OIC kumlipukia Membe


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 July 2009

Printer-friendly version
Wabunge waandaliwa kumsulubu
Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe

HOJA ya kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Duniani (OIC) huenda ikazikwa mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, MwanaHALISI limegundua.

Taarifa kutoka Riyadh, Saudi Arabia; London, Uingereza; na New York, Marekani; zinasema kuingia kwa mataifa makubwa katika umoja huo kumezua utata na migogoro ambayo "imetibua hadhi ya OIC ambayo wengi walitaka kujiunga nayo."

Taarifa za kibalozi na mashirika ya habari zinasema, hata hivyo, kwamba wimbi la kutaka kujiunga na OIC limepungua nguvu kutokana na ushindani wa mataifa makubwa kujipenyeza kwenye taasisi hiyo, wengine wakihofu kwamba ni kwa "shabaha ya kuudhoofisha."

Awali nchi masikini na zile zenye uchumi wa kati zilijiunga na jumuia hiyo kwa malengo ya kupata misaada mbalimbali, wakati mengine yalitaka kujitambulisha nayo kwa misingi ya madhehebu ya Kiislamu.

Tanzania imewahi kuwa na mjadala juu ya umuhimu wa kujiunga na OIC wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Alikuwa baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyezima mjadala huo na kujenga hoja kuwa Zanzibar iliyokuwa imejiunga, ilikuwa imekiuka katiba na kwamba kama ni uanachama, "basi inayojiunga ni Tanzania."

Tangu hapo mjadala wa kujiunga na OIC imekwenda kimyakimya hadi mapema 2006 wakati hoja hiyo ilipoanza kupamba moto upya ikienda sambamba na hoja ya Mahakama ya Kadhi nchini.

Suala la OIC linatarajiwa kuibuka kwa nguvu bungeni wakati Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe atakapowasilisha bajeti ya wizara yake Jumamosi.

Madai ya uanachama OIC yatakuwa makubwa kutokana na kauli ya serikali wiki mbili zilizopita, kuonekana kutotilia maanani suala la Mahakama ya Kadhi ambalo limepelekea baadhi ya viongozi wa Kiislam kuapa kutopigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Mjini Dodoma na hasa kwenye viwanja vya bunge, tayari kuna mvumo juu ya hatua ya baadhi ya wabunge kumkwamisha Membe iwapo hataonyesha uwezekano wa serikali kuruhusu kujiunga na OIC.

Membe, ambaye ameanza kuhusishwa na nia ya kugombea urais mwaka 2015, atakuwa na kibarua kigumu; hivyo atatakiwa kuwa mwangalifu katika kauli zake ili kupenyeza bajeti yake bila mikwaruzo.

Angalau wabunge watano (majina tunayo), ambao wanapiga chapuo kwa ajili ya watumainiwa wa ugombea urais mwaka 2015, wamekuwa wakijiapiza "kumpa Membe wakati mgumu."

Hata hivyo, wiki mbili zilizopita, Membe alionyesha ukomavu wa diplomasia pale alipokataa kujibu mashambulizi bungeni, akisema kwa vile suala lililoletwa na Mbunge wa Mchinga, Mudhihir M. Mudhihir linatokea mkoani kwao, basi atalipeleka kwenye vikao vya CCM vya mkoa.

Mudhihir alimtuhumu Membe kuathiri maamuzi ya ujenzi wa kiwanda cha saruji nje ya jimbo la Mchinga, akisema waziri huyo ni "nyoka kidimu."

"Katika hili, Membe ameonyesha ukomavu. Kulumbana hakuna maana, hasa unapokuwa na wadhifa kama alionao," ameeleza mmoja wa wabunge kutoka mkoani Lindi.

Suala la OIC litafuatia kauli ya Membe mwaka jana alipkuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake. Alisema, "hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na IOC" na kwamba ni suala linalojadilika.

Baadaye Oktoba mwaka jana, Membe alikaririwa akiwashangaa baadhi ya Watanzania kwa kile alichoita "kutoa kauli zinazoashiria kuiogopa OIC na baadhi ya nchi za Kiislamu."

Alikuwa akielezea hatua iliyofikiwa katika mazungumzo kati yake na Rais wa Iran, Mahmoud Ahmednejad iliyolenga kuomba nchi hiyo kufuta madeni inayoyadai Tanzania yapatayo zaidi ya Sh. 200 bilioni.

Membe aliwageuzia kibao waandishi wa habari na kuuliza, "Kwa nini tunashikwa na woga? Tukipewa msaada na Marekani tunaambiwa kuna mkono wa mtu; tukipewa na Iran tunaambiwa vivyo hivyo. Sasa niambieni mimi, kama Waziri wa Mambo ya Nje, niende wapi?"

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam amenukuliwa akisema, hakuna tena haraka ya kujiunga na OIC kwa vile tayari jumuiya hiyo imekumbwa na migogoro ya "wakubwa."

"Mimi siyo Mwislamu wala msemaji wa serikali, bali sioni umuhimu wa kujiunga na OIC kwa sasa; mataifa makubwa ya Marekani na Uingereza yamejiingiza huko ili kuiuwa. Kuna haja ya kuendelea kutafakari," ameeleza bila kutaka kutajwa jina gazetini.

MwanaHALISI haikuweza kumpata Waziri Membe wala naibu wake kwa kile msaidizi wake alisema "wana kikao kirefu."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: