Ofisi ya Mwakyembe hatari


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

OFISI ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe imetelekezwa, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema tangu Septemba mwaka jana, ofisi hiyo imekuwa tishio kwa wafanyakazi kutokana na Dk. Mwakyembe kutamka kuwa “matatizo yake ya ugonjwa unaomsibu yalianzia ofisini.”

Ofisi ya Dk. Mwayembe ipo ghorofa ya pili kwenye jengo la Holland, Barabara ya Samora, katikati ya jiji la Dar es Salaam. Katika jengo hilo ndipo pia zilipo ofisi za Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, hata inapotokea kunahitajika kitu ndani ya ofisi ya Dk. Mwakyembe, hakuna mtumishi aliyetayari kuingia na kuchukua kitu hicho.

“Imekuwa shida sana kwa wafanyakazi. Huwezi kuamini kwamba hakuna aliye tayari kuingia ofisini kwa mheshimiwa Mwakyembe,” amesema mtoa taarifa.

Taarifa za ndani ya wizara hiyo zinasema wafanyakazi wameogopa ofisi hiyo baada ya baadhi yao kuhojiwa na maofisa usalama waliokuwa wakichunguza madai ya Dk. Mwakyembe kwamba ugonjwa wake ulianzia ofisini kwake.

Imeelezwa kuwa wafanyakazi wamehojiwa kwa siri kubwa na katika nyakati tofauti ndani ya jengo hilo la wizara.

Mtoa taarifa amesema miongoni mwa watumishi waliohojiwa na maofisa hao –  makachero wa polisi na usalama wa taifa – ni wale wanaofanya kazi ofisini kwa Mwakyembe.

Hawa ni katibu binafsi wa naibu waziri Dk. Mwakyembe, katibu muhtasi wake na wahudumu wawili.

Mmoja wa viongozi wa wizara hiyo amesema, “Haya yote kayasababisha Dk. Mwakyembe mwenyewe… anazungumza sana, ndiyo maana watu wameona kwamba wakae kando na ofisi yake.”

“Angetulia na kusubiri uchunguzi. Tunalojua sisi ni kwamba anaumwa ugonjwa wa ngozi. Tusubiri majibu maana nadhani atarejea wiki ijayo.”

Mtoa habari anasema wanadai kuwa ugonjwa ulitokana na sabuni na taulo. “Kama hivyo ndivyo vyanzo, mbona hakuvibeba?” anahoji.

Anasema iwapo vitu hivyo vilidhaniwa kuwa tatizo vingechukuliwa na wapelelezi kwa ajili ya uchunguzi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert Mrango alisema juzi kwa njia ya simu, “Aah, umepata wapi hayo mambo? Ni mambo mazito wizarani kwangu.”

“Ni vigumu kulizungumzia suala hili kwenye simu. Mimi nipo nje ya jiji kwa sasa,” alisema baada ya kuulizwa iwapo taarifa kuwa wafanyakazi wa wizara hiyo wamehojiwa ni za kweli.

Balozi Mrango alisema wakati anapigiwa simu, alikuwa kwenye shughuli za ufunguzi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Mwisho, Barabara ya Morogoro nje kidogo ya Dar es Salaam.

MwanaHALISI lilitaka kupata kauli ya katibu mkuu juu ya ofisi hiyo ya Dk. Mwakyembe sambamba na ripoti iliyoko Wizara ya Ujenzi kuhusu kuugua kwake ambako alidai kulianzia ofisini hapo.

Dk. Mwakyembe, mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya, anaumwa na ugonjwa wake  haujatolewa taarifa za kina. Kwa sasa amerejea nchini India kuendelea na matibabu.

Hiyo ni mara ya pili kwenda India. Mara ya kwanza ilikuwa 10 Oktoba 2011, alipoondoka baada ya kubainika tatizo la ngozi yake kuanza kutoka ungaunga, huku nywele zikinyonyoka.

Kumekuwa na uvumi kuwa ugonjwa unaomsumbua ulisababishwa na kulishwa sumu.

Madai hayo yalianza kutolewa na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye aliwahi kumtembelea hospitali ya Apollo iliyoko Hyderabad, India.

Baadhi ya magazeti nchini yalichapisha picha iliyoonyesha Sitta akiwa pembeni mwa kitanda cha Dk. Mwakyembe. Sitta ni mbunge wa Urambo Mashariki na spika wa bunge lililopita.

Sitta anasema, “Ushahidi wangu ni wa kimazingira. Haiwezekani kuugua ngozi kiasi cha kuvimba na ikitokea kujikuna inamwaga unga.”

Sitta alisisitiza hilo alipohudhuria ibada maalumu katika kanisa la Wokovu na Ufufuo, Kawe jijini Dar es Salaam miezi miwili iliyopita.

Hata hivyo, hivi karibuni, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba alikaririwa akisema kuwa Dk. Mwakyembe “hakulishwa sumu…”

Manumba alidai kuwa alipata taarifa hiyo kutoka wizara ya afya ambayo alidai pia kuwa iliwasiliana na hospitali alikolazwa Dk. Mwakyembe.

Baada ya taarifa hiyo kutoka, Dk. Mwakyembe alitoa kauli ya kupingana na DCI Manumba.

Alisema, "Napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu.”

“Alichokisema hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya hospitali inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow (uboho) kinachochochea hali niliyonayo,” alieleza Mwakyembe.

Nao mawaziri wawili, akiwamo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, wamekana kauli ya Manumba.

Dk. Mponda amekaririwa akiwaambia waandishi wa habari, “Muulizeni DCI Manumba awape ufafanuzi…lakini wanaoweza kuzungumzia maradhi ya Dk. Mwakyembe ni familia yake au yeye mwenyewe mwenye ripoti…”

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema uchunguzi wa afya ya Dk. Mwakyembe bado unaendelea na kwamba ni yeye atakayetangaza matokeo.

Waziri Nahodha ambaye kikazi anasaidiwa na viongozi wa idara mbalimbali ndani ya jeshi la polisi, alijitenga na kauli ya DCI Manumba.

“Mimi ndiye waziri; nasema uchunguzi bado unaendelea na mimi ndiye nitatangaza hitimisho la jambo hilo,” ameeleza Nahodha.

Alionya kuwa “…wanaolifanya suala hili kuwa jepesi wanachezea kitu hatari.”

Gazeti hili liliripoti wiki mbili zilizopita kuwa Rais Jakaya Kikwete alitoa taarifa ya ugonjwa wa Dk. Mwakyembe kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri.

Akizungumzia utaratibu wa urejeshaji wa ripoti kwa wagonjwa wanaotibiwa nje ya nchi kwa gharama za serikali, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli amesema ripoti hizo hupelekwa wizarani hapo.

“Technical Report – ripoti ya kiufundi –  huletwa wizarani na kuwekwa kwenye faili la mgonjwa. Mganga Mkuu na watalaam wake ndio huisoma na kuona ni hatua gani zinazofuata kwa mgonjwa huyo. Mgonjwa mwenyewe hupewa summary (muhutasari) ya ripoti,” alisema Kikuli.

Alipoulizwa iwapo ripoti ya Dk. Mwakyembe imefuata hatua hizo, alisema yeye hajaiona na inawezekana ilipoletwa alikuwa hajateuliwa kukaimu nafasi hiyo.

Kikuli anakaimu nafasi iliyoachwa na Blandina Nyoni aliyesimamishwa kazi kutokana na mgomo wa madaktari.

Alipobanwa zaidi aeleze iwapo ripoti ya Dk. Mwakyembe ilikuwa wizarani na kwamba ndio waliitoa kwa polisi, alisukuma mpira kwa Afisa Habari wa Wizara, Nsachris Mwamwaja.

Hata hivyo, Mwamwaja alipoulizwa alisema, “Ripoti hiyo inakuwa mali ya mgonjwa.”

Alisema wizara inaweza tu kupewa nakala ya ripoti ikiwa watahitaji kama kuna jambo maalumu. “Tukitaka nakala anaweza kutuletea kama kuna vitu maalum,” alisema.

Kuhusu ripoti ya Mwakyembe alisema, kama waziri ameshasema hajaiona, “unataka mimi nisemeje? Ninachoweza kusema ni kwamba ripoti ni ya mgonjwa, sisi wizara tunaratibu tu safari yake,” alisema Mwamwaja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: