OIC ni ajenda tata ya shinikizo la vizito


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 02 September 2008

Printer-friendly version

SERIKALI inasema imeanza Tanzania imeanza mchakato wa kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam Duniani (OIC) baada ya kuridhika kuwa hakuna madhara yoyote kwa kuwa hata zisizokuwa nchi za Kiislam, ni wanachama.

Tamko hilo limekuja miaka 14 tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoilazimisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kujitoa OIC kwa hoja kuwa haina mamlaka ya kujiunga na taasisi za kimataifa bila ya kupitia mgongo wa Jamhuri hiyo.

Ilipozuia Zanzibar kujiunga, Jamhuri iliahidi kutafiti jumuiya hiyo ili ikiwezekana Tanzania ndio ijiunge. SMZ ilisema hakukuwa na tatizo lolote kujiunga kwao na ilijiunga kwa sababu za kiuchumi zaidi kuliko nyingine. Hata hivyo ilijitoa.

Ingawa ilielezwa kulikuwa na upotoshaji wa malengo na majukumu ya OIC, ukweli ni kuwa OIC inajumuisha nchi za Kiislam, hata kama kuwepo kwa zisizokuwa nchi za kiislam – mfano mzuri Msumbiji na Uganda.

Uganda, kwa mfano, licha ya kudai ni nchi ya kisekula (isiyo na dini), uongozi wake una mwegemeo wa Kiislam tangu utawala wa dikteta Idi Amin, na ina uhusiano mkubwa na nchi za kihafidhina kama Libya na Saudi Arabia. Amin aliwahi kutangaza dhamira ya kuifanya Uganda taifa la kiislam.  

Msumbiji ilijiunga na OIC kwa lengo la kuukomoa Uzayuni ukiwakilishwa na Makaburu wa Afrika Kusini (enzi hizo), waliokuwa wakipinga harakati za ukombozi/maendeleo ya Msumbiji, na ambao ndio waliomuua Samora Machel, aliyekuwa rais wa kwanza wa Msumbiji huru, kwa kuitungua ndege aliyokuwa anasafiria kutoka mpakani mwake na Afrika Kusini.

Uzayuni wa Waisraeli ambao ni maadui wa kudumu wa nchi za kiislamu, na Makaburu wa Afrika Kusini ni ndugu wa damu.

Katika mkutano wa 15 wa OIC uliofanyika Sanaa, mji mkuu wa Yemen, 18 Desemba 1984 na kuhudhuriwa na wanachama 41 wa OIC, kati ya 45 wakati ule, moja ya ajenda kuu ilihusu harakati za kuikomboa Namibia, nchi iliyokabili utawala wa Makaburu baada ya kuachiwa na Wajerumani.

Kwanini sasa Namibia isijiunge OIC? Wahenga walisema vita havichagui silaha, hata zikitolewa na shetani. Sasa madhumuni ya OIC yapo wazi kwa Msumbiji, Uganda na nchi nyingine zisizokuwa za Kiislam.

Moja ya madhumuni ya OIC ni kuendeleza mapambano dhidi ya Israel na utamaduni wa Magharibi. Wanachama wa OIC wanataka Israel iondoke Jerusalem, kwa msimamo kwamba huo ni mji wa asili wa Wapalestina kama hatua muhimu ya kutambuliwa kwa taifa lao.

Tunajifunza hapa inawezekana sababu za kiuchumi zina msingi lakini lengo hasa ni kuendeleza Uislam na utamaduni wake dhidi ya ule wa kiharamia unaoongozwa na nchi za Magharibi, ikiwemo Marekani, unaoitawala dunia leo.

Kwa mfano, chini ya mwamvuli wa OIC, mambo ya biashara yanashughulikiwa na soko la pamoja – Islamic Common Market - ICM), linaloratibiwa na Kamati ya Kudumu ya Maendeleo ya Kiuchumi na Ushirikiano. Ni dhahiri hii ni taasisi dhidi ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) ambalo wanufaikaji wake wakuu ni nchi za Magharibi.

OIC pia inakusudia kuanzisha taasisi ya kifedha itakayorahisisha biashara katika soko linalojumuisha nchi wanachama wake. Taasisi hii inafanana na Economic Currency Unit (ECU) ya Umoja wa Ulaya.
 
OIC pia inapanga kuimarisha shughuli za Benki ya Maendeleo ya Kiislam (Islamic Development Bank, IDB) ikiwemo kusaidia masoko kwa bidhaa za nchi wanachama wake. Hii ni mfano wa American Export/Import (EXIM) ya Marekani.

Ajenda za OIC ni zaidi ya kuimarisha uchumi wa wanachama wake. Kama hoja ya Mahakama ya Kadhi inavyozidi kupamba moto nchini, ndivyo ilivyo nia ya OIC; kuona Mahakama ya Kimataifa ya Kiislamu ikianzishwa, na pia kuundwa kwa jeshi la kimataifa la nchi hizo, ambalo, pamoja na kupambana na ubeberu wa Kimagharibi, litatumika katika vita ya ukombozi wa Yerusalem “ –al-Quds”, kwa mujibu wa Azimio la Makkah.

Majeshi ya Marekani na washirika wake walipovamia Afghanistan baada ya tukio la 11 Septemba 2001, OIC ilipeleka watazamaji wa kijeshi kushuhudia madhara ya vita hivyo vilivyoua maelfu ya raia wasio na hatia. Afghanistan ni nchi ya Kiislam na mwanachama wa OIC.

Naona jamii ya Waislam duniani inakataa utamaduni wa dini hiyo kuingiliwa na hatimaye kumezwa na ule wa kimagharibi. Inataka sheria za Kiislam zitawale dhidi ya sheria za ki Magharibi katika nchi wanachama wake.

Wanataka kuona uchumi wenye mtizamo wa Kiislam ambao una desturi ya kuzingatia haki, usawa na uadilifu dhidi ya uchumi wa kiutandawazi unaochochea umasikini, ufisadi, uonevu na maovu katika jamii.

Wanaona usawa unaotangazwa kwa vazi la ubabe wa ki- Magharibi si lolote si chochote bali unaojenga wazungu pekee.

Jamii ya Kiislam na OIC wanakataa dhana ya usekula au mfumo wa maisha usiojali misingi ya Uislam. Hiyo ndio misingi na malengo ya OIC.

Barani Afrika, OIC inajaribu kueneza na kushawishi nchi kushiriki kampeni ya kupinga ustaarabu wa ki magharibi. Jumuiya ya Uislam Afrika (IOA), ambayo Tanzania ilikuwa mwanachama mwanzilishi mwaka 1988, inalenga hapo.

Moja ya matamko maarufu yaliyotolewa katika mkutano wa kwanza uliofanyika mwaka 1988 Abuja, mji mkuu wa Nigeria, lililaani masalia na athari ya ukoloni kwa jamii za Kiislam barani Afrika.

Wakoloni walikuja; wakaisambaratisha jamii ya Kiislam; wakaifuta shariah (sheria ya Kiislam) na wakaleta Sheria za Uingereza, kisha wakageuza watawaliwa makafiri kwa roho na kwa vitendo, lilisema tamko lao.

Mitizamo na matukio hayo hayawezi kuchukuliwa kulenga mahusiano ya kiuchumi ya kimataifa bila kukubali kuwa dini ni ajenda kuu miongoni mwa nchi wanachama wa OIC.

Sawa na suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, ndivyo inavyoonekana kwa harakati za Tanzania kujiunga na OIC. Ni sehemu ya mpango wa nchi kuingizwa katika vita baridi vya kiutamaduni kati ya mataifa ya Magharibi na mataifa ya Kiislam.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Tanzania ni taifa lisilo dini na kazi ya “kueneza dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”

0
No votes yet