania.

Lakini kwa bahati mbaya (au nzuri) waandalizi wa mkutano wao huo walisahau kukizima kifaa kwenye vinasa sauti (microphone) ambazo zilikuwa zimeunganishwa (bila waya) kwenye video recorder za waandishi.

Hivyo walipokuwa chumba cha pili, waandishi waliweza kuona na kusikia laivu kabisa baadhi ya mazungumzo kati ya Obama na Sarkozy. Kiongozi waliyekuwa wakimsengenya ni Benjamin Nyetanyahu, Waziri Mkuu wa Israel ambaye hakuwapo. Israel ni swahiba mkubwa wa Marekani na Ufaransa.

Sehemu ya mazungumzo ilisema:

Sakorzy: Nashindwa kumvumilia Nyetanyahu. Ni muongo kupindukia!

Obama: Unasema umechoka naye? Nihurumie mimi ambaye inanibidi nishughulike naye kila siku!

Haya na mengine yalinaswa na waandishi hao wa Kifaransa waliokuwa chumba cha pili na walijikuta hawajui wafanye nini.

Waandishi hao waandamizi hawakuweza kuitangaza kashfa hiyo mara moja kwa sababu walikuwa ni maswahiba wa walio madarakani kwa hivyo iwapo kashfa hiyo ingevuja wangejulikana ni wao mara moja, na wangejiharibia kazi zao kwani huko kwa wakubwa ndiko huwa wanapata zile ‘scoop’ zao za kuandika.

Lakini hata hivyo kuna mmoja kati yao aliyaingiza mazungumzo hayo ya video (U-Tube) na kwa maneno kwenye blogu moja na huko ndiko vyombo kadhaa vya habari vilipoipata kashfa hiyo na kuanza kuitangaza kwa kasi.

Kashfa hii ilionekana kuleta hali ya mtafaruku baina ya nchi za magharibi na Marekani, hasa pale ripoti ya Wakala wa Usimamizi wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ilikuwa inasubiriwa ilipokuwa inakaribia kutoa ripoti yake kali dhidi ya Iran kuhusu maradi wake wa nyuklia.

Ikumbukwe kwamba Iran ina uhasama mkubwa na Israel katika eneo hilo na mara kadha taifa hilo la Kiyahudi limekuwa likitoa vitisho vya kuishambulia Iran kutokana na mradi huo unaodaiwa kuwa ni wa kutengeneza zana za nyuklia kwa lengo la kuiangamiza Israel, dai ambalo daima Iran imekuwa ikilikanusha.

Na kuongezea chumvi kwenye donda, kashfa hiyo ya kumsengenya Netanyahu ilikuja siku chache tu baada ya Waziri Mkuu (Chancellor) wa Ujerumani alipoliambia baraza lake la mawaziri kwamba “kila neno litokalo kwa Netanyahu ni la uongo.”

Mara kadha uhusiano kati ya Marekani na Israel umekuwa ukikumbwa na misukosuko lakini si kama kwa suala kama hili. Maafisa wa nchi zote hizo tatu (Marekani, Ufaransa na Israel) mara kwa mara hutamka kwamba uhusiano baina ya nchi zao ni mzuri na kwamba Israel daima huiona Ufaransa ni nchi rafiki.

Lakini pamoja na hilo, kauli hiyo ya Sarkozy pia ni kielelezo kinachoonyesha hali isiyoridhisha kuhusu kushindikana kwa kuanzisha tena mazungumzo ya amani baina ya Palestina na Israel na hivyo kusababisha hali ngumu na malumbano yasiyo ya lazima ndani ya Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Palestina kujiunga na Umoja huo na mashirika yake.  
Aidha huko nyuma kumekuwapo na misuguano kati ya Obama na Netanyahu hususan katika suala na kuendelea kwa Israel kujenga makazi ya Wayahudi katika maeneo ya Jerusalem ya Mashariki na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa ujumla taarifa za kusengenywa kwa Netanyahu zimekuja wakati ambapo Wizara ya Nje ya Marekani imetangaza kwamba wapatanishi kutoka Marekani, nchi za Ulaya ikiwemo Russia pamoja na Umoja wa Mataifa watakutana kwa mikutano tofauti na maafisa wa Israel na Palestina kujadili namna ya kuanzisha tena mazungumzo ya amani.

Isitoshe, Ufaransa wiki mbili zilizopita ilipiga kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuruhusu Palestina kujiunga na UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni), huku Marekani na Israel yenyewe zikipinga.

Hatua hiyo moja kwa moja imeipelekea Marekani kukata misaada yote kwa shirika hilo, kutokana na azma yake iliyotoa katka miaka ya 90 iwapo kitu hichi kingetokea.

Maafisa wakuu wa nchi zote tatu hawakuweza kuzungumzia tukio hilo la Obama na Sarkozy la kumteta Netanyahu lakini afisa mmoja wa Israel juzi alisikika akimwambia mwandishi mmoja wa habari kwamba suala hilo ni la Sarkozy na Natenyahu na siyo la Obama na Netanyahu.

Na msemaji mmoja wa Wizara ya Nje wa Ufaransa baada ya kubanwa na waandishi wa habari alisema: “Nadhani suala lote hili lisitufanye kupoteza lengo letu na hasa katika mambo muhimu – ambayo ni kwamba hakuna kupoteza hata dakika moja katika kuendelea kulishughulikia suala la mgogoro kati ya Israel na Palestina.

0
No votes yet